Na Mohamed Ali
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, imetekeleza
mkakati wake wa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na upatikanaji wa mashauri
yaliyoisha, kwa kuanzisha mfumo wa Kielektroniki
kwa kuanzisha utunzaji wa majalada.
Mfumo huo wa Kielektroniki ulioanzishwa ili
kuboresha uhifadhi na ufuatiliaji wa majalada yaliyoisha mpaka sasa utendaji
kazi wake umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza
kwa Niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga, Afisa
Utumishi wa Mahakama Nkurumah Katangira alisema mfumo huo wa utunzaji wa
majalada ulizingatia aina za mashauri mf. Kesi za madai na jinai, vilevile kwa
kuzingatia miaka mf. Kesi za madai za mwaka 2003 hadi mwaka 2007, ili kurahisisha upatikanaji wake
pindi yanapohitajika.
Limefanyika zoezi la kuyachambua majalada,
kuyaorodhesha na hatimaye kuyaingiza katika mfumo wa kompyuta na kasha majalada
hayo kuhifadhiwa stoo.
Aliongeza kwa kusema jumla ya maboksi 2104 yenye
majalada yamehifadhiwa stoo pia maboksi 1030 yenye majalada ya muda
yamehifadhiwa kwenye kontena.
Mfumo wa excel umetengenezwa ili kurahisisha
upatikanaji wa majalada hivyo kitengo cha TEHAMA Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
salaam kwa pamoja walipendekeza mfumo huo uitwe ‘ARCHIVE FILES TRACKING SYSTEM’,
alisema Katangira.
Akiongelea mafanikio ya mfumo huo Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam Mhe. Ruth Massam alisema mfumo huo, umerahisisha
utafutaji wa majalada kwakuwa sasa yanapangwa kwa kuzingatia miaka, aina ya
kesi na namba ya kesi, pia umesaidia kujua idadi ya majalada ambayo yaliisha na
hayaonekani kwa wakati.
Aidha mafanikio ya mfumo ni pamoja na kupunguza
malalamiko juu ya upotevu wa majalada hasa yale ya muda mrefu lakini pia mfumo
umerejesha imani ya wananchi kwa Mahakama.
Pamoja na kufanikiwa kwa mfumo huo kwa zaidi ya 90%
Katangira alikiri kukabiliwa na changamoto chache ikiwemo uelewa mdogo wa
watumishi juu ya matumizi ya kompyuta pamoja na kukata kwa mtandao wa intaneti
mara kwa mara hivyo kuzorotesha utendaji kazi wa mfumo huo.
Aidha kutokurejeshwa kwa majalada pindi yanapotoka
stoo kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni