Majaji nchini
wameagizwa kumaliza kesi zote za muda mrefu Mahakamani ifikapo Disemba 15,
mwaka huu ili kuendana na azma ya Mahakama ya kutoa haki kwa wote na kwa wakati.
Akizungumza katika
Mkutano wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Kiongozi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali alisema kuwa Kanda zote za Mahakama Kuu
nchini tayari zimeshaainisha idadi ya kesi zote za kuanzia miaka miwili
kuendelea (kesi za mlundikano) ambazo zitafanyiwa kazi.
“Nawaagiza Majaji wote
nchini kuendelea na zoezi la kusikiliza kesi hususani kesi za muda mrefu
Mahakamani, na zoezi hili lianze kufanyika Oktoba 16,mwaka huu na kazi hii
nataka ikamilike kufikia Desemba 15,mwaka huu,” alisisitiza.
Mhe.Jaji Kiongozi
amezitaja Kanda za Mahakama Kuu ambazo zinaonekana kuelemewa na mzigo wa
mashauri kuandaa orodha ya mashauri ‘causelist’wanayohitaji kusaidiwa.
Mahakama hizo ni
Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza, Mahakama
Kuu-Kanda ya Bukoba, Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Mahakama Kuu-Kanda ya
Shinyanga, Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi na Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi.
Aidha Mhe. Wambali
ameagiza zoezi hilo lifanyike ndani ya wiki moja kuanzia Jumatatu, Septemba 18
ili kuwezesha kujua uhitaji wa msaada wa Majaji wengine kutoka Kanda nyingine
watakaoenda kusaidia kusikiliza na kumaliza mashauri hayo katika maeneo tajwa.
Aidha Mhe. Jaji
Kiongozi amewataka Majaji Wafawidhi kuitisha vikao na Wadau wa Mahakama ili
waweze kujua juu ya kuwepo kwa Programu maalum ya kusikiliza na kumaliza kesi
zote za muda mrefu Mahakamani.
Kwa upande wake Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma amewataka Majaji na Watumishi
wa Mahakama kwa ujumla kufanya kazi kwa kuzingatia nguzo tatu za Mpango Mkakati
wa Mahakama ili kutekeleza majukumu kimkakati na hatimaye kupata matokeo chanya.
“Majaji Wafawidhi ni
nguzo muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkakati hususani katika nguzo namba
mbili ambayo ni Upatikanaji na utoaji wa Haki kwa wakati, kupitia Majaji na
Mahakimu waliopo chini yao” alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Akiongelea juu ya jukumu kuu la utoaji haki
nchini, Mhe. Jaji Mkuu amesisitiza juu ya kuwa na kumbukumbu sahihi ya takwimu
za mashauri zilizopo katika Mahakama husika hali ambayo itawezesha kujua ni
msaada utakaohitaji, bajeti na kadhalika.
Kwa upande mwingine Mhe. Jaji Mkuu amesisitiza
juu ya matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa kesi ili kuendeana na kasi ya
Teknolojia hali ambayo itawezesha huduma ya haki kuwafikia wananchi kwa wakati.
Mambo mengine aliyoyasisitiza Mhe. Jaji Mkuu
alipokuwa akifunga Mkutano wa Majaji Wafawidhi ni pamoja na ufanyaji kazi kwa
ushirikiano kwa Watumishi wote wa Mahakama na kubadili mtazamo hasi ‘change of
attitude’ na kuzingatia maadili katika utendaji kazi.
Mkutano wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, uliofanyika kwa siku mbili (2), Septemba 15&16 ni mwendelezo wa
Vikao mbalimbali ambavyo vimekuwa vikifanyika mara kwa mara vyote vikiwa na
lengo la kuhakikisha kuwa azma ya Mahakama ya Tanzania ya kutoa haki kwa wakati
inaonekana kutekelezeka.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa neno pindi alipokuwa akifunga Mkutano wa Majaji
Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa-AICC jijini Arusha, Septemba, 15 na 16,2017.
Sehemu ya Wahe. Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu nchini wakimsikiliza kwa makini Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani)
Wahe. Majaji Wafawidhi pamoja na Wasajili wakiwa katika Mkutano huo uliokamilika Septemba 16, 2017.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akiongea katika Mkutano wa Majaji Wafawidhi.
Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania,Mhe. Hussein Kattanga akitoa neno, amesisitiza juu ya ufanyaji kazi kwa malengo.
Mkuu wa Kitengo cha Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama,Mhe.Zahra Maruma akitoa mara ya utekelezaji wa kazi mbalimbali za Mradi mbele ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kuhitimisha kikao cha siku mbili cha kujadili juu ya mikakati ya kuondosha mashauri ya muda mrefu Mahakamani. aliyeketi katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania,Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali, wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa pia ni Jaji namba moja wa Mahakama Kuu ya Tanzania, wa pili kulia ni Kaimu Jaji Mfawidhi,Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Sekela Moshi na wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Wasajili na Watendaji wa Mahakama.
(Picha na Habari na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni