Na
Lydia Churi-Mahakama Kigoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma amewaagiza Mahakimu wote nchini
kutoa bure nakala za hukumu kwa wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa Haki.
Akizungumza
wakati wa ziara yake katika Mahakama za wilaya ya Uvinza na Kasulu mkoani
Kigoma leo, Jaji Mkuu amewaambia Mahakimu hao kuwa endapo watakutana na kikwazo
cha Sheria, au Kanuni katika kutekeleza agizo hilo wasisiste kumpelekea
mapendezo yao.
Jaji
Mkuu amefikia uamuzi huo kutokana na Maboresho ya Huduma za Mahakama
yanayoendelea pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa
Mahakama ya Tanzania (2015/16 hadi 2019/20).
Alisema
ni haki ya kila Mwananchi aliyekuwa na kesi mahakamani kupatiwa nakala ya
hukumu yake ndani ya siku 21 tangu kusomwa kwa hukumu hiyo au mapema
iwezekanavyo mara baada ya kesi yake kutolewa hukumu. Nakala ya hukumu imekuwa
ikilipiwa kiasi cha shilingi elfu kumi (10,000) kama gharama ya uandaaji wa
nakala hiyo.
Akizungumzia
maboresho ya huduma za mahakama, Prof. Juma alisema Mahakama inao mpango wa
kuanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ili kutatua changamoto ya
upungufu wa Mahakama kwenye baadhi ya Maeneo nchini ikiwemo mikoa ya Tabora na
Kigoma. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Zaidi ya watanzania milioni 25 wako mbali
na huduma za Mahakama.
Alisema
wananchi wa Wilaya ya Kasulu hulazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 376
kufuata huduma za Mahakama Kuu katika mji wa Tabora na kuongeza kuwa hivi sasa
Mahakama imeshaanza ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Kigoma unaotarajiwa
kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu. Aliongeza kuwa Mpango Mkakati wa Miaka
mitano wa Mahakama ya Tanzania unaainisha namna ya kutatua changamoto mbalimbali
za Mahakama ikiwemo ya umbali wa Mahakama na wananchi.
Akizungumza
na watumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu aliwataka watumishi hao kuzingatia maadili
ya kazi na Mahakamas zisiwe sehemu ya rushwa ili kujenga taswira nzuri ya Mhimili
huo kwa wananchi.
Alisema
Mahakama haina budi kushirikiana na wadau na ushirikiano huo uwe ni ule
usioingilia mamlaka ya mwenzake bali kila mhimili usimamie mipaka yake.
“Heshima
ya Mahakama itaongezeka tu kama watumishi watakuwa na maadili mema ikiwa ni
pamoja na kauli nzuri kwa wananchi wanaofika Mahakamani kutafuta haki zao”,alisema
Jaji Mkuu.
Awali,
Mkuu wa wilaya ya Uvinza, Mwamvua Mrindoko alimweleza Jaji Mkuu changamoto
zinazoikabili wilaya yake kuwa ni pamoja na kuwepo kwa makossa makubwa ya
kiuhalifu kutokana na madhara ya wakimbizi yakiwemo mauaji, ungang’anyi wa
kutumia silaha, pamoja na ubakaji.
Alizitaja
changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa gereza katika wilaya yake na kuiomba
Mahakama ya Tanzania kujenga jengo lake la Mahakama ya wilaya ili kurahisisha
suala zima la upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Jaji
Mkuu anaendelea na ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama katika kanda ya Tabora
ambapo leo ametembelea Mahakama za Wilaya za Kasulu na Uvinza .
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni