Na
Lydia Churi-Mahakama
Tanzania kwa mara ya
kwanza inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa mwaka wa Chama cha Majaji na
Mahakimu wa Jumuia ya Madola ambao utafunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Septemba 25 mwaka huu jijini Dar
es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkutano huo wa
siku tatu ni wa kihistoria kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji kwa mara ya
kwanza tangu kuanzishwa kwa umoja huo wa Majaji na Mahakimu mwaka 1970.
Mkutano huo wenye
maudhui “Mahakama Madhubuti, inayowajika na Jumuishi” unalenga kuwajengea uelewa
Majaji na Mahakimu kuhusiana na masuala ya uhuru wa mahakama, mikataba ya
kimataifa, maendeleo ya kisheria, upatikanaji wa huduma ya haki, na maendeleo
ya mahakama na changamoto zake katika kusikiliza mashauri.
Aidha Prof. Juma
alizitaja mada zitakazowasilishwa kwenye Mkutano huo kuwa ni mada kuhusiana na
masuala ya ugaidi, dhima ya wajibu wa Mahakama kwenye menejimenti ya
wanyamapori, kuboresha taratibu za kimahakama, namna ya kukabiliana na ucheleweshwaji
wa mashauri na wajibu wa mahakama katika kusikiliza mashauri ya biashara haramu
ya wanyamapori.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu
wa Tanzania, mada nyingine zitakazojadiliwa wakati wa mkutano huo ni pamoja na
rushwa mahakamani, uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa mahakama na mazingira
ya kazi, namna bora ya kushughulika na maoni ya wanasiasa, vyombo vya habari na
ukosoaji dhidi ya Mahakama.
Katika mkutano huo, jumla
ya Majaji wakuu kumi na tatu (13) watahudhuria ambao watatoka katika nchi za
Papua New Guine, Jersey,Guyana, Uganda, Malawi, Turks Caicos Islands,
Swaziland, Lesotho, Zanzibar, Tanzania, Msumbiji, Kenya na Namibia. Wakati huo
huo Tanzania itawakilishwa na wajumbe 50 ambao ni Majaji na Mahakimu kutoka
Tanzania bara na visiwani.
Mkutano huo pia
utahudhuriwa na watu mashuhuri sita ambao ni Marais na Majaji waandamizi wa
Mahakama za juu na Rufaa kutoka nchi za Australia, Afrika Mashariki, Pakistan
na Zambia. Washiriki wengine ni Mahakimu na Majaji kutoka nchi mbalimbali za
Jumuiya ya madola.
Jaji Mkuu alisema kuwa
mkutano huu ni muhimu kwa Mahakama ya Tanzania na Serikali kwa ujumla kwa kuwa
Majaji na Mahakimu watapata fursa ya kujengewa uwezo na kupata uzoefu kutokana
na mada zitakazojadiliwa ambazo nyingi zina umuhimu mkubwa kwa Tanzania ya leo
ikiwemo mada ya ugaidi na maliasili na wanyamapori.
Alisema Mkutano huo
utatoa fursa kwa nchi kujitangaza kiutalii na vivutio vingine pamoja na kukuza
biashara na kuongeza kipato pamoja na mahakama kujitangaza ndani nan je ya nchi
kuhusian ana shughuli zake, mafanikio iliyoyapata kupitia maboresho
yanayoendelea na Mpango Mkakati wa miaka mitano 2015/16-2019/20.
Wajumbe wa mkutano huo
pia watapata fursa ya kutembelea visiwa vya Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kama nafasi ya kuonyesha umoja na mshikamano wa watanzania.
Hadi sasa washiriki
wapatao 354 wameshathibitisha kushiriki mkutano huo huku baadhi wakiwa wameshawasili.
Nchi hizo ni Uingereza, Australia, Kanada, Uganda, Kenya, Scotland,
Ushelisheli, Jersey, Guyana na Ghana. Nchi nyingine ni Trinidad&Tobago,
Nigeria, Afrika ya Kusini, na Tanzania.
Nchi nyingine ni Cayman
Islands, Marekani, Gambia, Bermuda, Papua New Guine, Lesotho, Malawi, Bahamas,
Malasysia, Wales, Turks & Caicos, Sri Lanka, Singapore, New Zealand, India,
Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini na Cameroon. Nyingine ni Botswana, Zanzibar,
Zambia, Mauritius, Brazil, Msumbiji, Swaziland, na Namibia.
Mkutano wa mwisho wa Chama
cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola ulifanyika mwaka jana nchini Guyana
ambapo Mahakama ya Tanzania ilituma wawakilishi kushiriki mkutano huo.
Wakati
huo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania amesema Mahakama ya Tanzania iko
huru kimfumo na inafanya kazi zake kwa uhuru na kwa uwazi kuliko mhimili
mingine na kuwa changamoto iliyopo ni mtazamo wa jamii juu ya Mahakama.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma akizungumza na
Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya
ya Madola utakaofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania kuanzia Septemba
25-27, 2017. Kushoto ni Jaji Kiongozi waMahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand
Wambali na kulia ni Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Tanzania Mhe.Jaji
Ignas Kitusi.Mhe. Jaji Mkuu ameongelea juu ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji
na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kuanza rasmi, Septemba 25, 2017
katika Ukumbi wa Mikutano wa BOT.
Jaji Kiongozi-Mahakama Kuu
ya Tanzania-Mhe. Ferdinand Wambali akizungumza na Waandishi wa Habari katika
Mkutano huo uliofanyika Septemba 21, Katika Ukumbi wa Maktaba-Mahakama ya
Rufani (T).
Sehemu ya
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni