Ijumaa, 21 Julai 2017

MAHAKAMA YAENDELEA KUJIZATITI KUBORESHA HUDUMA ZAKE


Na Lydia Churi
Mahakama ya Tanzania imepanga kutoa huduma bora ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi kwa wakati. Mpango huo wa kutoa huduma bora kwa wananchi unatekelezwa kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano unaotekelezwa katika kipindi cha 2015/16-2019/20.

Mpango Mkakati huu ni dira na mwelekeo wa Mahakama katika kufikia lengo lake la kuwa Mahakama iliyo karibu na inayofikiwa na wananchi katika kutoa huduma bora za utoaji wa haki. Aidha, Mpango Mkakati huu unalenga kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 ya kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati. 

Mpango huu umejikita katika nguzo tatu ambazo ni Utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, Upatikanaji wa Haki kwa wakati pamoja na uimarishaji wa Imani ya wananchi kwa Mahakama pamoja na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama.

Katika nguzo ya kwanza ya Mpango Mkakati huu, Mahakama imeanzisha vikao maalum vya kutathmini kazi ya uendeshaji wa mashauri na kazi za mahakama kwa ngazi za Mahakama ya Rufani, Majaji wafawidhi wa kanda za Mahakama Kuu pamoja na kamati tano za kumshauri jaji Mkuu za kanuni, Mafunzo, Tehama, ufuatiliaji na Maboresho. Aidha Mahakama pia inasimamia suala zima la utendaji kazi kwa malengo kwa kada zote ndani ya Mhimili huo.

Matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama
Akiwasilisha Taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania kwa Waziri wa Katiba na Sheria hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanga alisema Mahakama imeanza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji kazi wake pamoja na kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. 

Mahakama tayari imeanzisha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za mashauri kwa njia ya kielekitroniki kuanzia ngazi ya Mahakama za wilaya, Mkoa, kanda na Taifa. Mbali na mfumo huu, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha 2017/2018, Mahakama itakuwa imeanza kutumia mitandao kwenye uendeshaji wa kesi. 

Aidha, Mahakama iko kwenye mpango wa kuweka kwenye mtandao na kuingiza mkongo wa taifa kwa Mahakama zote za wilaya, Hakimu Mkazi/Mkoa, Mahakama Kuu na Makao Makuu jijini Dar es salaam. Tayari majengo ya Mahakama Kuu Mbeya na lile la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha yameshawekewa.    

Ili kutekeleza nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania, mhimili wa Mahakama unapitia upya taratibu, kanuni na sheria zinazokwamisha na kuchelewesha kesi mahakamani na zile zilizopo nje ya mahakama na kushauri ipasavyo. Mpango huu umesaidia kupunguza kesi za madai kutoka 38 na kufikia mpaka 21.

Aidha, Mtendaji Mkuu alisema Mahakama pia imeandaa program na mazoezi endelevu katika ngazi zote za mahakama za kuondosha na kuzuia mashauri ya zamani na kuimarisha menejimenti ya mashauri, kuyajua, na kuyachambua majalada pamoja na kufanya vikao vya awali na wadau wote baada ya mazoezi na usikilizaji wa mashauri. Mahakama pia itaimarisha upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya kesi zikiwemo njia za kupeleka kwa wateja kwa njia ya posta na njia nyingine za kielektroniki.

Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama
Katika kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, Kattanga alisema Mahakama inao mpango wa miaka mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2010 ambapo matarajio ya mpango huu ni kujenga jengo moja la Mahakama ya Rufani, majengo 30 ya Mahakama Kuu, majengo 24 ya Mahakama za Hakimu Mkazi, majengo 109 ya Mahakama za Wilaya na majengo 150 ya Mahakama za Mwanzo. 

Hata hivyo, bado kutakuwa na upungufu mkubwa wa Mahakama za Mwanzo kwa kuwa kuna kata zaidi ya 3000 na Mahakama za Mwanzo zilizopo ni 960. Lengo ni kuwa na Mahakama ya Mwanzo kwenye kila kata. Aidha, kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara, ni mikoa 14 tu ndiyo yenye Mahakama Kuu. Baadhi ya mikoa, wananchi wake wamekuwa wakilazimika kufuata huduma za Mahakama Kuu kwenye mikoa mingine, kwa mfano, wananchi wa mkoa wa Singida hawana budi kupata huduma hizo katika mkoa wa Dodoma ambapo ndipo yalipo makao makuu ya kanda ya Dodoma. Wananchi wa Kigoma pia wamekuwa wakifuata huduma hizo katika mkoa wa Tabora ambapo ndiyo makao makuu ya kanda ya Mahakama Kuu Tabora. 
 
Mikoa yenye Mahakama Kuu ni Dar es salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Moshi, Tanga, na Bukoba (Kagera). Mikoa mingine ni pamoja na Iringa, na Songea (Ruvuma). Mikoa mingine ni Tabora, Mbeya, Sumbawanga (Rukwa), Mtwara na Shinyanga.   
Hivi sasa Mahakama ya Tanzania inajenga majengo sita ya mfano katika utafiti wa Teknolojia ya gharama nafuu na ya muda mfupi iitwayo Moladi katika maeneo ya Kigamboni, Mkuranga, Bagamoyo, Kinyerezi, Kawe pamoja na jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Pwani na Mahakama ya wilaya ya Kibaha ambalo limekamilika na kuzinduliwa rasmi mwaka jana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa na tayari limeanza kutumika. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama (katikati), Mhe. Hussein Kattanga akimkabidhi Mkataba wa kazi, Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji, Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Mwangu, Mikataba hii ya kazi ilisainiwa na Wakuu wote wa Idara ndani ya Mahakama, lengo ni kufanya kazi kwa wakati kulingana na Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania, aliyesimama kushoto ni Msajili-Mahakama ya Rufani (T), Mhe. John Kahyoza.



Mahakama yaboresha Huduma kwa Majaji wake
Pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi, Mahakama pia imekuwa ikiboresha mazingira ya kazi kwa Majaji wote nchini. Majaji 65 waliopo Mahakama kuu ya Tanzania wamepatiwa ofisi zenye nafasi ya kutosha ili kuwawezesha kufanya kazi zao za utoaji wa haki kwa ufasaha ili kesi ziweze kumalizika kwa wakati. Kuna jumla ya vyumba 91 vilivyotengwa na kutumika kama ofisi za Majaji kwenye Mahakama kuu zote nchini.

Kutokana na idadi ya Majaji waliopo nchini, mahitaji ya Majaji bado ni makubwa ili kufanikisha azma ya Mahakama ya kutokuwa na mlundikano wa kesi kwenye mahakama mbalimbali nchini. Tathmini ya Mahakama iliyofanyika mwishoni mwaka 2016, Mahakama Kuu na Divisheni zake imekuwa na mzigo wa Mashauri 35,878 kwa idadi ya wastani wa Majaji 75 waliokuwepo kipindi cha mwaka 2016. Kwa mantiki hiyo, kila Jaji alikuwa na mzigo wa wastani wa mashauri 478. Aidha, uwezo wa Jaji mmoja kusikiliza kesi unakomea kwenye kesi 198 kwa mwaka, hivi.

Pamoja na kufahamu idadi ya Majaji waliopo nchini, ni muhimu pia wananchi wakafahamu mchakato mzima unaowezesha Majaji kupatikana. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania huteuliwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa Mamlaka hayo katika uteuzi wa watoa haki hao.
Uteuzi wa Majaji

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 109 (6) mtu anaweza kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Jaji kama atakuwa na sifa maalum ambazo zimeelezwa katika ibara ndogo ya 7 na awe amekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka 10.

Sifa hizo maalum ni kuwa na digrii ya kwanza ya Sheria kutoka katika chuo kikuu kinachotambulika na mamlaka za utambuzi pamoja na;

(a)  Kuwa hakimu;

(b)  Ameshika nafasi katika ofisi yoyote ya Umma akiwa kama Mwanasheria au Wakili wa kujitegemea na

(c)  Awe na sifa ya kuweza kusajiliwa kama Wakili kwa kipindi cha miaka isiyopungua kumi.

Kwa mujibu wa Ibara hii, siyo Mahakimu peke yao wenye sifa ya kuteuliwa kuwa jaji wa mahakama Kuu. Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo mamlaka ya kuteua mtu mwenye sifa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania hata kama anatoka nje ya mhimili wa Mahakama.

yo basi Majaji waliopo ni wachache na kuna ofisi 24 zipo wazi hazina Majaji. 

Mafanikio katika Usikilizwaji wa Mashauri ya Zamani (Backlog)
Kwa Mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, hadi kufikia Desemba mwaka 2016, mlundikano wa mashauri kwenye mahakama mbalimbali nchini ulishuka kutoka wastani wa asilimia 46 mwaka 2013 na kufikia wastani wa asilimia 21 kwenye mahakama ya Rufani na kutoka wastani wa asilimia 33 mwaka 2013 na kufikia wastani wa asilimia 9 kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania. Katika Mahakama za Hakimu Mkazi/Mkoa, idadi ya mlundikano wa mashauri ya zamani ilipungua na kufikia wastani wa asilimia 3 kutoka wastani wa asilimia 9 mwaka 2013. Aidha kwenye Mahakama za wilaya mlundikano wa mashauri ulishuka kutoka wastani wa asilimia 9 mwaka 2013 na kufikia wastani wa asilimia 3 mwaka 2016 wakati kwenye Mahakama za Mwanzomlundikano ulishuka kutoka wastani wa asilimia 2 mwaka 2013 hadi kufikia kesi 0 au kutokuwa na mashauri hayo kabisa hivi sasa.

Mahakama ya Tanzania haina budi kujivunia mafanikio haya makubwa hasa kwa Mahakama za chini ambako asilimia 80 ya kesi zinazofunguliwa na wananchi zipo kwenye ngazi hizo. Mahakama pia imefanikiwa kupunguza mlundikano wa mashauri yenye zaidi ya miaka miwili  kutoka mashauri 10,832 yaani sawa na asilimia 10 mwaka 2012 hadi kufikia mashauri 2,702 sawa na asilimia (5%) tano mwaka 2016.  

Watanzania pamoja na wadau wengine wa Mahakama wakiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali,pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali hawana budi kushirikiana na Mahakama ya Tanzania bega kwa bega ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.

Mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha upatikanaji wa haki pasipo kuangalia mchango wa wadau wengine katika kufanikisha suala hili, hivyo basi, Taasisi hizi zote hazina budi kuendeleza ushirikiano na chombo hiki muhimu cha utoaji haki ili nchi iweze kukua kiuchumi. Upatikanaji wa haki kwa wakati hutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji na hivyo kukuza uchumi wa nchi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni