Alhamisi, 14 Septemba 2017

MAHAKAMA YATAJA SABABU ZA KESI KUTOMALIZIKA MAPEMA


Na Mary Gwera, MAHAKAMA

Mahakama ya Tanzania inao wajibu wa kutekeleza jukumu la utoaji haki kwa wananchi kwa wakati. ‘Kwa mujibu wa Kifungu na. 107(A) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa Mahakama. Na kazi kubwa ya Mahakama kama mhimili ni kutafsiri sheria zilizotungwa na Bunge.’

Kutokana na jukumu hilo, Mahakama ya Tanzania kupitia Mahakama zake ambazo ni Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi/Mkoa, Mahakama Kuu na Divisheni zake (Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi) na Mahakama Kuu divisheni ya Makosa ya Rushwa) pamoja na Mahakama ya Rufani imekuwa ikitekeleza jukumu hili la msingi kwa kujiwekea mikakati mbalimbali kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati.
Mahakama na Mikakati ya kumaliza kesi kwa wakati

Mikakati hiyo ni pamoja na kuandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano unaotekelezwa katika kipindi cha 2015/16-2019/20. Mpango huu ni dira na mwelekeo wa Mahakama katika kufikia lengo lake la kuwa Mahakama iliyo karibu na inayofikiwa na wananchi katika kutoa huduma bora za utoaji wa haki. Aidha, Mpango Mkakati huu unalenga kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 ya kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati.
Ili kutekeleza suala la kumalizika mapema kwa kesi zilizoko Mahakamani, Mahakama ya Tanzania imepanga muda maalum wa kumalizika kwa kesi katika mahakama zake mbalimbali kwa mfano, katika Mahakama Kuu kesi inatakiwa kumalizika ndani ya kipindi cha miaka miwili, Mahakama za Mikoa na Wilaya kesi zinatakiwa kumalizika ndani ya miezi 12 wakati katika mahakama za Mwanzo kesi zinatakiwa kusikilizwa na kumalizika ndani ya miezi sita tu.

Mkakati mwingine uliowekwa na Mahakama ili kumaliza kesi kwa wakati ni ule wa kufanya vikao na wadau ili kujadili namna ya kumaliza kesi kwa wakati kwa kuwa kitendo cha kuchelewa kwa kesi hakisababishwi na Mahakama pekee bali wadau wa Mahakama pia wanahusika.

Aidha; kwa asiyefahamu utaratibu mzima wa uendeshaji wa kesi mahakamani, ni rahisi kwake kuelekeza tuhuma kwa Mahakama kuwa ndiyo inayosababisha kesi kuchukua muda mrefu mpaka kumalizika ikiwemo na dhana ya upokeaji wa rushwa kwa baadhi ya watumishi wa Mahakama wasio waaminifu. Dhana hii inaweza kuwepo lakini isiwe mara zote inahusika. Wengine wamekuwa wakidhani kuwa Mahakama inachelewesha kesi zake bila sababu za msingi,
Aidha; kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka kwa Wananchi na Wadau mbalimbali wa Mahakama ya kuwa Mahakama inachelewesha kesi zake bila sababu za msingi, malalamiko haya yamekuwa yakitolewa kwa njia mbalimbali kama Magazeti, runinga, mitandao ya kijamii, Makongamano n.k.

Mfano; katika gazeti la Mwananchi Toleo namba 6232 la Agosti 20, 2017 katika ukurasa wake wa kumi (10) yaliandikwa maoni ya Mwananchi kwa Mhariri yakisomeka ‘SIELEWI SABABU YA KESI YENYE VIDHIBITI VYOTE KUKAA MIAKA’
Ieleweke kuwa kesi inapofika Mahakamani, inapitia taratibu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyiwa kazi kwa pamoja karibu na wadau wake mfano: - Waendesha Mashtaka, Polisi, Mkemia Mkuu wa Serikali kwa baadhi ya kesi n.k kabla ya hukumu/uamuzi kutolewa na Jaji/Hakimu.

Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye Mafunzo kwa ajili ya kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania ikiwa na pamoja na kuweka mikakati ya kumaliza mlundikano wa Mashauri Mahakamani. Mafunzo hayo yaliyofanyika April 3-7, 2017 jijini Arusha.
 
Taratibu/Miongozo ya kufuata katika utoaji wa Haki
Akizungumza na Mwandishi wa makala hii, Msajili-Mahakama ya Rufani, Mhe. John R. Kahyoza anasema kuwa Mahakama zote muhimu zimeanzishwa na Sheria na kuwekewa utaratibu na miongozo ya kufuata ili kutenda haki.
Mojawapo ya miongozo hiyo ni kuwa kama refa wa mpira wa miguu, refa hatakiwi kusaidia upande wowote wakati anachezesha mpira kwahiyo kama ambavyo Refa hawezi kupiga mpira golini hata kama mpira utamfikia refa akiwa eneo zuri la kufanya hivyo.
“Hali hii pia inafanyika hata kwa Jaji/Hakimu, hata akisikia au kuona kupitia Runinga (TV) kuwa mshtakiwa fulani awe amekutwa na kithibitisho hawezi kumtia hatiani, na utaratibu wa Mahakama kuwa lazima isubiri kuletewa ushahidi mahakamani,” alifafanua Mhe. Kahyoza.
Aliongeza kuwa Mahakama haijui wala haitakiwi kujua kama mshtakiwa kakutwa na vielelezo au la, wajibu wa Mahakama ni kutoa nafasi sawa kwa pande mbili kuleta mashahidi na vielelezo ili kuweza kutoa haki pasipo shaka yoyote.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Peace Mpango anasema Kwa mujibu wa Sheria ya Ushahidi Sura ya sita (6) ya mwaka 1967 kifungu cha 110 (1) na kifungu cha 114 (1) vinaeleza kwamba mtu ambaye anashitaki, amefungua shauri, anaiomba au kuitaka Mahakama itoe uamuzi au hukumu katika mashitaka au shauri kwa manufaa yake, analazimika kuwasilisha mahakamani ushahidi unaojenga hoja kuthibitisha madai au tuhuma anazozitoa dhidi ya  tuhuma anazozitoa dhidi ya mtuhumiwa au mshitakiwa. Kiwango cha uthibitishaji wa tuhuma, dai au hoja katika kesi ya jinai ni kutoacha shaka yoyote.
Hata hivyo pamoja na juhudi za Mahakama ya Tanzania za kuhakikisha inaondosha mashauri yaliyokaa muda mrefu mahakamani, bado Majaji wa Mahakama ya Rufani na wale wa mahakama kuu waliamua kujitolea kuacha likizo zao wanazoenda kati ya mwezi Desemba na Januari ili kusikiliza mashauri mbalimbali ukiwa ni mkakati wao waliojiwekea ili kupunguza mlundikano wa mashauri yaliyoko mahakamani. 
 “Kwa maana hiyo katika kesi za jinai anayefungua mashtaka ni waendesha mashtaka (prosecution) kwa niaba ya Serikali akisaidiana na Polisi na hivyo wao ndio wanaowajibika kuleta ushahidi Mahakamani utakaopaswa kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba mtuhumiwa ametenda kosa. Kazi ya Jaji au Hakimu ni kuangalia kama ushaidi uliowasilishwa Mahakamani na mwendesha Mashtaka kama hauna shaka yoyote kumtia mtuhumiwa hatiani au la ambapo hukumu hiyo inatolewa mwisho wa kesi,” alifafanua Bi. Mpango.
Anaongeza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ya pili (2) , Ibara ya 13 (6) (b) inasema “ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.”
Naye; Mkurugenzi Msaidizi wa Malalamiko-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Happiness Ndesamburo anasema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Taratibu za Makosa ya Jinai Sura ya 225, kifungu kidogo cha 4, Mahakama imepewa mamlaka ya kufuta baadhi ya kesi zilizozidi siku 60 bila kusikilizwa na vilevile Mahakama hiyo hiyo haina uwezo wa kufuta baadhi ya mashitaka mfano kesi za mauaji ‘Murder cases’, kesi za Madawa ya kulevya ‘drugs cases’ mpaka upande wa mashitaka ukamilishe upelelezi na kesi ianze kusikilizwa au upande wa mashitaka uamue kufuta wenyewe.
Mhe. Ndesamburo anaeleza vilevile kuna mashauri ambayo Mahakama huweza kuyafuta kama upelelezi haujakamilika na kesi kuanza kusikilizwa ndani ya siku 60 na kesi hizohizo zinaweza zisifutwe endapo mambo haya yatajitokeza; mfano Mkuu wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) atawasilisha hati ya kueleza sababu za kufanya ahirisho la kesi na endapo Mahakama itakubali shauri husika litaongezewa siku 60 nyingine.
Hata hivyo; Mkurugenzi wa Mashitaka naye anaweza kufungua/kuwasilisha hati akieleza sababu za ahirisho, endapo Mahakama itakubaliana pia na sababu tajwa itatoa ahirisho lingine kwa kipindi kisichozidi miezi 24 toka ahirisho la kwanza lililotolewa kwa Mkuu wa Makosa ya Jinai wa Mkoa.
Sababu za kuchelewa kumalizika kwa kesi
Aidha; ifahamike kuwa kuchelewa kwa kesi/shauri Mahakamani kunaweza kusababishwa na
·        Uchunguzi kuchukua muda mrefu kwa baadhi ya kesi
·        Uhaba wa Waendesha Mashitaka, Mawakili, Mashahidi kutopatikana kwa wakati na mara nyingine kutopatikana kabisa, umbali (distance) kati wenye kesi (wananchi) na Mahakama
·         Wafungwa na Mahabusu kutofikishwa Mahakamani kwa wakati mfano; Wilaya ya Karatu, Longido na Monduli hakuna Magereza wote wanategemea Magereza ya Kisongo iliyopo Arusha, hali hii pia inapelekea kesi kuchukua muda mrefu Mahakamani.

Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati ameainisha sababu nyingine ambazo zinapelekea kesi kukaa muda mrefu Mahakamani kuwa ni pamoja na utumiaji wa mfumo wa Kianalojia katika uendeshaji wa kesi, uhaba wa Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani (T).
“Katika jitihada za kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, hivi sasa Mahakama ya Tanzania inatekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano (5), 2015/2016-2019/2020 ambao unazingatia nguzo tatu (3) za Utawala Bora na Menejimenti ya Rasilimali, Upatikanaji na utoaji wa Haki kwa wakati na kuimarisha imani ya Jamii na Ushirikishaji wa wadau.”alisema Mhe. Revocati
Ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati; Majaji na Mahakimu wamejipangia mikakati kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwa na idadi maalum ya kesi ambazo wanatakiwa kumaliza kwa mwaka. Mfano, Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wanatakiwa kusikiliza na kumaliza kesi 220 kwa mwaka, huku Mahakimu wa Mahakama za Mkoa na Wilaya wanatakiwa kusikiliza na kumaliza kesi 250 kwa mwaka na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wanatakiwa kumaliza kesi 260 kwa mwaka.
Hali kadhalika, kila Mahakama ina ukomo wa umri wa shauri, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ukomo wa kesi kukaa Mahakamani ni miaka miwili (2), Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya ni mwaka mmoja na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita (6).
Katika uzingatiaji wa ukomo wa muda, Mahakama imefanikiwa kwa kiwango kikubwa hasa kwa Mahakama za mwanzo ambazo zinachukua asilimia 73 ya Mashari yote Mahakamani.
Hakuna kesi yenye zaidi ya miezi sita (6) Mahakama za Mwanzo, kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, kuna mafanikio isipokuwa isipokuwa kwa yale mashauri  ambayo sheria inaizuia Mahakama kuendelea na umalizwaji wa shauri kabla ya Wadau Fulani kukamilisha mambo mengine.
Kwa upande wa Mahakama Kuu na Rufani changamoto ya uhaba wa Majaji unakwamisha jitihada hizi.
Vilevile Mahakama imekuwa ikifanya jitihada za dhati katika kuhakikisha kuwa inashirikisha Wadau wake wanaoambatana nao katika mlolongo mzima wa uendeshaji wa kesi ili kuwa na nguvu ya pamoja kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ili kesi ziweze kumalizika kwa wakati.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni