Alhamisi, 28 Septemba 2017

MKUTANO WA CHAMA CHA MAJAJI NA MAHAKIMU WA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA MADOLA WAFUNGWA RASMI SEPTEMBA 27, 2017

Na Magreth Kinabo

Majaji na Mahakimu  wa  nchi  Wanachama  wa  Jumuiya  ya Madola wameshauriwa kukabiliana  na  changamoto wanazokumbana nazo katika utendaji  kazi ikiwemo suala la mlundikano wa kesi, maadili na rasilimali fedha, watu na maadili.


Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora-Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suuleiman kwa niaba ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Mhe. Dr. Ali Mohamed Shein Septemba 27, wakati akifunga mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Nchi za Madola, uliofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), uliopo jijini Dar es Salaam.


“Nchi za Afrika  zinatakiwa kuungana  pamoja katika kukabiliana na changamoto za vitendo  vya kigaidi, ikiwemo biashara ya usafirishaji wa binadamu na dawa za kulevya,” alisema Mhe. Ali.


Aidha Waziri  huyo,aliongeza kwamba, Majaji na Mahakimu wanatakiwa kufuatilia  maadili ya taaluma zao na kufuata  sheria , ili  kuweza kuendelea kujenga imani kwa wananchi.

Waziri huyo, alifafanua kwamba kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji kesi  na kuhakikisha  Watumishi wa Mahakama   wanawajibika ipasavyo katika kutekeleza  majukumu yao.

Kwa upande wake, Rais wa Chama na Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Mhe. Jaji Ignas Kitusi amesema kuwa katika mkutano huo wamekubaliana kuwa Majaji na Mahakimu wa nchi hizo za Jumuiya ya Madola waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na miiko ya kanuni zao za ufanyaji kazi ili kutekeleza jukumu la msingi la utoaji haki kwa wananchi.

"Katika Mkutano huu, tumejadiliana masuala mbalimbali jinsi ya kusikiliza kesi kwa namna moja, pamoja na hilo pia tumekubaliana kuuendelea kutekeleza jukumu la utoaji haki kwa kuzingatia miiko na maadili ya kazi yetu," alisema Mhe. Kitusi.

Wajumbe wa mkutano huo, Septemba 28,   wanatarajia kutembelea, Bagamoyo na Zanzibar kwa ajili ya kuangalia vivutio mbalimbali vya Tanzania.

Kwa upande wake Rais wa chama hicho, Mhe. Ignas Kitusi alisema mkutano mwingine, utafanyika mwakani    nchini Australia.  

Jumla ya Majaji Wakuu 13, walihudhuria mkutano huo, miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mkutano huo.

Mkutano huo unahudhuriwa na jumla ya Majaji wakuu kumi na tatu (13) kutoka nchi za Papua New Guinea, Jersey, Guyana, Uganda, Malawi, Turks Caicos Islands, Swaziland, Lesotho, Zanzibar, Tanzania, Msumbiji, Kenya na Namibia. 

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na watu mashuhuri sita ambao ni Marais na Majaji waandamizi wa Mahakama za juu na Rufaa kutoka nchi za Australia, Afrika Mashariki, Pakistan na Zambia. Washiriki wengine ni Mahakimu na Majaji kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola.

Aidha, mkutano huu ulikuwa wa kihistoria hapa nchini kwa kuwa Tanzania imekuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa umoja huo wa Majaji na Mahakimu mwaka 1970. Katika bara la Afrika mkutano huu unafanyika kwa mara ya pili.

  Waziri wa Katiba , Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora-Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman akifunga Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CMJA), kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania ulifungwa rasmi Septemba 27, 2017.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo wakimsikiliza Mgeni rasmi (hayupo pichani), wa tatu kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mhe. Sophia Wambura na katikati ni Mhe. Winifrida Korosso, Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
 Mgeni rasmi akiendelea kutoa hotuba yake katika Mkutano huo.
Washiriki wakimsikiliza kwa umakini.
 Rais wa CMJA (kushoto) akimpongeza Mgeni rasmi mara baada ya kuwasilisha hotuba yake ya kufunga Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Jaji John Lowndes akitoa neno katika Mkutano huo.
(Picha na Mary Gwera)
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni