Alhamisi, 16 Novemba 2017

JAJI MKUU MGENI RASMI MAHAFALI CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA-LUSHOTO

           CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO
                                     
         TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 SHEREHE ZA MAHAFALI YA 17 KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kinatarajia kufanya sherehe ya Mahafali ya Kumi na Saba kwa Wahitimu wa mwaka wa masomo 2016/17 mnamo tarehe 17 Novemba, 2017. Jumla ya Wahitimu 292 wanatarajiwa kutunukiwa vyeti kwa ngazi ya Astashahada ya Sheria na Stashahada ya Sheria. Jumla ya wahitimu wa ngazi ya Stashahada ya Sheria ni 142 na wale wa Astashada ya Sheria ni 150. Sherehe hiyo ya Mahafali itafanya jumla ya idadi ya Wahitimu wa Chuo kuwa 5283 tangu kufanyika kwa Mahafali ya kwanza ya Chuo mwaka 2001.
Mgeni rasmi katika sherehe ya Mahafali hiyo atakuwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye pamoja na kuwatunuku vyeti Wahitimu, atatunuku vyeti kwa Wanachuo bora Kitaaluma, Viongozi Bora wa serikali ya Wanachuo. Mwisho atazindua machapisho mawili ya Chuo ambayo ni, Jarida la Kitaaluma la Chuo na Jarida la Habari la Chuo.
Mahafali haya yatatanguliwa na tukio la kuwakaribisha Wahitimu wa Chuo wa miaka iliyopita, siku ya tarehe 16 Novemba 2017 ambapo watafanya kikao cha kwanza kuzindua Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto itakayoitwa; (IJA Alumni).

Imetolewa na Kitengo cha Mahusiano kwa Umma
S. L. P. 20 Lushoto
Simu: 255-27-2660133
Barua pepe: info@ija.ac.tz
Tovuti: www.ija.ac.tz

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni