Na
Lydia Churi-Geita
Katika
kutekeleza dhamira yake ya kuboresha huduma za Mahakama na kusogeza huduma hizo
karibu zaidi na wananchi, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia
imeanza rasmi ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama katika mkoa wa Geita pamoja
na wilaya zake za Bukombe na Chato.
Ujenzi
wa Mahakama hizi ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 hadi
2019/2020) wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za
Mahakama ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 2015. Miradi hii kwa pamoja
inalenga kuboresha huduma na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Mahakama
imeanza ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mkoa wa Geita ambalo litajumuisha pia na
Mahakama ya wilaya ya Geita. Majengo mengine yanayojengwa ni ya Mahakama za
wilaya za Bukombe na Chato.
Majengo
haya yanatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita kutoka sasa na
yanajengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na gharama nafuu na ya muda mfupi
iitwayo Moladi ambapo kampuni ya Moladi Tanzania ndiyo imepewa dhamana ya
kujenga majengo hayo. Jumla ya majengo ya Mahakama za Mkoa, wilaya na Mwanzo
sita tayari yameshajengwa kwa kutumia teknolojia ya Moladi katika jiji la Dar
es salaam na Mkoa wa Pwani.
Majengo
haya ni yale ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani na Mahakama ya Wilaya ya
Kibaha, Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Kigamboni, Mkuranga pamoja na jengo la
Mahakama ya wilaya ya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kigamboni na Mahakama ya
Mwanzo Kawe jijini Dar es salaam.
Mhandisi
wa Kampuni ya Moladi Tanzania anayesimamia ujenzi wa Mahakama za Geita, Bukombe
na Chato, Camilius Mihambo akielezea ujenzi wa Mahakama hizo alisema ujenzi huo
unaendelea vizuri na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi
sita kilichopangwa . Mhandisi Mihambo amesema hatua ya ujenzi iliyofikiwa sasa
ni hatua ya awali ya kujenga msingi katika majengo yote matatu.
“Kazi
kubwa na inayochukua muda mrefu kwa sasa ni ya kujenga msingi, hatua inayofuata
ya kuweka ukuta ni ya muda mfupi kwa kuwa tunatumia teknolojia ya Moladi ambayo
kuta zinaweza kusimama ndani ya siku tatu na kuendelea, alisema Mhandisi huyo.
Akizungumzia
hatua ya Mahakama ya Tanzania kuanza ujenzi katika Mkoa wa Geita, Mtendaji wa
Mahakama ya Mkoa wa Geita, Lothan Simkoko anaelezea kufurahishwa kwake kwa
uamuzi wa Mahakama kujenga Majengo ya Mahakama za wilaya na Mkoa katika mkoa wa
Geita. Anasema ujenzi huo utasaidia upatikanaji wa haki kwa wakati kwa wananchi
wanaofika Mahakamani kutafuta haki zao pia kumaliza changamoto ya ufinyu wa ofisi.
Alisema, jengo la Mahakama ya Mkoa litakapomalizika litatoa nafasi zaidi na
kuboresha huduma. Mahakama ya Mkoa wa Geita ina upungufu wa chumba cha
Mahabusu, chumba cha kuhifadhi ushahidi pamoja na ofisi kwa ajili ya watumishi
wake.
Mtendaji
huyo alisema Mahakama Mkoani Geita haina jengo la Mahakama ya wilaya na badala
yake jengo linalotumika sasa kwa Mahakama ya wilaya na Mwanzo ni la kuazima na
pia haliko katika hali nzuri. Alisema kukamilika kwa jingo jipya la Mahakama
mkoani humo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za Mahakama.
Hata
hivyo, baadhi ya wananchi waliohojiwa juu ya ujenzi wa Mahakama hizo
walionyesha kufurahishwa na hatua hiyo ya Mahakama kujenga majengo yake mapya.
Bwana Mika Jonathan Shija ambaye ni Mkazi wa Geita anaelezea kufurahishwa kwake
na ujenzi wa Mahakama ya Mkoa na ya Wilaya ya Geita na kusema kuwa ujenzi huo
utakapokamilika utawarahisishia wananchi kupata huduma. “kama tulivyoambiwa
kuwa Mahakama ya Mkoa na wilaya zitakuwa kwenye jengo moja hivyo kwetu sisi ni
rahisi kwa kuwa itakuwa ni rahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine”, alisema.
Naye
Pili Malongo Mkazi wa Bukombe yeye alisema amefurahishwa na ujenzi wa Mahakama wilayani
humo kwa kuwa anaamini jengo jipya la Mahakama litakuwa na sehemu iliyotengwa
kwa ajili ya wananchi kupumzika wakati wakisubiri kupatiwa huduma mahakamani
hapo.
Pamoja
na ujenzi wa Mahakama hizo tatu katika Mkoa wa Geita, Mahakama ya Tanzania tayari
imeanza kutekeleza program ya ujenzi wa majengo 18 ya Mahakama katika mwaka huu
wa fedha wa 2017/2018 anabainisha Mkuu wa Kitengo cha Majengo (Estate
Management) wa Mahakama ya Tanzania Mhandisi Khamadu Kitunzi.
Kwa
mujibu wa Mhandisi Kitunzi, kati ya majengo 18 yaliyoanza kujengwa nchini, majengo mawili ni ya Mahakama Kuu
yanayojengwa kwenye Mikoa ya Mara na Kigoma, matano ni ya Mahakama za Hakimu
Mkazi yanayojengwa katika mikoa ya Geita, Njombe, Lindi, Simiyu, na Katavi.
Aidha jumla ya majengo 11 ya Mahakama za Wilaya yanajengwa katika wilaya za
Kasulu, Rungwe, Ruangwa, Kilwa Masoko, Kilindi, Sikonge, Kondoa, Bunda na
Longido.
Aidha,
Mahakama pia imefanikiwa kujenga Mahakama za Mwanzo na pia kumalizia baadhi ya
Mahakama zilizoanza kujengwa kwa nguvu ya wananchi katika maeneo mbalimbali
nchini kama vile Itinje-Meatu, Robanda-Serengeti, Wasso-Loliondo, na Karatu
Arusha. Maeneo mengine ni Beleko-Kondoa, Mahakama ya Old Korogwe-Korogwe,
Mvomero Morogoro, Mahakama ya Mwanzo Totoe iliyopo Mkoani Songwe na Mahakama ya
Mwanzo Iguguno mkoani Singida.
Akifafanua
zaidi kuhusu ujenzi wa majengo ya Mahakama, Mhandisi Kitunzi anaeleza kuwa hivi
sasa zipo Mahakama Kuu 14 na baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama kuu katika
mikoa ya Mara na Kigoma kutakuwa na jumla ya Mahakama kuu 16 nchini na kubaki
na uhitaji wa Mahakama Kuu 10 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. Mahakama
ya Tanzania inalenga kujenga majengo ya Mahakama kuu ambayo yatatumika kama
Kituo Jumuishi cha kutoa huduma za kimahakama yaani Intergrated Justice Centre. Mahakama tayari ilifanya ukarabati mkubwa
wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya ambapo hivi sasa Mahakama hiyo inafanya
kazi kama kituo Jumuishi cha huduma za Kimahakama.
Mhandishi
Kitunzi anasema Mahakama inao mpango wa kujenga Majengo ya Mahakama Kuu ambayo
yatatoa huduma kama kituo Jumuishi cha kutoa Huduma za Kimahakama kwa
kushirikiana na Benki ya Dunia katika mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Dodoma,
Singida, Mwanza na Arusha.
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita na Mahakama ya Wilaya ya Geita likiwa katika hatua za awali za ujenzi. Jengo hili linajengwa kwa kutumia Teknolojia ya gharama nafuu na inayotumia muda mfupi iitwayo Moladi na Kampuni ya Moladi Tanzania . Ujenzi unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita.
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita na Mahakama ya Wilaya ya Geita likiwa katika hatua za awali za ujenzi.
Hapa ndipo ilipo Mahakama ya wilaya ya Bukombe. Jengo hili si mali ya Mahakama ya Tanzania. Hivi sasa Mahakama tayari imeanza ujenzi wa jengo lake la Mahakama ya wilaya ya Bukombe.
Ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe linalojengwa katika mji mdogo wa Ushirombo wilayani Bukombe kama inavyoonekana pichani ukiwa katika hatua ya uchimbaji wa Msingi. Jengo hili litajengwa kwa kutumia Teknolojia ya gharama nafuu na inayotumia muda mfupi iitwayo Moladi. Ujenzi unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita.
Hili ni jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato kama linavyoonekana pichani. Mahakama imeanza ujenzi wa Jengo jipya wilayani humo kwa ajili ya Mahakama hiyo.
Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato kama linavyoonekana kwenye picha likiwa tayari limeanza kujengwa ili kuboresha zaidi huduma za Mahakama wilayani humo. Jengo hili linajengwa kwa kutumia Teknolojia ya gharama nafuu na inayotumia muda mfupi na Kampuni ya Moladi Tanzania . Ujenzi unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita.
Sehemu ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato lililoanza kujengwa hivi karibuni.
Sehemu ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato lililoanza kujengwa hivi karibuni.
Sehemu ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato lililoanza kujengwa hivi karibuni.
Mhandisi anayesimamia ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama za Geita, Bukombe na Chato wa kampuni ya Moladi Tanzania, Camilius Mihambo akiwa kwenye eneo la ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Chato. Mhandisi Mihambo anasema anatarajia kazi ya ujenzi wa Majengo yote matatu itakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita endapo hakutakuwa na changamoto yoyote itakayo jitokeza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni