Na
Lydia Churi-Mahakama, Kigoma
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri Serikali kuishirikisha Mahakama ya
Tanzania kwenye mipango yake ya uanzishaji wa maeneo mapya ya kiutawala ikiwemo Mikoa na wilaya ili
kupunguza changamoto za upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa
ziara yake mjini Kigoma, Jaji Mkuu amesema mipango ya Serikali ya uanzishwaji
wa wilaya au mikoa izingatie pia uanzishwaji wa Mahakama. Aliongeza kuwa Mikoa
na wilaya mpya ndizo zenye ukosefu wa Mahakama hali inayowafanya wananchi kufuata
mbali huduma za kimahakama.
Alisema Mahakama kupitia
Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16
hadi 2019/20) imejipanga kutatua tatizo la ukosefu wa huduma za Mahakama
pamoja na kusogeza huduma hizo karibu Zaidi na wananchi. Kwa kushirikiana na Benki
ya Dunia, tayari imeanza ujenzi wa Mahakama tano za Hakimu Mkazi katika mikoa
ya Simiyu, Katavi, Geita, Njombe na Manyara pamoja na ujenzi wa Mahakama 16 za
wilaya na Mahakama Kuu mbili katika Mikoa ya Kigoma na Mara.
Jaji Prof. Juma amesema
kupitia ziara yake ya siku saba kwenye Mahakama Kuu kanda ya Tabora amebaini
kuwa watanzania wengi hufuata mbali huduma za Mahakama na maeneo mengine ni
kutokana na jiografia ya maeneo hayo. Akitolea mfano wa wilaya ya Uyui mkoani
Tabora, Jaji Mkuu amesema kutokana na wilaya hiyo kuzunguka mkoa, wananchi wake
hulazimika kufuata huduma za Mahakama Kuu zilizopo umbali wa Zaidi ya kilometa
377.
Alisema Mahakama
itaanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) kwenye maeneo yote yenye
changamoto kama hizo kabla ya kujenga Mahakama kwa kuwa changamoto ya
upatikanaji wa huduma za kimahakama bado ni kubwa nchini.
Kuhusu utendaji kazi,
Jaji Mkuu aliwapongeza watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Tabora kwa kubuni mkakati
wa kupunguza mlundikano wa kesi kwenye Mahakama zake. Kanda ya Tabora ndiyo
kanda pekee nchini iliyopunguza siku za mpango wa upimaji wa kumaliza mashauri Mahakamani
kutoka miaka miwili mpaka moja kwa kesi za Mahakama Kuu, miezi sita badala ya
12 kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na wilaya na kutoka miezi 6 mpaka 3 kwa kwa
Mahakama za Mwanzo.
Katika kipindi cha mwezi
Januari hadi Disemba 2017, kanda ya Tabora ilisajili jumla ya mashauri 1112 na
mashauri yaliyosikilizwa na kumalizika yalikuwa 1194 wakati mashauri yaliyobaki
Desemba 2016 yalikuwa ni 541.
Aidha Kanda ya Tabora
imemaliza mashauri ya mlundikano kwa kiasi kikubwa hivyuo kufanya mashauri hayo
kwisha kabisa katika Mahakama za Mwanzo na kupungua kwa kiasi kikubwa katika
Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya. Mashauri ya mlundikano yaliyobaki
Mahakama Kuu hadi kufikia Desemba 31 yalikuwa 4.
Kati ya mashauri hayo, mashauri
yenye umri kati ya miezi 25-48 Mahakamani yalibaki 3 na shauri moja (1) lenye
umri wa miaka 5-10 lilibakia. Aidha, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora haina
mashauri yenye umri wa Zaidi ya miaka 10.
Jaji Mkuu amemaliza ziara
yake ya siku saba katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora ambapo
alikagua shughuli mbalimbali za Mahakama pamoja na kuwatembelea baadhi ya wadau
wa Mahakama wakiwemo wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kujadiliana na viongozi hao
namna ya kupunguza changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania pamoja na
kuimarisha ushirikiano na wadau hao.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wakandarasi wa Kampuni ya Masasi Construction Ltd wanaojenga jengo la Mahakama Kuu ya Kanda ya Kigoma kwenye eneo la ujenzi wa Mahakama hiyo. Wa tatu Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Solanus Nyimbi.
Jengo la Mahakama Kuu ya Kanda ya Kigoma kama linavyoonekana likiwa limefikia hatua hiyo. Jengo hili linatarajiwa kukamilika Aprili, 2019.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wakandarasi wa Kampuni ya Masasi Construction Ltd wanaojenga jengo la Mahakama Kuu ya Kanda ya Kigoma kwenye eneo la ujenzi wa Mahakama hiyo. Wa tatu Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Solanus Nyimbi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni