MAHAKIMU wapya
wanaotarajia kuanza kazi rasmi ndani ya Mhimili wa Mahakama wametakiwa kufanya
kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za Mhimili huo.
Akizungumza na baadhi
ya Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo walioajiriwa hivi karibuni katika
Ukumbi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam mapema Machi 20, Jaji Kiongozi- Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali amewaasa Waajiriwa hao kufanya kazi kwa
maadili na kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
“Katika ufanyaji kazi
wenu wa Uhakimu, mnatakiwa kuzingatia mambo makuu manne ya msingi ni; Ujuzi wa
taratibu na mazoea ya Kimahakama, Uelewa kuhusu Sheria za Msingi ‘Substantive law’ na Sheria za Mwenendo ‘Procedural Law’ kuangalia mazingira ya
utoaji haki na kadhalika,” alieleza Mhe. Wambali.
Aidha Jaji Kiongozi pia
aliwataka Mahakimu hao pia kufanya kazi kwa kuwaheshimu Wadau wote wanaojumuika
nao katika mchakato mzima wa utoaji wa haki, ikiwa ni pamoja na Makarani, Wazee
na Baraza na wengineo.
“Heshimuni kila mtu
mnayeingia naye Mahakamani, kila mtu ana mchango katika upatikanaji wa haki, na
moja ya sifa ya Hakimu ni upole lakini upole sio udhaifu,” alisisitiza Mhe. Jaji
Wambali.
Mbali na kuwaasa
kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, Mhe. Jaji Kiongozi aliwaasa pia Mahakimu
hao kutojihusisha na masuala ya siasa katika kazi zao.
“Ibara ya 113A ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema, Hakuna Jaji au Hakimu
anayeruhusiwa kuwa Mwanachama wa Chama chochote cha Siasa” alisisitiza Mhe.
Jaji Kiongozi.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania, Bw. Edward
Nkembo amesema kuwa jumla ya Mahakimu wapya 78 kati ya 100 wameripoti kazini.
“Jumla ya Mahakama
wapya 78 wa Mahakama za Mwanzo wameripoti, hata hivyo baadhi wametoa taarifa ya
kushindwa kuripoti Machi 20,2018 kutokana na dharura mbalimbali,” alisema Mkurugenzi huyo.
Bw. Nkembo ameeleza kuwa
baadhi ya Mahakimu watakaoshindwa kuripoti ndani ya siku
14 tangu Machi 20, nafasi zao zitatafutiwa watu wengine watakaoomba na kukidhi
vigezo.
Mahakimu hao na
Watumishi wa Kada zingine walioajiriwa na Mahakama hivi karibuni watasambazwa katika Mahakama
mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuongeza nguvu kazi katika kuendelea
kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Jaji Kiongozi-Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali (wa pili kulia) akiongea na jumla ya Mahakimu
wapya 78 wa Mahakama za Mwanzo (hawapo pichani) walioripoti katika Ofisi za
Mahakama Kuu- Kanda ya Dar es Salaam, wa pili kushoto ni Msajili-Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Ilvin Mugeta, wa kwanza kushoto ni Bw. Edward Nkembo,
Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania na wa kwanza kulia ni
Mtendaji-Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.
Baadhi ya Mahakimu
wapya wakimsikiliza Mhe. Jaji Kiongozi.
Wakiendelea kumsikiliza
Mhe. Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi-Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali (Katikati), Bw. Edward Nkembo,
Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania (aliyeketi kushoto) na Mtendaji-Mahakama
Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na
baadhi ya Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo walioajiriwa hivi karibuni.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni