Na
Mary Gwera, Tabora
Uhairishwaji wa kesi wa
mara kwa mara unaotolewa na baadhi ya Mawakili umeelezwa kuwa moja ya sababu
zinazopelekea kutofikiwa kwa malengo ya umalizaji wa mashauri kwa wakati.
Hayo yalisemwa na Jaji
Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Mhe. Sam Rumanyika katika kikao
kilichoketi baina ya Mahakama katika Kanda hiyo na Wadau wake Oktoba 03, 2017
katika Ofisi ya Mhe. Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora.
“Lengo la kuwaita
katika kikao hiki cha pamoja ni kukaa kama ndugu tukiwa na nia moja ya kumaliza
mlundikano wa mashauri yaliyopangwa kusikilizwa katika mfululizo wa vikao saba
(7) vya kuondoa mlundikano wa mashauri ambavyo vitaanza rasmi kesho, Oktoba 04,
2017” alisisitiza Mhe. Rumanyika.
Kikao hicho cha kabla
ya kuanza kwa kikao maalum cha kusikiliza mashauri ‘pre session meeting’ kiliwahusisha
wajumbe wafuatao; Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Naibu
Msajili-Kanda ya Tabora, Mtendaji-Mahakama Kuu-Tabora, Wanasheria wa Serikali
na wa Kujitegemea, Mkuu wa Gereza la Uyui na RCO.
Kwa upande wake Naibu
Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Mhe. Sharmillah Sarwatt alisema kuwa
lengo la Kikao hicho na Wadau ni kujipanga kwa pamoja kuhakikisha mashauri yote
ya mlundikano yaliyopangwa kusikilizwa katika vikao saba yanamalizika kufikia Desemba
15 mwaka huu.
“Lengo la Kanda yetu ya
Tabora ni kuhakikisha kuwa tunamaliza mlundikano wa mashauri na Mkakati Mkuu
tulionao kama Kanda ni kumaliza mashauri mengi kuliko yanayopokelewa; ili
yanayobakia yawe machache,” alifafanua Mhe. Sarwatt.
Akiongelea juu ya kikao
maalum cha kuondoa mashauri kinachoanza rasmi Oktoba 04, mwaka huu, Mhe. Sarwatt
alisema kuwa jumla ya kesi 14 za mauaji (katika kikao cha kwanza) zimepangwa kwa
ajili usikilizwaji wa awali (PH) na hatua awali za kuwahoji watuhumiwa ‘Plea
taking.’
Aidha; Naibu Msajili
huyo aliongeza kuwa katika mfululizo wa vikao hivyo saba (7) vya kuondoa
Mlundikano, jumla ya kesi 82 za aina tofauti za mlundikano zimepangwa
kusikilizwa na kumalizwa ifikapo Disemba 15, 2017 na kuongeza kuwa kesi ya muda
mrefu zaidi ambayo pia imepangwa kusikilizwa katika vikao hivyo,ni ya mwaka
2011 ambayo ipo katika hatua ya mwisho ya kutoa hukumu.
Hata hivyo; Mhe.
Sarwatt alisema kuwa mchakato cha kuondoa mlundikano wa mashauri kwa Kanda ya
Tabora, ulianza kwa muda mrefu hata kabla ya kutolewa kwa maagizo kutoka Makao
Makuu ya kumaliza mlundikano wa kesi hali ambayo imeonyesha mafanikio kwa kiasi
kikubwa.
Akitoa mfano wa
uondoshaji wa mashauri kwa takwimu, Mhe. Sarwatt alisema kuwa kwa mwaka 2015
jumla ya mashauri 894 yalipokelewa Mahakamani na mashauri 1030 yalimalizika na
kubaki mashauri 795, hali hii inayoonesha kuwa kesi zilizofunguliwa zilimalizika
zote na baadhi ya kesi za mlundikano za kipindi cha nyuma kushughulikiwa.
“Kwa mwaka 2016, jumla
ya kesi 1347 zilifunguliwa, zilizomalizwa ni kesi 1464 na zilizobaki ni kesi
621, na kwa mwaka huu 2017 hadi kufikia mwezi Septemba jumla ya kesi 1062
zilifunguliwa huku 878 kumalizwa na kubaki na jumla ya kesi 526,” alifafanua
Naibu Msajili.
Akiongelea juu ya
mkakati wa kupambana na mlundikano, Mhe. Sarwatt alisema kuwa wamejiwekea
utaratibu kama Kanda wa kufanya ufuatiliaji wa takwimu za umri wa mashauri kwa
wiki ‘weekly tracking’ ili Majaji na Mahakimu waweze kushughulikia/kuyapa
kipaumbele mashauri yanayokaribia umri wa kuwa mlundikano ‘back stopping.’ Pamoja
na kufanya mikutano ya wadau ya mara kwa mara ili kuongea lugha moja ya
kutokuwa na mlundikano.
“Lengo letu Kanda ya
Tabora ni kuondoa kesi zote za Mlundikano ili tuweze kubaki na kesi
zilizofunguliwa kwa mwaka huu 2017 tu,” alisisitiza Mhe. Sarwatt.
Katika kuhakikisha kuwa Mahakama ya Tanzania
inatekeleza wajibu wake wa utoaji haki kwa wananchi na vilevile inatekeleza
ipasavyo nguzo namba mbili (2) ya Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) wa
Mahakama (2015/2016-2019/2010) ya Upatikanaji na utoaji wa Haki kwa
wakati, Majaji Wafawidhi kupitia
Mkutano wao uliofanyika tarehe 15 na 16, Septemba,2017 waliazimia kuwa Mahakama
zote nchini zimalize mlundikano wa mashauri yote ya muda mrefu ifikapo Desemba
15, 2017.
Pichani ni Muonekano wa sehemu ya jengo la Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora
Jaji Mfawidhi,Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Mhe. Sam Rumanyika akiongea jambo na Wajumbe/Wadau wa Mahakama (hawapo pichani) katika kikao cha kujadili juu ya ushirikiano wa pamoja wa kuondosha mlundikano wa mashauri.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili-Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Kikao kikiendelea.
Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kushoto) akiongea jambo na Wadau (hawapo pichani), kulia ni Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Mhe. Sam Rumanyika akisikiliza kwa umakini.
RCO wa Mkoa wa Tabora, SSP Simon Maigwa (katikati) akichangia jambo katika kikao hicho.
RCO wa Mkoa wa Tabora, SSP Simon Maigwa (katikati) akichangia jambo katika kikao hicho.
Mtendaji-Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Bw. Sumera Manoti (kushoto) akichangia jambo katika kikao hicho. Wajumbe wote wa kikao hicho wameridhia kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha zoezi la uondoshaji wa Mlundikano wa Mashauri.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni