Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mahakama ya Tanzania
kwa kuanza kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika suala
zima la utoaji wa haki nchini.
Akizungumza kwenye
kilele cha wiki ya Sheria na siku ya Sheria Nchini, Rais Magufuli amesema Tehama
inayo nafasi kubwa katika kurahisisha mfumo
wa utendaji kazi na utoaji wa haki na kuahidi kuusadia Mhimili huo katika vifaa
vya Tehama.
Mhe. Rais alisema kwa
Mahakama kutumia Tehama katika kazi zake, itasaidia kuongeza kazi ya utendaji
pamoja na kupunguza tatizo la rushwa ambalo limekuwa ni kubwa katika Taasisi nyingi
za serikali.
Aidha, Kufuatia Tume ya
Utumishi wa Mahakama kuwafukuza kazi zaidi ya watumishi 112 wa Mahakama kutokana na makosa mbalimbali
ya ukosefu wa maadili na uwajibikaji, Rais amempongeza Mhe. Jaji Mkuu wa
Tanzania na kuzitaka Taasisi nyingine kuiga mfano wake.
“ Naipongeza Tume ya
Utumishi wa Mahakama ambayo wewe ni Mwenyekiti wake kwa kuwafukuza kazi
watumishi 112 wakiwemo Mahakimu 27, asante sana na sijutii kukuteua kuwa Jaji
Mkuu, alisema Mhe. Rais.
Alisema Mahakama
inafanya kazi zake vizuri lakini bado wapo watumishi wachache wanaokiuka
maadili na hawa hatupaswi kuwaacha maana
wanachelewesha utoaji wa haki kwa wakati.Amevitaka vyombo husika kupanga
mkakati wa kutatua tatizo hili.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amevitaka vyombo vyote vya dola kutoa kipaumbele katika Sheria kwa kuwa
sheria ni msingi wa amani na amani ni maendeleo.
Alisema kwa kulitambua
hilo, Mahakama ya Tanzania katika wiki ya sheria imetoa elimu ya sheria na taratibu za sheria
kwa wananchi mbalimbali na imejiwekea
malengo ya kuongeza uwazi na ufanisi katika masuala utawala na uendeshaji wa
mashauri na Tehama ndio jibu sahihi la karne ya 21.
Jaji Mkuu alisema
Mahakama imedhamiria kuondokana na tatizo la rushwa na imeazimia na haitaki
kubaki nyuma na kasi ya mabadiliko ya kunufaika na manufaa makubwa ya Tehama.
Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania imelenga kunufaika na
Tehama kwenye eneo la usimamizi wa
fedha, ukusanyaji wa takwimu, ukusanyaji wa mapatona usikilizaji wa mashauri.
Siku ya Sheria nchini huadhimishwa
kila mwaka na ilianza kuadhimishwa nchini
mwaka 1996.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Chimala jijini Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Chimala jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wastaafu kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Chimala jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Dini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni