Na
Mary Gwera, Zanzibar
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim H. Juma ashauri juu ya uwezekano wa kuwa na Kanuni za pamoja
zitakazosimamia Sheria ya Biashara na Uwekezaji ‘Trade Investment Regulations’ kati ya
Tanzania na China zitakazowezesha ukuaji wa uchumi ambao utasaidia kuleta
maendeleo baina ya nchi hizi mbili.
Aliyasema hayo, Desemba
1, katika maongezi maalum na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe.
Zhao Dacheng, pindi alipotembelewa na Naibu Waziri huyo Mahakama Kuu-Zanzibar
ambapo Mhe Jaji Mkuu anaendelea na Vikao maalum vya Mahakama ya Rufani ‘court
session.’
Mhe. Jaji Mkuu alisema
kuwa; China ni nchi ambayo tayari imeshapiga hatua kubwa kiuchumi na
kimaendeleo, hivyo kuwepo kwa Kanuni wezeshi za Biashara Uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (2) utasaidia ukuaji
wa uchumi wa Tanzania pia.
“Ni vyema kuangalia juu
ya uwezekano wa nchi zetu; Tanzania na China kuwa na kanuni zinazofanana
zitakazotoa muelekeo wa jinsi ya kuwekeza kwa manufaa ya pande zote mbili,”
alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng aliafiki ushauri huo
uliotolewa na Mhe. Jaji Mkuu na kumtaka kuendelea na hatua za awali za
uwasilishaji wa pendekezo hilo kwa taratibu zinazotakiwa kufanyika ili
kufanikisha utekelezaji wa ushauri uliotolewa.
Aidha; Mhe. Jaji Mkuu
pia alimueleza Naibu Waziri huyo juu ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati
unaoendelea kufanyika ndani ya Mahakama kwa kutaja baadhi ya vipaumbele ambavyo
Mahakama imejiwekea ikiwa ni pamoja na utoaji wa Mafunzo kwa Watumishi wa
Mahakama, Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na
kadhalika.
Aliongeza kuwa Mahakama
ya Tanzania inakusudia pia kuwafikishia huduma ya Mahakama Watanzania wote kwa
ngazi ya Kata.
“Kwa sasa changamoto
kubwa tunayokabiliana nayo ni jinsi ya kuwafikishia huduma ya Mahakama wananchi
wote, tuna zaidi ya Kata 3000, lakini Mahakama ya Tanzania ina majengo ya
Mahakama za Mwanzo yasiyozidi 900, hivyo Mpango uliopo ni kufikisha huduma za
Mahakama kwa wananchi wote ili kuwaondolea aza za umbali pindi wanapotafuta
haki zao,” alifafanua Mhe. Jaji Mkuu.
Naye, Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng ameahidi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa Mahakama katika uendeshaji wa shughuli zake.
“China ni nchi
inayoendelea kukua kiuchumi hivyo tunapaswa kutoa mchango kwa Tanzania pia ili kuendelea kukua kimaendeleo,”
alisema Mhe. Zhao Dacheng.
Naibu Waziri huyo aliyeambatana
na Ujumbe wa Wakurugenzi na Maafia sita (6) kutoka Wizara ya Katiba na Sheria
ya Watu wa China walionana na Mhe. Jaji Mkuu lengo likiwa ni kuimarisha
ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili; Tanzania na China.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Juma akimkaribisha Naibu Waziri wa Jamhuri ya Watu wa China,
Mhe. Zhao Dacheng pindi alipowasili katika Ofisi ya Jaji Mkuu-Mahakama Kuu
Zanzibar.
Naibu Waziri wa Jamhuri
ya Watu wa China, Mhe. Zhao Dacheng (katikati) akiongea jambo na Mhe. Jaji Mkuu
pindi alipomtembelea Desemba 01, 2017.
Majadiliano yakiendelea;
pichani ni baadhi ya Wajumbe walioambatana na Naibu Waziri huyo, mbali na
Wajumbe hao pia kuna Wajumbe kutoka Mahakama ya Tanzania na Wizara ya Katiba na
Sheria, wa pili kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Hussein Kattanga na wa kwanza kushoto ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Katiba na
Sheria-Tanzania.
Wajumbe wakifuatilia
kwa umakini majadiliano hayo.
Naibu Waziri wa Jamhuri
ya Watu wa China, Mhe. Zhao Dacheng akipitia nakala ya Kitabu cha Mpango Mkakati
wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/2016-2019/2020) alichozawadiwa na
Mhe.Jaji Mkuu wa Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Juma akichangia jambo katika majadiliano baina yake na Naibu
wa Waziri wa Katiba na Sheria wa China.
Mhe. Jaji Mkuu
akifurahia zawadi ya picha aliyopatiwa na Mgeni wake.
Picha ya pamoja baada
ya Majadiliano: wa nne kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Juma, katikati ni Naibu Waziri wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Zhao Dacheng,
wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga
pamoja na Wajumbe waliombatana na Naibu Waziri.
(Picha na Mary Gwera, Zanzibar)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni