Jumanne, 28 Novemba 2017

UTARATIBU WA USULUHISHI (MEDIATION) “MUAROBAINI” WA KUMALIZA MLUNDIKANO WA KESI MAHAKAMANI


Na Mary Gwera, Mahakama
MAWAKILI nchini washauriwa kukuza na kuendeleza Usuluhishi ‘Mediation’ badala ya kung’ang’ania utaratibu wa kawaida wa Usikilizaji wa Mashauri hali inayowapotosha Wadaawa/Wananchi kwa kuona kuwa utaratibu huo haufai.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni katika mahojiano maalum na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi ‘Mediation centre’ Mhe. Rose Teemba ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Mhe. Teemba alisisitiza kuwa Mawakili wanatakiwa kubadili mtazamo kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa Usuluhishi kwani  kuna faida nyingi chanya zinazotokana na Usuluhishi pindi unapofaulu.

“Mawakili kama sehemu ya Maafisa wa Mahakama, wanapaswa kukuza na kuendeleza Usuluhishi ‘Mediation’ badala ya kung’ang’ania utaratibu wa kawaida wa usikilizaji wa Mashauri,” aliongeza Mhe. Teemba.

Akizungumzia kuhusu Faida za Usuluhishi, Mhe. Jaji Teemba alisema kuwa Usuluhishi ukishinda/kufanikiwa ndio unakuwa mwisho wa shauri lenyewe. Jaji/Msuluhushi huandaa tunzo ‘decree’ ambayo ina hadhi kama ile inayotokana na utaratibu wa usikilizaji wa shauri la madai. Wadaawa hupewa nakala ya tunzo ‘decree.’

Aidha; Mhe. Teemba anabainisha juu ya faida nyingine za usuluhishi kuwa ni pamoja na kusaidia kupunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani, vilevile husaidia kujenga mahusiano mazuri baina ya Wadaawa kwa kuwa Wadaawa hao wanakuwa wametengeneza hukumu yao wenyewe.

Usuluhishi hupunguza gharama za uendeshaji wa kesi za Madai na vilevile huokoa muda. Badala ya wadaawa kufika Mahakamani kila wakati na kwa muda mrefu kusikiliza kesi, Usuluhishi huchukua masaa  au siku chache mpaka kufikia muafaka” alifafanua Mhe. Jaji Teemba.

Mhe. Teemba anasema Suala la Usuluhishi ni takwa la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107A, inayosomeka ‘Katika kutoa maamuzi ya Mashauri ya Madai, kwa kuzingatia Sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo: yaani Kukuza na kuendeleza USULUHISHI baina ya wanaohusika katika migogoro.’
Pichani ni Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu, Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Rose Teemba.

Nini maana ya Usuluhishi?
Usuluhishi ni hatua mojawapo katika mwenendo wa kesi za madai ambapo wahusika katika kesi chini ya usaidizi wa usuluhishi (Jaji au Hakimu Msuluhishi) wanajadiliana kukubaliana, kuafikiana, kumaliza mgogoro wa shauri lao kwa namna wanavyoona inafaa bila ya kulazimika kuingia kwenye uendeshaji wa kesi hiyo ya madai kwa kutoa ushahidi/kuita mashahidi.

Kwa lugha nyepesi unaweza pia ukaelezea Usuluhishi kuwa ni mchakato wa majadiliano ya kujaribu kumaliza mgogoro wa madai kwa maafikiano ya ridhaa ya kila Mdaawa.

“Katika kutekeleza Ibara hiyo ya Katiba Mahakama ya Tanzania ikaona ni vyema kuanzisha kituo hiki maalum, na kwa kuanzia hushughulikia Mashauri yanayoanzia Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, ambayo ina mashauri mengi ya madai” alisema Jaji huyo.

Mhe. Jaji Teemba anaongeza kuwa Dar es Salaam ilichaguliwa kwanza kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mashauri; na kuongeza kuwa Kituo cha Usuluhishi ‘Mediation centre’ kinashughulika na Usuluhishi wa Mashauri ya Madai yanayohusika na ambayo yapo tayari kwa usuluhishi.

“Baada ya hati za Madai kukamilika kuwasilishwa Mahakamani ‘Pleadings’ Shauri linatakiwa lipelekwe kwa Msuluhishi ili kujaribu kuwasuluhisha Wadaawa  na kwa kawaida usuluhishi unatakiwa kufanyika kwa kipindi kisichozidi siku 60,” alifafanua Jaji Teemba.

Kwa mujibu wa Jaji Mfawidhi huyo anasema kuwa katika zoezi la Usuluhishi linahusisha Wahusika wa shauri husika/Wadaawa , Mawakili wao kama wapo, Jaji Msuluhishi na katika usuluhishi mbinu mbalimbali hutumika kuhakikisha Wadaawa hao wanafikia suluhu (successful mediation).

Mhe. Teemba anafafanua zaidi kuwa moja ya mbinu wanazotumia katika Usuluhisho ni pamoja na kuwaweka Wadaawa katika Vyumba maalum ‘Break out Rooms’ kila upande peke yake kwa ajili ya tafakuri ya kina kuhusu majadiliano ili kufikia Suluhu.

Mhe. Jaji Mfawidhi anaongeza kuwa pindi Wadaawa wanapofikia Suluhu, Wadaawa hao hupatiwa nakala ya Makubaliano waliyofikia wote kwa pamoja ambayo yanatiwa sahihi na pande zote za Mgogoro/kesi pamoja na Mawakili wao kama wapo na mwishoni inasainiwa na Jaji Msuluhishi.

Mhe. Teemba anaongeza kuwa Usuluhishi ukishinda/ukifanikiwa ndio unakuwa mwisho wa shauri lenyewe. Pia, Jaji huandaa tunzo inayoendana na makubaliano yaliyofikiwa na Wadaawa pamoja na utekelezaji wake ambao huwapatia Wadaawa pamoja na Mawakili wao kama wapo.

“Hata hivyo baada ya Usuluhishi kukamilika na kufaulu Wadaawa hupatiwa Hati ambayo lazima ionyeshe tarehe ya makubaliano, Mhuri wa Kituo cha Usuluhishi ikionyesha pia na namba ya Shauri na majina ya Wadaawa na mambo yote waliyokubaliana, na makubaliano hayo yataonyesha maeneo yote ya maafikiano na utekelezaji wa makubaliano,” alifafanua Mhe. Jaji Teemba.

Kwa upande wake, Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi ‘Mediation centre’, Mhe. Saidi Ding’ohi anasema licha ya Kituo hiki kuanzishwa, Suala la Usuluhishi pia hufanyika katika Mahakama za Wilaya, Mahakama za Mahakimu Wakazi (RM’s Courts) pamoja na Mahakama Kuu, tofauti ni kwamba kwenye mahakama zingine hakuna jaji au hakimu mahususi anayeshughulika na usuluhishi pekee; jaji au hakimu msuluhishi anakuwa na mashauri mengine ya kusikiliza.
 Pichani ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Saidi Ding’ohi.
Mhe. Saidi Ding’ohi anasema kituo hiki nacho kina jukumu la kupambana na mlundikano wa Mashauri kwa kasi kama ilivyo katika  Mahakama nyingine za ngazi mbalimbali.

Mhe. Ding’ohi anasema kuwa baada ya kikao cha Wahe. Majaji Wafawidhi kilichofanyika Arusha Septemba 16 na 17, 2017 kumalizika, na ambacho kilichoazimia, pamoja na mambo mengine, kusikiliza na kumaliza kesi zote za muda mrefu. Kituo hiki pia kilitekeleza agizo hilo na kuweka mikakati ya kushughulikia Mashauri yaliyowasilishwa kwa ajili ya Usuluhishi kwa haraka zaidi.

“Baada ya agizo hilo, Kitengo hiki pia kiliamua kufanya utaratibu wake wa ndani wa kuandaa vikao vya mfululizo kwa ajili ya kufanya usuluhishi na zoezi hilo lilianza rasmi Oktoba 9, 2017,” alisema Bw. Saidi Ding’ohi. 

Kwa mujibu wa Naibu Msajili huyo anasema, Usuluhishi ukifanyika mapema husaidia kutokwamisha hatua zingine za usikilizaji Mashauri, hasa mashauri ya mlundikano.
Bw. Ding’ohi anaongeza kuwa katika vikao hivyo jumla ya mashauri 34 yalipangwa kwa ajili ya kusuluhishwa.

“Lengo tulilo nalo ni kuhakikisha kuwa Mashauri yote 34 yaliyokuwepo yawe yamefanyiwa usuluhishi hadi kufikia Novemba 22 sambasamba na yale yatakayokuwa yanaingia; kipaumbele ikiwa ni mashauri ya mlundikano (back log),” alisisitiza Bw. Ding’ohi.

Akizungumzia juu ya idadi ya Mashauri yaliyosuluhishwa mwaka huu, Naibu Msajili huyo alisema kuwa kwa mwaka huu mpaka kufikia October, 2017 jumla ya Mashauri 170 yalipokelewa kwa ajili ya usuluhishi ambapo kati ya hayo Mashauri 37 yalifaulu usuluhishi (successful mediation). 

Akiongelea juu ya takwimu za Mashauri yaliyowasilishwa katika Kituo hicho toka kuanzishwa kwake Julai 2015 mpaka Oktoba 2017, Bw. Ding’ohi anasema kuwa jumla ya Mashauri 504 yalipokelewa kutoka Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam. Yaliyosuluhishwa kati ya hayo, ni jumla ya Mashauri 485 ambayo ni asilimia 96 ya mashauri yote yaliyopokelewa.

“Kati ya Mashauri 485 yaliyosuluhishwa, jumla ya mashauri 112 usuluhishi wake ulifaulu (successful mediation) ambayo ni sawa na asilimia 23 (23%).” alifafanua Naibu Msajili.

Aliongeza kuwa Mashauri yaliyofaulu kwa kiwango Fulani (partly successful) yalikuwa ni sita (6) kwa kipindi hicho hicho ambayo ni asilimia moja (1%) na mashauri ambayo usuluhishi ulishindikana/ulishindwa (failed mediation) yalikuwa 367 ambayo ni sawa na asilimia 76.

“Mpaka kufikia Oktoba, 2017 yalibaki mashauri 19 sawa na asilimia nne (4%). Mashauri yanayoshindikana kusuluhishika hurudishwa Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam haraka ili kuendelea na utaratibu wa kawaida wa usikilizaji wa kesi,” alieleza Bw. Ding’ohi.

Aidha; Bw. Ding’ohi alisema kuwa Usuluhishi haufanikiwi kwa kiwango ambacho tungetaka kwa maana ya kuwa na asilimia kubwa zaidi ya ufaulu wa usuluhishi kwa sababu kadhaa, kubwa zaidi ikiwa ni Uelewa mdogo wa Wadaawa kuhusu umuhimu wa Usuluhishi. Mtazamo wa watu wengi ni wa kimezoea kwamba hukumu halali na bora ni ile inayotokana na usikilizaji wa kesi kwa njia ya kawaida. 
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kitengo cha Usuluhishi (aliyeketi mbele) akiwa katika moja ya mazungumzo ya usuluhishi baina ya Wadaawa pamoja na Mawakili wao.
“Kimsingi utaratibu wa usuluhishi ukihimizwa na kutumika vizuri unaweza kuwa ni muarobaini wa kumaliza tatizo la mlundikano wa kesi mahakamani. Mahakama kupitia mpango mkakati wake wa 2015/2016 hadi 2019/2020 imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia usuluhishi katika kumaliza migogoro kwa kesi za madai zinazoandikishwa mahakamani” alibainisha Bw. Ding’ohi.

Akiongelea kwa undani kuhusu Kituo cha Usuluhishi, Bw. Ding’ohi anasema kuwa Kituo hiki kilianzishwa Julai 1, 2015 na kilianzishwa ili kufanya shughuli zote za Usuluhishi katika Mashauri ya Madai. Lengo ni kwamba kuwe na jaji mahususi ambaye jukumu lake ni kuendesha usuluhishi pekee.

“Kituo hiki bado kinafanya Usuluhishi kwa Mashauri yanayoanzia mahakama kuu kanda ya Dar es salaam pekee. Hata hivyo ufanisi wa kituo hiki unaweza kupelekea kusambaa huduma za kituo kwa Mahakama Kuu nchi nzima, ingawa usuluhishi unaendelea kufanyika katika Mahakama zetu zote,” alisema Naibu Msajili huyo.

Naye Bi. Nancy Mosha, Wakili wa kujitegemea, anasema kuwa Usuluhishi ni muhimu katika mustakabali mzima wa kuhakikisha kupungua kwa mlundikano wa Mashauri Mahakamani na vilevile husaidia kupunguza muda kwa Mahakama na pande wa Wadaawa pia.

“Suala la Usuluhishi (Mediation) ni kitu kizuri kwa sababu yanafanyika kirafiki na maridhiano yanayofikiwa yanakubalika na pande zote mbili bila kinyongo chochote,” alisema Bi. Mosha.

Bi. Mosha aliendelea kusema kuwa Usuluhishi ni njia sahihi ya kumaliza migogoro baina ya Wadaawa, hivyo kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa umma ili watambue faida za Usuluhishi (Mediation).

Aidha; nilifanikiwa kukutana na Baadhi ya Wadaawa waliosuluhishwa katika Kituo cha Usuluhishi (Mediation centre), Bw. Mohamed Hamis Mtulia anasema kuwa utaratibu wa maridhiano ni mzuri na uboreshwe na kuongeza kuwa jukumu la maridhiano ni la pande zote mbili.
Wadaawa wakipeana mikono huku wakiwa na nyuso za furaha mara baada ya kufikia muafaka baina yao baada ya mazungumzo ya usuluhishi yaliyoongozwa na Jaji Msuluhishi kuzaa matunda.

“Binafsi nasema kwamba chombo hiki ni kizuri kwani maamuzi yanafikiwa kwa maridhiano ya pamoja hivyo ni muhimu kuheshimu chombo cha Usuluhishi, tusiogope maridhiano ,” alieleza Bw. Mtulia.

Naye Mdaawa Mwenza waliokuwa na kesi na Bw. Mtulia, Bw. Charles Mallya anasema kuwa usuluhishi unasaidia kupunguza muda wa kwenda Mahakamani kufuatilia kesi hivyo kuna haja ya kuelimisha umma juu ya Kitengo hiki ili wananchi waweze kukitumia.
Muonekano wa mbele wa Ofisi ya Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi, Ofisi za Kituo hiki zinapatikana ‘floor’ ya tatu katika jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni