Na Mary Gwera
Mtaalamu Mwandamizi wa Maboresho ya Utumishi
wa Umma kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Waleed Malik amesifu Mahakama ya
Tanzania kwa kasi nzuri inayoenda nayo katika utekelezaji wa Mradi wa Maboresho
ya Huduma za Mahakama pamoja na Mpango Mkakati wa miaka mitano
(2015/16-2019/2010) wa Mahakama.
Bw. Malik aliyasema hayo mapema Desemba 11 ndani
ya Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Kitengo cha Usimamizi wa Mradi wa Maboresho
ya Mahakama (JDU) jijini Dar es Salaam, katika kikao cha Majumuisho baada ya ziara ya Ujumbe Benki
ya Dunia (WB) na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.
“Kufuatia ziara tuliyofanya ya kukagua na kujionea maendeleo ya
utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama, tumeona mnaendelea
vizuri na ninapenda kuwapongeza kwa ushirikiano wenu, kwani Mahakama ni moja
kati ya Taasisi zinazokwenda vizuri katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali inayofadhiliwa
na Benki ya Dunia,” alieleza Bw. Malik.
Mbali na Pongezi, Bw. Waleed aliwasihi
Viongozi wa Mahakama kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuwapa mafunzo Watumishi
wake juu ya matumizi ya TEHAMA yatakayowezesha maboresho yanayofanyika
kutekelezeka vizuri.
“Ni muhimu kuwapa mafunzo ya TEHAMA Watumishi
wa Kada mbalimbali wa Mahakama ili Mifumo ya Kiielektroniki itakayowekwa iweze
kutumiwa na Watumishi bila shida yoyote,” aliongeza Mtaalam huyo kutoka Benki
ya Dunia.
Aliongeza pia juu ya umuhimu wa kuimarisha
mawasiliano/utoaji taarifa kwa jamii ili wananchi waweze kujua juu ya maboresho
mbalimbali yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Akiongea kwa niaba ya Mtendaji Mkuu-Mahakama
ya Tanzania, Mtendaji Mahakama ya Rufani, Bw. Sollanus Nyimbi aliahidi kufanyia
kazi maelekezo na changamoto zilizoibuliwa kutoka ujumbe wa Benki ya Dunia ili
kuendana na matakwa ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama.
“Tunashukuru kwa pongezi, lakini pia tunaahidi
kufanyia kazi yale yote mliyoyaibua lengo likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji
haki nchini,” alisema Bw. Nyimbi.
Ujumbe wa Benki ya Dunia uliwasili nchini Desemba 04, lengo likiwa ni kukagua
utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama pamoja na Mpango
Mkakati wa miaka mitano (2015/16-2019/2010) wa Mahakama.
Ujumbe huo pia ulipata wasaa wa kutembelea
Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
kilichojengwa eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mradi wa Ujenzi wa
Mahakama ya Mwanzo Kawe pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya
Kigamboni.
Pichani
ni Mtaalamu Mwandamizi wa Maboresho ya Utumishi wa Umma kutoka Benki ya Dunia
(WB), Bw. Waleed Malik akizungumza katika kikao hicho.
Bw.
Malik akiendelea kuzungumza na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania,
Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mradi wa Maboresho ya Mahakama (JDU),
Mhe. Zahra Maruma.
Baadhi
ya Wajumbe wa Menejiment wakiwa katika kikao hicho.
Wajumbe
wakichukua maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mtaalam kutoka Benki ya Dunia, Bw.
Waleed Malik.
Bw.
Malik akiendelea kutoa mada katika kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa Mradi
kilichofanyika mapema Desemba 11.
Baadhi
ya Wajumbe wa Menejimenti wakifuatilia mada kwa umakini.
(Picha na Mary Gwera)
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni