Kaimu Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi
wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya. Jengo hilo lilifanyiwa ukarabati
Mkubwa uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.4 za kitanzania. Kazi ya
ukarabati huo ilifanywa kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Benki ya
Dunia ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020)
wa Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akiwasisitiza Watumishi wa Mahakama pamoja na Wananchi kufurahia tendo la Uzinduzi wa Mahakama wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo hilo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akishangilia baada ya kukata utepe kuzindua jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akioneshwa mfumo wa Mawasiliano uliofungwa kwa ajili ya ufuatiliaji wa Mashauri Mahakamani.
Baadhi ya Majaji pamoja na wageni wengine waalikwa wakiangalia mfumo wa Mawasiliano kwa njia ya Video (video conferencing) unavyofanya kazi. Katika uzinduzi huo, Kaimu Jaji Mkuu alizungumza na Waziri wa katiba na Sheria moja kwa moja akiwa mjini Dodoma. Mfumo huo umewekwa kwa ajili ya kurahisisha usikilizaji wa mashauri pamoja na kupunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Waziri wa katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi kupitia mfumo wa Mawasiliano kwa njia ya Video -video conferencing, (haupo pichani) wakati wa uzinduzi wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya.
Kikundi
cha kwaya maalum ya Watumishi wa Mahakama kanda ya Mbeya kikiingia kutumbuiza
wakati wa sherehe za uzinduzi wa wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya.
Kiongozi
wa Dini ya kikristo wa Dhehebu la Anglican akiwakilisha viongozi wengine wa
kikristo katika kuombea jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya lililozinduliwa na
Mhe. kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma jijini Mbeya.
Kiongozi
wa Dini Kiislamu akiomba dua kwa ajili ya jengo la Mahakama Kuu kanda
ya Mbeya lililozinduliwa na Mhe. kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim
Hamis Juma jijini Mbeya.
KITUO
JUMUISHI CHA UTOAJI HAKI CHAZINDULIWA MBEYA
Na
Lydia Churi-Mahakama MbeyaKaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezindua jengo la Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya ambayo inakuwa ni Mahakama kuu ya kwanza nchini kufanya kazi kama kituo jumuishi cha utoaji wa huduma za Mahakama.
Jengo la Mahakama Kuu
ya Mbeya lilifanyiwa ukarabati mkubwa ambapo baada ya kukamilika kwa ukarabati
huo, hivi sasa jengo hilo linajumuisha pia ofisi za wadau wa mahakama
wakiwemo Polisi, Magereza, na Ustawi wa
Jamii ili kurahisisha kazi ya utoaji haki.
Akizindua jengo hilo
mwishoni mwa wiki jijini Mbeya, Kaimu Jaji Mkuu alisema maboresho ya jengo hilo
ni hatua ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015/16-2019/20) wa Mahakama ya Tanzania ambao moja ya nguzo zake ni
kusogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi.
Alisema pamoja na
kuboreshwa kwa huduma za mahakama bado wananchi watapenda kuona wanahudumiwa na
watumishi wanaofuata maadili ya kazi zao hivyo aliwataka watumishi wa mahakama
nchini kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kutanguliza mbele utu.
Kaimu Jaji Mkuu alisema
kuzinduliwa kwa jengo hilo ni ishara kuwa mahakama ya Tanzania inabadilika na
kuachana na ujenzi wa kizamani wa majengo yake ambapo alisema sasa Mhimili huo
unajenga majengo yanayozingatia matumizi ya teknolojia ya habari na
mawasilianoa (TEHAMA) pia ambayo yatatoa nafasi kwa wadau wa Mahakama kuweka
ofisi zao ili kurahisisha suala la utaoji haki.
Aidha, Jaji Mkuu
ameiomba serikali kutenga fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa mahakama pale inapoanzisha
maeneo mapya ya kiutawala zikiwemo wilaya na mikoa ili kuisaidia mahakama
kuendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi.
Aliwaomba Wakuu wote wa
mikoa nchini pamoja na wakuu wa wilaya kuwa sehemu ya maboresho ya Mahakama kwa
kuwa wanategemewa kuratibu ustawi wa maendeleo ya wananchi hivyo basi viongozi
hao hawana budi kusimamia ipasavyo suala la amani kwa kutatua migogoro katika
jamii.
Kaimu Jaji Mkuu pia
aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika ujenzi wa mahakama nchini. Alisema
hivi sasa Taasisi hiyo imetoa wazo la kuanzishwa kwa Mahakama zinazotembea
(Mobile Courts ili kutimiza azma yake ya kusogeza karibu huduma za mahakama kwa
wananchi.
Jengo la mahakama Kuu
kanda ya Mbeya lilianza kufanyiwa ukarabati Februari 2016 na kukamilika mwezi Aprili
mwaka huu uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.4 ikiwa ni pamoja na kufungwa
kwa mifumo ya kisasa (video conferencing) ili kurahisisha utendaji kazi na kumaliza
mashauri kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni