Ijumaa, 6 Oktoba 2017

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KIGOMA YAKUTANA NA WADAU WAKE WA HAKI JINAI KUJADILI NAMNA YA KUSUKUMA MASHAURI



 Na Mary Gwera, Kigoma
KAIMU Hakimu Mkazi Mfawidhi-Mahakama ya Hakimu Mkazi/Mkoa-Kigoma, Mhe. Flora A. Mtarania amewasihi Wadau wa Haki Jinai wa mkoa huo kushirikiana na Mahakama ili kumaliza mashauri yote yaliyofunguliwa mwaka huu ifikapo Desemba mwaka huu.

Mhe. Mtarania aliyasema hayo mapema Oktoba 06 katika kikao maalum cha Kusukuma Mashauri ‘Case Flow Management Meeting’ kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mahakama hiyo ya Mkoa.

 “Mpaka sasa Mahakama ya Mkoa-Kigoma kuna jumla ya mashauri 24 ambayo bado hayajatolewa maamuzi ‘pending cases’ huku 16 yakiwa mashauri ya Madai na nane (8) ya Jinai, na kwa upande wa Mahakama za Wilaya kuna jumla ya mashauri 103 ambayo bado hayajakamilika huku mashauri 79 yakiwa ya Jinai na 24 mashauri ya Madai,” alisema Mhe. Mtarania.

Alisema kuwa kesi hizo ambazo zina wastani wa kati ya miezi mitatu (3) hadi miezi sita (6) tangu kufunguliwa kwake Mahakamani zimekuwa zikikwama kwa sababu mbalimbali ambazo ni pamoja na kutopatikana kwa Mashahidi hali inayopelekea haki kutopatikana kwa wakati, upelelezi kutokamilika kwa wakati, fedha za Mashahidi kutotosheleza uhitaji na kadhalika.

Aliongeza kuwa ni vyema Suala ya mchakato wa usikilizwaji wa kesi hadi ukamilikaji wake lifanyike kwa ushirikiano kati ya Mahakama na Wadau wa Haki Jinai ili haki ipatikane kwa wakati stahiki.

Aidha; Mhe.Mtarani alisema kuwa lengo la vikao vya pamoja na Wadau wa Mahakama ni kujadili namna ya kusukuma mashauri ili yaweze kumalizika kwa wakati, kupeana mikakati ya kushughulikia mashauri na kuhakikisha kuwa kila mtu anatimiza wajibu wake katika mchakato mzima wa usikilizaji wa mashauri.

Mhe. Mtarania aliendelea kusema kuwa vikao hivi hufanyika kila baada ya miezi mitatu na hiki ni kikao cha tatu (3) kufanyika kwa mwaka huu, huku akieleza kuwa kabla ya kikao hiki cha ngazi ya Mkoa kufanyika huwa kuna vikao vya kusukuma Mashauri ambavyo hufanyika kwa ngazi za Mahakama za Wilaya ili kuwasilisha mipango yao katika kikao cha Wadau cha Mkoa.

“Kimsingi kwa hatua tuliyofikia sasa vikao hivi vimesaidia kumaliza  mashauri yaliyokuwa yalikaa muda mrefu Mahakamani kutokana na sababu mbalimbali zilizosababishwa  na Wadau,” alieleza Mhe. Mtarania.

Kikao kilihudhuriwa na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi ambaye ndiye Mwenyekiti, Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi, Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya za Kasulu na Kibondo, Mkuu wa Takukuru-Mkoa, Afisa Uhamiaji wa Mkoa, Mkuu wa Upelelezi (RCO), Afisa Ustawi wa Jamii, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea na Mtendaji wa Mahakama-Kigoma.

Hata hivyo, Wajumbe wa Kikao hicho waliazimia kufanya kazi kwa kushirikiana ili ifikapo Desemba 30, kesi ambazo hazijakamilika ziwe zimekamilika.
 Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi-Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Flora Mtarania (kulia) akiongoza kikao cha Kusukuma Mashauri ‘Case Flow Management Meeting’kilichofanyika katika Ukumbi wa Mahakama ya Mkoa Kigoma, Oktoba 06,2017.
 Kikao kikiendelea
Wajumbe wakiwa katika kikao hicho (katikati) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi-Mahakama ya Wilaya-Kasulu, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama-Kigoma, Bw. Humphrey Paya na wa kwanza kushoto ni Mwakilishi kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii, Manispaa ya Kigoma.
Wajumbe wakiwa katika kikao.
Mtendaji-Mahakama ya Mkoa Kigoma, Bw. Humphrey Paya (kulia) akichangia jambo katika kikao hicho.

Wadau wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kikao cha Kusukuma mashauri ya Mahakama-Mkoani Kigoma.
Muonekano wa nje wa jengo la Mahakama ya Mkoa na Wilaya-Kigoma.
Muonekano wa sehemu  ya jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi-Kigoma,hata hivyo jengo hilo ni chakavu hivyo linahitaji ukarabati ili liendelee kukidhi mazingira ya bora ya kutolea haki kwa wananchi.
Baadhi ya Wananchi wakisubiri kupata huduma ya Mahakama ya Mkoa-Kigoma. 
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni