Na
Mary Gwera
Katika mwendelezo wa
Utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) (2015/2016-2019/2020), Mahakama
ya Tanzania inaendelea na jitihada za kupata uzoefu na ujuzi kutoka katika
Mahakama mbalimbali duniani zilizopiga hatua katika maboresho ya huduma ya
utoaji haki kwa wananchi.
Haya yamejidhihirisha
kufuatia ugeni wa Maafisa wa Mahakama waliowasili kutoka nchini Guatemala kwa mualiko
wa Mahakama ya Tanzania kushiriki katika Hafla ya Siku ya Sheria nchini, iliyofanyika
Februari 01, 2018 na vilevile kupata maoni na ushauri zaidi wa
jinsi ya kuendelea kuiboresha Mahakama nchini kwa manufaa ya wananchi ambao
ndio walengwa Wakuu.
Akiwatambulisha wageni
hao kwa Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Februari 1 katika Ofisi ya Mhe. Jaji Mkuu, Mahakama
ya Rufani jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein
Kattanga alisema kuwa takribani mwaka mmoja sasa baadhi ya Maafisa wa Mahakama
nchini walifanya ziara nchini Guatemala kwa lengo la kujifunza ni kwa namna
gani Mahakama nchini humo imefanikiwa katika utoaji wa huduma zake.
“Mhe. Jaji Mkuu,
tulichojifunza na tukaona ni vyema kuiga kutoka Guatemala ni pamoja na huduma
ya Mahakama inayotembea ‘mobile court’, ufanyaji kazi wa Mahakama kwa masaa 24,
kuweka mbele matumizi ya teknolojia katika shughuli zake n.k, hivyo tumeona ni vyema pia kwa Mahakama nchini
kupata utaalamu/uzoefu kutoka kwa wenzetu jinsi ya kuweza kutekeleza haya,”
alisema Bw. Kattanga.
Mahakama ya Tanzania
imeonyesha nia ya dhati katika suala zima la maboresho, hivyo basi ujio wa
Wageni hawa ambao watakuwepo nchini kwa takribani siku 5, utawezesha Wataalamu
wa Mahakama kupata uzoefu na ujuzi zaidi wa namna gani Mahakama zinazotembea
zinavyofanya kazi n.k.
Aidha; kwa upande wake,
Jaji Mkuu aliyemaliza muda wake wa Mahakama nchini Guatemala, Mhe. Osvaldo
Mendez alisema kuwa Mahakama nchini humo amepiga hatua kubwa katika suala zima
la Matumizi ya TEHAMA hali ambayo imesaidia kurahisisha utendaji na kutoa haki
kwa wakati.
“Mahakama yetu pia
inafanya kazi masaa 24, na tunatoa huduma hii katika Miji mikubwa mitano nchini
Guatemala na tunafanya kwa ushirikiano na Wadau wetu wa Mahakama kama Waendesha
Mashitaka ‘Prosecutors’ n.k ili kufanikisha kumaliza mashauri hayo kwa muda
muafaka,” alieleza Mhe. Mendez.
Mpango Mkakati unaotekelezwa
na Mahakama umegawanyika katika nguzo
kuu tatu ambazo ni Utawala na Menejimenti bora ya Rasilimali, Upatikanaji na
utoaji wa Haki kwa wakati na kuimarisha imani ya Jamii na Ushirikishaji wa
wadau katika shughuli za Mahakama; nguzo zote zikilenga katika uboreshaji wa
huduma za Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele) akiwa pamoja na baadhi ya Wahe.
Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu na Ugeni kutoka
Mahakama nchini Guatemala pindi Wageni hao walipomtembelea Mhe. Jaji Mkuu
ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Jaji
Mkuu wa Tanzania (pichani) akiwa katika mazungumzo na Wageni hao (hawapo
pichani), katika mazungumzo yao Mhe. Jaji Mkuu amefurahishwa na hatua
iliyofikiwa na Mahakama nchini Guatemala.
Baadhi
ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwa katika kikao hicho, wa kwanza kushoto ni Mhe. Jaji Sauda Mjasiri, katikati ni Mhe. Jaji Mussa Kipenka na kulia ni Mhe. Jaji Stella Mugasha.
Jaji
Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akiongea jambo na
Wageni hao, Mhe. Wambali aliwaelezea Wageni hao juu ya Mfumo wa Mahakama
nchini.
Jaji Mkuu aliyemaliza
muda wake wa Mahakama nchini Guatemala, Mhe. Osvaldo Mendez akizungumza jambo.
Mtendaji
Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga akizungumza jambo katika
kikao hicho.
Mtaalamu
kutoka Benki ya Dunia, Bw. Waleed Malik akiongea jambo katika kikao hicho.
Picha ya pamoja baada
ya mazungumzo: Walioketi (katikati) ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Juma, wa pili kulia ni Mhe. Sauda Mjasiri,Jaji wa Mahakama ya Rufani, wa kwanza kulia ni Mhe. Mussa Kipenka, Jaji wa Mahakama ya Rufani (T) wa pili kushoto ni Jaji Mkuu aliyemaliza
muda wake wa Mahakama nchini Guatemala, Mhe. Osvaldo Mende, wa kwanza kushoto ni Mhe. Napoleon Porfirio Guix Zarate, Naibu Meneja Mkuu wa Tawi la Mahakama-Guatemala wakiwa pamoja na Viongozi pamoja na Wahe. Majaji wa Mahakama walioshiriki katika mazungumzo na ugeni huo.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni