Na
Lydia Churi-Mahakama ya Tanzania
Viongozi wanaohusika na Oparesheni
za kuzuia uhalifu wameshauriwa kufuata na kuzingatia sheria inayoongoza namna
ya ukusanyaji wa ushahidi ili kuepuka kuharibu ushahidi kabla haujawasilishwa
Mahakamani na kupelekea kesi nyingi kuharibika kwa kukosa ushahidi au Mahakama
kushindwa kutoa hukumu zinazoendana na kosa husika.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameyasema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Uyui alipomtembelea Mkuu wa wilaya
hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake inayoendelea Mahakama Kuu kanda ya Tabora.
Akitolea mfano wa Oparesheni
za uteketezaji wa dawa za kulevya yakiwemo mashamba ya bangi, Jaji Mkuu amesema
ushahidi kuteketezwa bila ya kufuata utaratibu huathiri mienendo ya kesi
Mahakamani.
Akizungumzia suala la
Maadili ndani ya Mahakama, Jaji Mkuu amewaomba Wakuu wa mikoa pamoja na Wakuu
wa wilaya ambao anawatambua kama walezi wa Mahakama kushirikiana kwa karibu
zaidi na Mahakama ili kuhakikisha wanawahudumia wananchi ipasavyo katika suala
zima la utoaji wa Haki.
Kuhusu kusogeza huduma za
kimahakama karibu Zaidi na wananchi, Jaji Mkuu amesema Mahakama kwa
kushirikiana na Benki ya Dunia inao Mpango wa kuanzisha Mahakama zinazotembea
(Mobile Courts) ili kuwafikia wananchi walio mbali na huduma za kimahakama hasa
katika wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Naye Mkuu wa wilaya ya
Tabora na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Uyui, Queen Mlozi alimweleza
Jaji Mkuu kuwa kwa namna wilaya ya Uyui ilivyokaa kijiografia, wananchi
hulazimika kufuata huduma za kimahakama umbali wa Zaidi ya kilometa 150 katoka Loya
kwenda Kigwa mkoani Tabora.
Awali akiwa wilaya ya
Urambo, Jaji Mkuu alipata wasaa wa kuzungumza na Mkuu wa wilaya hiyo, Angelina
Kwingwa ambaye alimshukuru Jaji Mkuu kwa mkakati wa Mahakama wa kukarabati na
kujenga majengo ya mahakama maeneo mbalimbali nchini ambayo yatasaidia
kupunguza mashauri mahakamani.
“Tumepata faraja kusikia suala
la kuongezeka kwa majengo ambayo yatasaidia kupunguza mlundikano wa kesi
Mahakamani na upatikanaji wa haki kwa wakati”, alisema.
Jaji Mkuu anaendelea na ziara
Mahakama kuu kanda ya Tabora inayojumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma. Leo alitembelea na kukagua shughuli za Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo Ilolangulu, Mahakama ya wilaya ya Urambo na Mahakama ya Mwanzo Upuge-Uyui zilizopo mkoani Tabora.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Urambo mara baada ya kuwasili.
Afisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania, Anatory Kagaruki akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali kwa watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Urambo akiwa katika ziara ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma inayoendelea katika kanda ya Tabora.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Urambo wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania alipozungumza nao.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Urambo Mhe. Hassan Momba akimuelezea jambo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tabora Mhe. Sam Rumanyika pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Urambo Mhe. Hassan Momba (kushoto).
Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa akizungumza wakati alipotembelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania ofisini kwake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora akizungumza.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza alipomtembelea Mkuu wa wilaya ya Urambo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika kanda ya Tabora.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi machapisho mbalimbali ya Mahakama ya Tanzania Mkuu wa wilaya ya Urambo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali ambao pia ni wajumbe wa kamati ya Ulionzi na Usalama ya wilaya ya Urambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni