Na Lydia Churi-Mahakama
Mahakama ni moja kati ya Mihimili mitatu ya dola wenye jukumu la msingi la kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati. Mhimili huu hufanya kazi ya kutafsiri Sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwapatia wananchi haki. Kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano, Mahakama ya Tanzania imeendelea kusimamia haki za Watoto kama zilivyo haki nyingine wanazostahili kuzipata wananchi wa Tanzania.
Utekelezwaji wa haki za Watoto
zilizoainishwa katika mikataba mbalimbali ya kikanda na Kimataifa na kupewa
nguvu ya kisheria kupitia Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009, kunahitaji ushirikiano
baina ya Taasisi na wadau wa haki za watoto. Katika kulinda haki za watoto wa
Tanzania, hivi karibuni, Mahakama ya Tanzania ilizindua Mahakama ya Watoto (Juvenile
Court) katika jiji la Mbeya na kufanya idadi ya Mahakama hizo kufikia mbili
hapa nchini. Mahakama nyingine ya Watoto iko Kisutu jijini Dar es salaam.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma akikata utepe kuzindua Mahakama
ya Watoto (Juvenile Court) leo jijini Mbeya. Hii ni Mahakama ya Pili ya
Watoto nchini Tanzania baada ya ile iliyoko Kisutu Jijini Dar es salaam.
Mahakama hii imejengwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF)
Akinukuu andiko la Shirika
la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), kuwa “Maendeleo Endelevu
yanaanza na kukamilika
kwa misingi ya watoto
kuwa salama, wawe ni
wenye afya bora na
waliopata elimu bora” (Sustainable Development starts and ends with safe, healthy and
well-educated children- UNICEF, May 2013).
Katika neno lake la utangulizi katika
andiko hilo, Anthony Lake, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF aliandika kuwa: Haki za
watoto na afya yao njema, lazima ipewe kipaumbele katika maandalizi ya ajenda ya
maendeleo endelevu ya baada ya mwaka 2015. Uwekezaji kwa manufaa ya watoto ni
njia bora ya kufuta umaskini, kuongeza kasi ya kuchanua kwa manufaa kwa wote.” Alisema andiko hilo linatukumbusha kuwa ustawi
wa Watanzania unaanza na Ustawi wa watoto.
Ustawi wa watanzania unaanza na ustawi wa watoto
Kaimu Jaji Mkuu aliendelea kusema kuwa maana ya ustawi wa watanzania unaanza na ustawi wa watoto ni kwamba tayari Katiba imetamka kuwa lengo kuu na jukumu la Serikali ni ustawi wa wananchi na ustawi huo wa wananchi ni lazima ujengewe misingi imara ya ustawi wa watoto wa leo.
Alisema jamii ya
watanzania bado inayo mengi ya kufanya ili kuendeleza asilimia 50 ya wananchi
wake ambao wana umri wa miaka 18 na chini ya miaka hiyo. Alisema, kwa mujibu wa
Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka 2012, Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ilikuwa na idadi ya watu milioni 44,928,923 na kati ya
hao, watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0 hadi 17 ni asilimia 50.1
Mikataba ya Haki za
Watoto iliyoridhiwa na Tanzania
Kutungwa kwa Sheria ya
Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 nchini Tanzania kunatokana na mikataba mbalimbali
ya kimataifa inayotambua na kulinda haki za Watoto ambayo Tanzania iliridhia.
Baadhi ya Mikataba hiyo ni Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (UN Convention on
the Rights of the Child -UNCRC), Mkataba
wa Afrika wa
Haki na Ustawi
wa Mtoto (African Charter on
the Rights and Welfare of the Child-ACRWWC).
Mikataba mingine ni ule wa United Nations
Standard Minimum Rules
for the Administration of
Juvenile Justice (Beijing Rules) na United
Nations Guidelines for
the Prevention of
Juvenile Delinquency (The Riyadh Guidelines).
Tanzania ilitunga Sheria
ya Mtoto Namba 21 ya 2009 kwa ajili ya haki, ulinzi na ustawi wa mtoto. Aidha,
Sheria hii imekusanya mapendekezo yote ya ndani ya nchi, ya kikanda na ya
kimataifa kuhusu maboresho ya haki na maslahi mapana ya mtoto na kutoa nguvu ya
kisheria. Baada ya kutungwa kwa Sheria hii, mihimili ya dola imepewa majukumu ya kutekeleza na
kuwajibika. Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania anasema kwa upande wa mhimili wa Mahakama,
inategemewa Mahakama ya Watoto isaidie kuwajibika na kutekeleza Sheria ya Mtoto.
Alisema kuna maeneo kadhaa
katika Sheria ya Mtoto ambayo yanasimamiwa na mamlaka nyingine. Pamoja na
ukweli huo, bado Mahakama ya Watoto inaweza kutoa ushirikiano kwa mamlaka hizo au amri za mahakama
zikasaidia utendaji wa mamlaka hizo, kwa mfano; mazingira mbalimbali
ambayo yameainishwa
na Sheria Namba 21 ya 2009 kuwa
ni hatarishi kwa mtoto kama vile uyatima, kutelekezwa, kuteswa, kuzurura,
kukinzana na sheria ambapo alisema Mahakama ya Watoto inaweza kutoa tafsiri na kupanua
wigo wa “mazingira hatarishi”. Mahakama
ya Watoto inaweza
kutoa tafsiri na kupanua wigo wa Ulinzi na wajibu wa wazazi kwa matunzo ya mtoto, matibabu
na elimu, sifa za mtu kuwa mlezi na uasili wa mtoto; namna gani Mahakama
itawasilisha taarifa mbali mbali au kutumia
rejista ya watoto
walioasiliwa kwa Msajili
wa Vizazi na Vifo pamoja na uzuiaji wa kazi za udhalilishaji kwa watoto wenye
umri wa chini ya miaka 18.
Aidha Serikali za Mitaa
na Serikali Kuu zitakapoanzisha vituo vya kutunzia na kulelea watoto wenye
shida ya malezi na Bunge kutoa fedha za kutosha kuendesha vituo hivyo zitaisadia
Mahakama kwa kiasi kikubwa, alisema Kaimu Jaji Mkuu na kuongeza kuwa Mahakama za
Watoto pia zinaweza kugundua mapungufu katika Sheria na kupendekeza kuwa Waziri mwenye dhamana ya
watoto atunge kanuni stahiki.
Sheria ya Mtoto Shirikishi na inataka Ushirikiano
Akizungumzia ushiriki na
ushirikishwaji wa Sheria ya Mtoto, Kaimu Jaji Mkuu alisema Sheria kuwa sheria
hii imesimama katika misingi ya ushirikiano baina ya mihimili yote, ushirikiano
na wadau mbali mbali kama UNICEF na NGOs, taasisi ambazo zinashughulika na
masuala ya haki za watoto. Alisema, Sheria hii pia inaitaka Mahakama ichukue
uongozi, na kuna masuala ambayo mihimili mingine imepewa nafasi ya
uongozi hivyo Mahakama inayo nafasi nzuri ya kuipa uhai sheria hii kwa kuwa kwanza,
haki zote stahili
zilizoainishwa ndani ya
Sheria hii zinamfaidisha mtoto, pili,
Sheria hii inapotafsiriwa, pale ambapo wanaona kuna “kutofahamika,
“utata” wawe na ujasiri wa kuielekeza
sheria kufikia malengo mazuri yaliyowekwa na Mikataba ya Kikanda na
Kimataifa kuhusu haki ya watoto.
Mahakama pia inayo
nafasi nzuri ya kuipa uhai Sheria hii kwa sababu Mahakimu katika Mahakama ya
Watoto watakuwa na nafasi
ya karibu kabisa
kuona namna vifungu mbali
mbali vya Sheria hii vinavyofanya kazi, hivyo Kaimu
Jaji Mkuu aliwaagiza Mahakama wanaosikiliza kesi za Watoto kuorodhesha mapungufu ya Sheria hii na kuhyawasilisha kwenye kamati
ya Kanuni ya Jaji Mkuu kwa ajili ya kupendekeza kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kuhusu mabadiliko ya Sheria.
Akisisitiza juu ya
kulinda haki za Watoto, kaimu Jaji Mkuu aliwataka mahakamu wanaosikiliza kesi
za Watoto wasome taarifa za Utekelezaji zinazowasilishwa na Tanzania na pia
zile zinazowasilishwa na mataifa mengine kuhusu Tanzania ili waweze kugundua mapungufu yetu ya kiutekekezaji ili tuweze
kupanga namna ya kuboresha utekekezaji. Mahakimu hao pia wametakiwa kufuatilia
haki za Watoto pindi wanapofanya ukaguzi kwenye Magereza.
Ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Watoto Mbeya
Jengo la Mahakama ya
Watoto jijini Mbeya lililojengwa kwa ushirikiano kati ya
Mahakama ya Tanzania na
UNICEF limegharimu kiasi cha shilingi za kitanzaniaMilioni 415 ambapo Mahakama imechangia kiasi cha shilingi milioni 214 na UNICEF shilingi milioni 201. Jengo hili lilianza kutumika April 18, 2017 na lina ofisi mbili za Hakimu, Ofisi ya Wakili wa Serikali, ofisi ya Afisa Ustawi wa Jamii na chumba cha Mawakili wa Kujitegemea.
Sababu za
Mahakama kujengwa Mbeya
Jengo hili ambalo ni la pili la Mahakama ya Watoto nchini limejengwa jijini
Mbeya kwa kuzingatia upatikanaji wa wadau na huduma zote muhimu za haki kwa
mtoto. Huduma hizo ni pamoja na uwepo wa shule ya maadilisho (approved school)
ikiwa ni pekee nchini, kuwepo kwa Mahabusu ya watoto mkoani humo, na kuwepo kwa
dawati la jinsia la watoto lenye viwango vinavyotambulika lililoanzishwa na
Jeshi la polisi. Mahakama hii pia ilianzishwa kutukana na uwepo wa timu ya
ulinzi na usalama wa mtoto (child protection team) na kuwepo kwa mfumo wa
marekebisho ya tabia kwa watoto (community rehabilitation programme).
Ushirikiano wa Mahakama na
UNICEF katika masuala ya haki ya Mtoto
Katika kipindi cha takribani miaka mitano yaani tangu mwaka 2012, UNICEF
na Mahakama walishirikiana katika kutengeneza kanuni za Mahakama ya Watoto
ikiwa ni matakwa ya kifungu cha 99(1) cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambacho
kinamtaka Jaji Mkuu kutengeneza kanuni za kutumika katika uendeshaji wa kesi
katika Mahakama za Watoto.
UNICEF ilitoa msaada wa kitaaluma (technical support) na fedha katika
kuandaa kanuni ambazo zilitangazwa katika Gazeti la Serikali No 182/2016.
Uandaaji wa kanuni hizo ulihusisha wadau mbalimbali wa haki za watoto kama
Majaji, Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Maafisa Ustawi wa Jamii, na Mashirika
yasiyo ya kiserikali vinayotoa msaada wa kisheria na vyombo vingine vinavyohusika
na masuala ya mtoto.
Aidha, UNICEF imeshirikiana na Mahakama katika kuandaa mafunzo kwa
wakufunzi (TOT) juu ya uendeshaji wa kesi za watoto kwa mujibu wa Sheria na
kanuni za watoto.Wakufunzi walitoka Mahakamani, Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Idara ya Ustawi wa Jamii.
UNICEF pia imeshirikiana na Mahakama kutoa mafunzo kwa Mahakimu, Mawakili, wa Serikali na Waendesha Mashtaka,
Maafisa Ustawi wa Jamii, taasisi
zinazotoa msaada wa kisheria na Taasisi zisizo za Kiserikali katika Mkoa wa Dar
es Salaam, Pwani, Mbeya, na Iringa.
Aidha mafunzo kwa wadau wote yanaendelea kufanyika katika wilaya mbalimbali kwa
kutumia wakufunzi waliopata mafunzo yaliyotolewa na UNICEF na Mahakama.
Mwakilishi wa UNICEF nchini, Stephanie Shanler akizungumza
wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Mahakama hiyo.
Sambamba na hilo kwa mwaka huu wa fedha
UNICEF wataendelea kushirkiana na Mahakama katika mpango endelevu wa kutoa mafunzo kwa wadau
wote wa haki za Watoto. Pia UNICEF imeonyesha nia ya kushirikiana na Mahakama
katika ukarabati mdogo wa Mahakama ili kuziweka katika mazingira rafiki kwa
watoto.
Hata hivyo, bado iko haja ya kuongeza idadi ya Mahakama za watoto nchini
kutokana na kuwepo kwa kesi za watoto na nyingine ambazo kwa namna moja au
nyingine zinawahusisha watoto katika mikoa mbalimbali nchini ili kutekeleza
azma ya kulinda na kutetea haki za Mtoto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mahakama ya watoto jijini Mbeya, Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali aliiomba UNICEF kuangalia
uwezekano wa kujenga majengo mengine manne ya Mahakama za watoto katika mikoa
ya Arusha, Mwanza, Dodoma na Tabora ili kuwapatia Mahakimu fursa ya kujifunza
kwa vitendo namna Mahakama za watoto zinavyofanya kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni