Na Lydia Churi- Mahakama
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza Mahakama za nchi za
Jumuiya ya Madola kupambana na rushwa ili kuzifanya Mahakama hizo kuwa huru
zinapotekeleza jukumu lake la msingi la utoaji haki.
Akifungua Mkutano wa
mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola kilichoanza leo
nchini, Makamu wa Rais alisema kuwepo kwa vitendo vya rushwa ndani ya Mahakama
husababisha Mahakama kutokuwa huru na kukosekana kwa utawala wa sheria.
Alisema kila nchi
inapaswa kuwa na Mahakama huru na inayowajibika ili kujenga msingi wa
Demokrasia. Aliongeza kuwa kuwa Serikali ya Tanzania itahakikisha Mahakama yake
inapambana na vitendo vya rushwa ili kuimarisha uhuru wake.
“Naamini kuwa nia ya
kujenga Mahakama bora na yenye kuwajibika kwa Tanzania haiwezi kutenganishwa na
juhudi za Serikali Katika kupambana kuondoa umaskini na rushwa”, alisema Makamu
wa Rais.Makamu wa Rais alisema amefurahishwa kuona Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola wanakutana ili kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia nchi zao kuendana na kauli mbiu ya Mkutano huo inayosema kujenga mahakama shirikishi, inayowajibika na thabiti kiutendaji.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza kwenye Mkutano huo alisema Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ndiyo njia ya kuifanya Mahakama kuwa shirikishi, inayowajibika na thabiti kiutendaji.
Alisema ni mwaka wa
pili sasa tangu Mahakama ya Tanzania ianze kutekeleza Mpango Mkakati wake wa
miaka mitano ambao msingi wake ni kujenga Imani ya wananchi kwa Mahakama na
kuhakikisha upatikanaji na utoaji wa haki kwa wote na wakati.
“Nina uhakika kwa wiki
hii moja tutaweza kubadilishana uzoefu juu ya umuhimu wa Mpango Mkakati katika
kusaidia Mahakama zetu za Jumuiya ya Madola ili ziwe thabiti, zinazowajibika na
shirikishi” alisema Jaji Mkuu wa Tanzania na kuongeza kuwa kwa kuwaondolea
Majaji na Mahakimu majukumu ya kiutawala kumesaidia kuifanya Mahakama kuwa
inayowajibika zaidi katika kutoa haki kwa wakati.
Prof. Juma alisema
kupitia Mpango Mkakati huo, Mahakama, inakusudia kusogeza huduma kwa wananchi
kwa kujenga kuongeza idadi ya Majengo. Hadi kufikia mwaka 2020 jumla ya majengo
100 ya Mahakama za Mwanzo, 48 Mahakama za wilaya, 14 Mahakama za Hakimu Mkazi,
13 Mahakama kuu na jengo moja la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania
yatajengwa.
Mkutano huo
unahudhuriwa na jumla ya Majaji wakuu kumi na tatu (13) kutoka nchi za Papua
New Guinea, Jersey, Guyana, Uganda, Malawi, Turks Caicos Islands, Swaziland,
Lesotho, Zanzibar, Tanzania, Msumbiji, Kenya na Namibia.
Mkutano huo pia
unahudhuriwa na watu mashuhuri sita ambao ni Marais na Majaji waandamizi wa
Mahakama za juu na Rufaa kutoka nchi za Australia, Afrika Mashariki, Pakistan
na Zambia. Washiriki wengine ni Mahakimu na Majaji kutoka nchi mbalimbali za
Jumuiya ya Madola.
Aidha, mkutano huu ni
wa kihistoria hapa nchini kwa kuwa Tanzania imekuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza
tangu kuanzishwa kwa umoja huo wa Majaji na Mahakimu mwaka 1970. Katika bara la
Afrika mkutano huu unafanyika kwa mara ya pili.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassani
akizungumza katika Mkutano wa kumi wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Nchi za
Jumuiya ya Madola (CMJA), Makamu wa Rais amewataka Majaji na Mahakimu kutoka
katika nchi hizo kupambana na Vitendo vya rushwa.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa
Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya nchi za Madola wakimsikiliza Mhe.
Makamu wa Rais alipokuwa akifungua rasmi Mkutano huo ulioanza rasmi Jumatatu,
Septemba 25 hadi tarehe Septemba 28, 2017
Washiriki wakipiga makofi kumpongeza Mhe. Makamu wa Rais mara baada ya kumaliza kutoa hotuba yake ya Ufunguzi katika Mkutano huo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma akitoa neno katika ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Nchi za Madola. Katika hotuba yake Mhe. Jaji Mkuu amesisitiza juu ya Maboresho ya huduma za Mahakama nchini na kuahidi kuwa hadi kufikia mwaka 2020 Mahakama ya Tanzania itakuwa imejenga Mahakama za Wilaya 48, Mahakama za Mwanzo 100, Mahakama za Mahakimu Wakazi 14 na Mahakama Kuu 13.
Mhe. Jaji Mkuu akiendelea kutoa neno kwa Washiriki (hawapo pichani)
Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga (kushoto) pamoja na Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati wakiwa katika Mkutano huo.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzani, Mhe. Ferdinand Wambali (aliyeketi mbele) mwenye suti nyeusi pamoja na Washiriki wengine wa Mkutano wakiwa katika Mkutano huo.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe.
David Kenani Maraga, (wa kwanza kushoto) akibadilishana mawazo na Majaji Wakuu
wa Tanzania na Zanzibar, katikati ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe.
Omar Othman Makungu.
Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya nchi za Madola (CMJA), Mhe. Jaji John Lowndes akizungumza katika Mkutano huo.
Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Jaji Ignas Kitusi akitoa neno kwa Washiriki wa Mkutano (hawapo pichani), wa pili kulia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kushoto ni Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria.
Meza Kuu ikiongozwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Nchi za Jumuiya ya Madola. (CMJA)
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya Majaji, Mahakimu pamoja na Wasajili Wanawake walioshiriki katika Mkutano huo.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni