Na
Mary Gwera
Jumla ya Majaji 32 wa
Mahakama Kuu ya Tanzania wanaendelea kupatiwa Mafunzo jijini Arusha lengo
likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji haki nchini.
Katika mahojiano maalum
na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyika Machi 26, 2018
katika Ukumbi wa Mikutano wa AICC jijini Arusha, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo amesema
kuwa Majaji hao wanaoshiriki katika Mafunzo hayo ni wa awamu ya pili.
“Mafunzo haya ya siku
tano (5) yaliyoanza Machi 24 na kumalizika Machi 28, 2018 yamejikita katika
maeneo mawili ambayo ni ‘Namna ya uendeshaji wa Mashauri ya Kikatiba’ na ‘Matumizi
ya TEHAMA katika kutoa haki,” alisema Mhe. Kihwelo.
Mhe. Jaji Kihwelo
alisema kwa kuwa moja ya Vipaumbele vya Mahakama katika Mpango Mkakati wake ni
pamoja na Matumizi ya TEHAMA, hivyo wameona ni vyema kutoa mafunzo kwa awamu ka
Waheshimiwa Majaji na Watumishi wengine ili kujua matumizi ya TEHAMA na
changamoto zake.
Mkuu huyo wa Chuo
amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Waheshimiwa Majaji juu ya
maeneo hayo na vilevile kujenga taswira chanya ya Mahakama.
“Katika mafunzo haya,
Waheshimiwa Majaji wamepewa ufafanuzi juu ya Sera ya TEHAMA ya Taifa pamoja na
mifumo ili wanapotumia Vifaa vya TEHAMA pamoja na mifumo yake
iliyopo Mahakamani wazingatie taratibu na miongozo kama zilivyoainishwa katika
Sera hiyo,” alifafanua Mhe. Jaji Kihwelo.
Mhe. Kihwelo aliendelea
kusema kuwa baada ya Mafunzo hayo kukamilika wanatarajia kuwa na uelewa wa
pamoja ili kurahisisha utekelezaji wa lengo la Mahakama ya kuwa Mahakama
mtandao ‘e-Judiciary’.
Aidha Mhe. Jaji Kihwelo
aliongeza kuwa wanatarajia Weledi wa Majaji kuongezeka juu ya namna bora zaidi
ya uendeshaji wa Mashauri ya Kikatiba.
“Mashauri ya Kikatiba
ni Mashauri ambayo hupelekwa Mahakamani kupinga ukiukwaji wa Katiba au kudai
haki ya Kikatiba,” alifafanua Mhe. Kihwelo.
Mhe. Jaji Kihwelo
anafafanua zaidi kuwa Mashauri ya Kikatiba ni mashauri ambayo hufunguliwa
Masjala Kuu ya Mahakama Kuu inapokaa kama Mahakama ya Kikatiba na huendeshwa na
Majaji watatu.
Mafunzo haya ya
Waheshimiwa Majaji yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa fedha
za Mradi wa Benki ya Dunia na kuratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu-Kanda ya Mtwara, Mhe. Jaji Fauz Twaib (kushoto) akifurahia jambo
na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo.
Baadhi ya Waheshimiwa
Majaji wa Mahakama Kuu wanaoshiriki katika Mafunzo wakiwa katika kazi ya
kikundi ‘group work’, Mafunzo hayo yanafanyika AICC mkoani Arusha.
Majadiliano
yakiendelea.
Waheshimiwa Majaji
wakiendelea kujadiliana.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni