Hivi karibuni
nilibahatika kutembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, miongoni mwa maeneo ambayo
nilivutiwa nayo kutaka kufahamu zaidi katika Kanda hiyo aina gani ya kesi/mashauri yanayofunguliwa kwa wingi .
Mahojiano maalum
na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mkoa-Iringa, Mhe. David Ngunyale
yanabainisha kuwa Kesi za Unyanyasi wa Kijinsia hususani za Vitendo vya Ubakaji
zinaongoza kufunguliwa kwa wingi katika Mahakama mkoani humo huku akitaja
idadi kuwa kwa mwaka 2016 jumla ya kesi 62 zilifunguliwa katika Mahakama hiyo.
“Matukio ya Ubakaji
katika Mkoa wa Iringa yanazidi kushika kasi, hii inajidhihirisha kufuatia takwimu
za kesi/mashauri yanayofunguliwa Mahakamani mwaka hadi mwaka, mfano kwa mwaka
huu pekee hadi kufikia Juni jumla ya kesi 36 tayari zilifunguliwa hali hii
inaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kutakuwa na kesi nyingi za namna
hii,” alieleza Mhe. Ngunyale.
Kufuatia hali hii,
Hakimu huyo Mkazi anaeleza kuwa Mahakama inazipa kipaumbele zaidi kesi za namna hii kwa kuzisikiliza na kuzitolea maamuzi haraka iwezekanavyo, hata hivyo Mhe. Ngunyale
anakiri kuwa katika uendeshaji wa kesi za namna hii wanakabiliwa na changamoto
kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya walalamikaji kula njama na washitakiwa
na matokeo yake kesi inashindwa kuendelea, mashahidi kutotokea Mahakamani, baadhi kesi
kuhusisha ndugu ambao mara nyingine huelewana na hatimaye kusababisha kesi
kutoendelea.
Muonekano wa jengo la Mahakama ya
Iringa, ndani ya uwanja huo kuna Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na
Mahakama ya Wilaya-Iringa ‘Judiciary Square’
Mhe. Ngunyale anasema
kwa mujibu wa sheria, endapo mtu hubainika kuwa alishiriki katika kitendo cha
ubakaji pasipo shaka Mahakama hutoa adhabu ya kifungo cha miaka 30,
viboko sita (6) na fidia kwa familia ya muathirika wa tukio hilo.
Aidha; Hakimu huyo
Mfawidhi amesifu ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na Wadau wake mkoani humo ikiwa
ni pamoja na Polisi, Wanasheria, Ustawi wa Jamii katika uendeshaji wa kesi
hizo.
Pichani ni Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Mahakama ya Hakimu Mkazi/ Mkoa-Iringa, Mhe. David Ngunyale.
Kwa Upande wake, Mkuu
wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), ACP. Deusdedit Kasindo akizungumza kwa niaba
ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, ACP. Julius A. Mjengi anakiri kuwa tatizo
la kesi
za Ubakaji kwa Mkoa huo lipo huku akitaja visababishi vya tatizo
hilo kuwa ni pamoja na Ulevi wa kutumia Madawa
ya Kulevya, pombe za kienyeji (ulanzi), Tamaa ya mapenzi hususani
kwa watoto wa shule, kutelekezwa kwa watoto pamoja na umaskini.
Pichani ni Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Iringa, Acp. Julius A. Mjengi
Anafafanua kuwa imani za kishirikina pia zinachangia ongezeko la kesi za aina hii kwa kuwa katika
imani za kishirikina Waganga wa kienyeji wamekuwa wakiwadanganya watu kna kwa hali hii wanasababisha kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa
vitendo hivyo. Kwa mujibu wa takwimu, Mkuu huyo wa Upelelezi alisema kuwa kwa
mwaka 2016 zilipokelewa jumla ya kesi 259 kati ya kesi hizo 239 zilikuwa
zinawahusu watoto akifafanua kuwa kubaka watoto ilikuwa ni kesi
203, kujaribu kubaka 11 na kulawiti zilikuwa kesi
25.
Aliongeza kuwa kubakwa
wanawake zilikuwa kesi 18, kujaribu kubaka ni kesi 2 na hivyo kupelekea kuwa na
idadi ya jumla ya kesi 259.
ACP Kasindo alisema
kuwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hususani ubakaji
wana umri kati ya miaka 2 hadi miaka 10.
Mkuu huyo wa Upelelezi
alidai kuwa kati ya kesi hizo 259 jumla ya kesi 163 zilifikishwa Mahakamani
ambapo kati ya kesi hizo zilizofikishwa Mahakamani jumla ya Watuhumiwa 41
walitiwa hatiani, kesi nyingine zilizobaki zinaendelea kusikilizwa Mahakamani.
Akizungumzia juu ya kesi
walizopokea Polisi kwa mwaka huu, 2017 hadi kufikia mwezi Mei, Mkuu huyo wa
Upelelezi alisema wamepokea jumla ya kesi 139 ambapo kati ya kesi hizo
zinazowahusu watoto pekee ni jumla ya kesi 121.
“Kubaka peke yake ni
kesi 98, kujaribu kubaka ni kesi 7, wanawake zipo kesi 18, kati ya hizi 17 ni kubaka na kujaribu kubaka na zilizopelekwa Mahakamani ni kesi 105, na
waliotiwa hatiani ni 12, walioachiliwa ni 45, na zinazoendelea Mahakamani zipo
48 huku mafanikio yakiwa ni asilimia 10 hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu,”
alieleza ACP. Kasindo.
Pichani ni Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO),
Acp. Deusdedit Kasindo
Aidha, ACP. Kasindo
alieleza kuwa kuna changamoto ya kesi nyingi zinazopelekwa Mahakamani kukwama, huku
akitoa sababu ya kusuasua kwa kesi hizo kuwa ni pamoja na umri mdogo wa Wahanga
unaosababisha kushindwa kujieleza kwa ufasaha, Watuhumiwa wa makosa hayo kuwa
ndugu mfano baba na mtoto, mjomba na mpwa na kadhalika, baadhi ya ndugu kuanza
kusuluhishana na hatimaye kuelewana hali inayosababisha kesi kutoendelea.
Katika jitihada za
kuendelea kupambana na vitendo hivyo, Mkuu wa Upelelezi mkoani humo anasema
kuwa kuna mikakati kadhaa wameweka ili kudhibiti vitendo hivyo, akitaja mikakati
hiyo kuwa ni pamoja na kuanzisha Vipindi vya Redio, kuelimisha jamii, mikutano
na wananchi, kufanya semina kwa kushirikiana na NGOs pamoja na Ustawi wa Jamii
kwa Viongozi ambao wapo karibu na Wananchi, kushughulikia kwa haraka zaidi
mashitaka ya aina hiyo.
ACP. Kasindo amekemea vikali
vitendo hivyo vya ubakaji huku akisema vitendo
hivi vinavyofanywa ni kosa la jinai na dhambi kwa Mungu, hivyo kuwaasa wananchi kuacha ulevi wa kupindukia pamoja na kuachana na imani za kishirikina.
Katika mwendelezo wa
kutaka kujua vyombo mbalimbali katika mkoa wa Iringa vinafanya nini katika
kudhibiti na kutokomeza vitendo hivi, nilifanikiwa pia kuonana na Afisa Ustawi
wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Bw. Ismail Mambo ambaye anafafanua kwa undani
kuhusu vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto.
“Tunapozungumzia
ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto tunamaanisha kwamba ni vile vitendo
ambavyo vinamuathriri mtoto katika ukuaji wake hasa kiakili, kimwili na
kihisia,” alifafanua Bw. Mambo.
Anasema kutokana na
hilo unakuta watoto wanaofanyiwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji ni wale
waliopo chini ya umri wa miaka 18, Bw. Mambo anasema kuwa vitendo hivyo
wafanyiwavyo watoto ni pamoja na Ubakaji, Ulawiti, pamoja na Kutelekezwa na
wazazi.
“Kuna watoto wengi
wanafungiwa majumbani bila msaada wowote wakati wazazi wao wakiwa katika
shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato, pia watoto hutelekezwa kwa kukosa
matunzo kutoka kwa wazazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba
zisizotarajiwa, ulemavu wa watoto, mimba za utotoni,” alieleza Bw. Mambo.
Anayeonekana pichani ni Mkuu wa
Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), Acp. Deusdedit Kasindo na kulia ni Afisa
Ustawi wa Jamii, Halmashauri ya Iringa, Bw. Ismail Mambo, katika mahojiano.
Afisa huyo anasema
kutokana na tatizo hilo, Halmashauri imeweka mikakati kadhaa ya kukabiliana/kudhibiti
ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kamati za mitaa za kuhudumia watoto waishio katika
mazingira hatarishi, moja ya kazi ya Kamati hizo za Mitaa ni kuibua vitendo
vyote vinavyotokea katika mitaa yao vinavyohusu ukatili na unyanyasaji dhidi ya
watoto na kuviripoti kwenye kamati ya Ulinzi na Usalama ya mtoto na kwa
kushirikiana na Kamati hiyo huenda moja kwa moja kuripoti Kituo cha Polisi
katika dawati la Jinsia, Wanawake na Watoto la Polisi na hapo hatua mbalimbali
huchukuliwa kati ya Polisi na Ustawi wa Jamii ikiwemo kuhakikisha kwamba mtoto
mhanga anapata haki stahiki ikiwa ni pamoja na kupata matibabu, kuusikilizwa na
kupatiwa huduma za taratibu za kisheria katika ngazi ya Mahakama.
Hata hivyo Bw.Mambo
anadokeza kuwa uelewa wa jamii katika suala zima la malezi ya watoto
umeongezeka kwa kiasi fulani, zamani watu walikuwa hawatoi taarifa kutokana na
kuwa na uelewa mdogo pamoja na uwoga.
“Katika Sheria ya mtoto
namba. 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 95 kifungu kidogo cha kwanza (1)
kinazungumzia wajibu wa kuripoti ukiukwaji wa haki za mtoto,” alifafanua Bw.
Mambo.
Anaendelea kueleza
Mikakati iliyopo Ustawi wa Jamii mkoani humu akitaja kuwa ni pamoja na kutoa
elimu ya malezi katika ngazi ya jamii, kuanzisha vikundi kwa kila mtaa
vinavyotoa elimu ya malezi kwa kila kaya na kusimamia utekelezaji wake (kati ya
kuhudumia watoto waishio katika mazingira hatarishi, kutoa mafunzo kwa
Wasaidizi wa Jamii (Para Social) wawili wawili (2) kwa kila mtaa.
Anaongeza kuwa; mkakati
mwingine ni kufanya ufuatiliaji wa karibu wa Wataalamu na Wanachama wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ngazi ya Halmashauri katika kamati za watoto waishio
katika mazingira hatarishi ngazi za mitaa na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya
suala zima la ulinzi na usalama wa mtoto.
Afisa Ustawi huyo wa
jamii alimalizia kwa kusema kuwa katika mitaa yote 192 ndani ya Manispaa ya
Iringa imefikiwa katika mafunzo na kupewa mafunzo na kuteua makundi ya ‘Para
Socials’ na Wasaidizi wa Ustawi wa jamii.
Naye, Sheikh Shams Elmi
Obsiye, Katibu Mkuu- Taasisi ya DHI, NUREYN- Islamic-Iringa naye alizungumzia juu ya tatizo hili na kukiri lipo kwani tayari Viongozi wa dini wa Mkoa huo walishadokezwa
na Mkuu wa Mkoa juu ya uwepo wa tatizo hilo.
Anayeonekana pichani ni Kiongozi wa
Dini ya Kiislamu mkoani Iringa, Sheikh Shams Elmi Obsiye
“Ni kweli tatizo hili
lipo mkoani kwetu, kwa upande wetu Viongozi wa Dini ya Kiislamu tunajitahidi
kuhamasisha jamii kupitia Madrasa za Watoto, ambapo kwa sasa tuna jumla ya
Madrasa 25, na katika Madrassa zetu miongoni mwa mambo tunayowafunza watoto ni
pamoja na kuwafahamisha kuhusu vitendo vinavyoashiria ubakaji mfano kununuliwa
pipi, kupakatwa, kuitwa mchumba nk, madrasa zote
zinafundisha hivyo,” alieleza Sheikh Obsiye.
Aliongeza kuwa katika
Redio yao iitwayo Kibla Ten Fm iliyopo mkoani Iringa, huwa wana kipindi
kinachohusu masuala ya Udhalilishaji wa Kijinsia ambapo hutoa elimu ili
wananchi waweze kujua vitendo hivyo ni kosa la jinai na havimpendezi Mwenyezi Mungu.
“Mbali na vitendo vya ubakaji
ambavyo vinaripotiwa katika misikiti yenu, yapo pia matendo mengine ya
unyanyasaji wa Kijinsia kama baadhi ya wanaume kuwapiga wake zao na kadhalika,”
alibainisha Sheikh Obsiye.
Alisema kuwa kwa mwezi
wanapokea malalamiko mbalimbali zaidi ya 30, hata hivyo Sheikh huyo amevitaka
vyombo husika kutoa elimu zaidi kwa Viongozi wa Dini ili kuwapa mbinu zaidi ya
jinsi ya kushughulikia kesi za ubakaji na nyingine zinazohusiana na unyanyasaji
wa kijinsia.
Aidha Sheikh huyo pia
alivitaka Vikundi vingine vya Jamii kushiriki katika kupambana na vitendo hivi,
mfano Makundi ya akina mama wanaweza pia kushiriki kutoa elimu kwa watoto juu
ya viashiria vya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na umuhimu wa kutoa
taarifa juu ya vitendo hivyo kwa vyombo husika vya sheria.
Vitendo
vya Ubakaji na Udhalilishaji wa Kinjisia, vimekuwa
vikishika kasi kila uchwao hali ambayo inapelekea wasiwasi na hali ya kutoaminiana
miongoni mwa wanajamii, aidha; vitendo hivi ambavyo vinasababishwa na imani za
kishirikina, tamaa, Utandawazi na masuala mengineyo kama ilivyoelezwa na
Wataalam katika makala hii.
Hivyo kuna umuhimu
mkubwa kwa Wazazi, Walimu, Viongozi wa Dini na kila mmoja kwa nafasi yake
kushiriki kwa namna moja au nyingine katika kuelimisha na kutahadharisha makundi
mbalimbali katika jamii kama watoto juu ya viashiria vya vitendo hivi na umuhimu
wa kutoa taarifa kwa vyombo husika ikiwa ni pamoja na Ofisi za Serikali za
Mitaa, Polisi katika Dawati la Jinsia, Ustawi wa Jamii, Makanisani, Misikitini
n.k
Vilevile Wanaharakati
wa Masuala ya Kijinsia, Ustawi wa Jamii na vyombo vinginevyo vinavyojihusisha
na kupigania haki za binadamu, kuangalia uwezekano wa kuongeza kasi ya utoaji
elimu kwa njia ya semina, vipindi vya redio na runinga na njia nyinginezo ili
kuwafikia wananchi wengi ili vitendo hivi viweze kutokomea kabisa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni