Na Mary Gwera
JUMLA ya Kesi za Mauaji 24 zimepangwa
kwa ajili ya kusikilizwa kuanzia Agosti 14 hadi Agosti 25 Mwaka huu katika
Kikao maalum cha kusikiliza mashauri ‘Court session’ kitakachofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Akizungumza na Mwandishi wa habari
hii mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya
Dodoma, Mhe. Messeka John Chaba alisema kuwa mashauri manne (4) kati ya
mashauri hayo 24 yamepangwa kusikilizwa ‘hearing’ huku mashauri 20 yakiwa
yamepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali ‘Plea taking.’
Kufuatia maandalizi ya kikao hiki
maalum Mhe. Chaba ametoa wito kwa mashahidi
muhimu ambao wametumiwa wito wa kuitwa shaurini ‘summons’ kufika
Mahakamani na kutoa ushahidi wao ili haki iweze kutendeka.
Kwa upande wa Waendesha Mashtaka - Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jeshi la Polisi Mkoani
Dodoma, Mhe. Chaba amewasihi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo ikiwa
ni pamoja na kuhakikisha Mashahidi wote wanapatikana na kufika Mahakamani ili
kuiwezesha Mahakama kusikiliza mashauri hayo na kuyatolea uamuzi kwa mujibu wa
sheria.
“Miongoni mwa mashauri hayo 4
yatakayosikilizwa, mashauri 2 yalisikilizwa na Mahakama ya Rufani Tanzania na
kuamuliwa yaanze upya,” alifafanua Mhe. Chaba. Aliyataja mashauri hayo kuwa ni “Crim. Sess. Case No. 52/2014 Mshtakiwa - Adrian
Francis na Crim. Sess. Case No.39/2012 Mshtakiwa - Wylife Salumu@Nyendo & 2
Others.
Kikao
hicho kitaendeshwa na Majaji watatu (3) wa Mahakama Kuu Dodoma, ambao ni; Mhe Jaji M.A. Kwariko, Jaji Mfawidhi, Mhe Jaji H.H.
Kalombola, na Mhe Jaji L.
Mansoor.
“Matarajio yetu ni kwamba kikao hiki
kitasaidia kumaliza/kuondoa mashauri ya jinai ambayo ni mlundikano. Aidha, kikao hiki kitatoa fursa kwa washtakiwa
20 kufika Mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa awali/uchukuaji wa kiri (plea
taking) na huenda baadhi yao wakakiri makosa yao na kupunguza ama kuongeza
idadi ya mashauri ambayo yatakuwa yameamuliwa na Mahakama Kuu kwa mwaka huu
2017,” alibainisha Mhe. Chaba.
Mahakama
ya Tanzania imedhamiria kusikiliza na kutoa uamuzi kwa wakati kwa mashauri yote
ya muda mrefu na yanayoendelea kufunguliwa Mahakamani ili haki ipatikane kwa
wakati na pia kurejesha
imani ya jamii.
Pichani ni Mhe. Messeka Chabba, Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni