Na
Mary Gwera, Tabora
Mahakama-Kanda ya
Tabora yaunda Kamati za ndani za Maadili kwa kila ngazi ya Mahakama katika
Kanda hiyo kushughulikia maadili na nidhamu ya Watumishi wa Mahakama katika
Kanda hiyo.
Hayo yalisemwa na Mtendaji, Mahakama Kuu, Kanda
ya Tabora, Bw. Sumera Manoti jana katika mahojiano maalum na Mwandishi wa
habari hii ambapo alisema kuwa hii imetokana na maelekezo/maazimio yaliyotolewa
katika kikao cha Wasajili/Watendaji kilichofanyika mkoani Dodoma Julai, 2016.
“Kamati hizi za nidhamu
ambazo zipo katika kila ngazi ya Mahakama katika mkoa huu ziliundwa tangu mwaka
jana na zimesaidia kurejesha maadili kwa Watumishi wa Kanda hii kwa kiwango
kikubwa,” alisema Bw. Manoti.
Alisema kuwa Kamati
hizi za Maadili ndani ya Mahakama, zinaundwa na baadhi ya Watumishi wa ndani ya
Mahakama ambayo ni Mhe. Jaji Mfawidhi, Naibu Msajili, Mtendaji, na baadhi ya
Wakuu wengine wa vitengo ambao hukaa katika vikao na kujadili na kuwahoji
Watumishi ambao wameonaka kuonesha utovu wa nidhamu.
Bw. Manoti anasema kuwa
endapo mtumishi atabainika kuwa amekiuka taratibu za kazi mfano kwa
kutowahudumia wateja vizuri kwa kutoa lugha chafu na kadhalika, Mtumishi huyo
huketishwa mbele ya Kamati na kujieleza na hatimaye kuwajibishwa aidha kwa
kupewa onyo au vinginevyo.
Anaongeza kuwa Suala la
Maadili na nidhamu nzuri ya kazi katika Ofisi yoyote hupelekea utoaji wa huduma
bora na nzuri inayotolewa kwa wananchi/wanufaika wa huduma husika.
Kwa upande wake Afisa
Malalamiko wa Mahakama Kuu-Tabora, Bi. Aisha Abdallah anasema kuwa idadi ya
malalamiko imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka, anasema kuwa kwa mwaka huu jumla
ya malalamiko 31 kutoka katika ngazi zote za Mahakama katika mkoa huo
yalipokelewa.
“Kabla ya kuanzishwa
kwa Dawati la Malalamiko katika Mahakama hii kulikuwa na malalamiko mengi na hakukuwa
na mfumo unaoeleweka wa pokeaji na ushughulikiaji wa malalamiko hayo, lakini
kwa sasa dawati hili limesaidia na malalamiko yote 31 tuliyoyapokea yamefanyiwa
kazi yote,” alisema. Bi. Aisha.
Kutokana na malalamiko mbalimbali
yaliyokuwa yakitolewa na wananchi wanaotafuta huduma ya haki nchini, Mahakama
ya Tanzania kupitia Muundo wake katika
Sheria Namba. 4 ya Uendeshaji wa Mahakama ya mwaka 2011 (Judicial Administration Act.No.4,2011) ilianzisha Idara maalum ya
Ukaguzi na Malalamiko lengo likiwa ni kushughulikia malalamiko hayo kwa mujibu wa Taratibu na
miongozo iliowekwa, na kwa maana hiyo kila Mahakama ina Dawati maalum la
kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi.
Mtendaji, Mahakama
Kuu-Kanda ya Tabora, Bw. Sumera Manoti akifafanua jambo mahojiano maalum na
Mwandishi.
Wananchi wakisubiri kupata huduma- Mahakama Kuu na ya Hakimu Mkazi-Tabora.
Utunzaji sahihi wa Kumbukumbu (Mahakama Kuu-Tabora): pichani ni muonekano wa Maboksi ambayo ndani yake yamepangwa majalada ya kesi zilizoisha, majalada hayo yamepangwa kulingana na mwaka, utunzaji sahihi wa majalada ya kesi na mengineyo hurahisisha upatikanaji wa kumbukumbu na hatimaye kurahisisha kazi ya utoaji haki nchini kufanyika kwa ufasaha kutokana na kwamba hutegemea ushaidi na nyaraka ili kesi iweze kusonga mbele na hatimaye kukamilika kwa wakati.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni