Na Mary Gwera, Mahakama
Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya
Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Nicola Smithers ameipongeza Mahakama
kwa utekelezaji wake wa Mradi wa Maboresho wa huduma za Kimahakama.
Bi. Smithers aliyasema hayo mapema Machi 19,
alipokutana na Mhe. Jaji Mkuu ofisini kwake Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam
ambapo alipata nafasi ya kuongea na Mhe. Jaji Mkuu na Viongozi wengine wa
Mahakama akiwemo Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
“Nimefurahishwa na maendeleo ya utekelezaji
wa Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia,
hususani katika eneo la uondoshaji wa mlundikano wa mashauri,” alisema Bi.
Smithers.
Akimkaribisha ofisini kwake, Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Profesa Ibrahimu Juma alimueleza Bi. Smithers juu ya maboresho mbalimbali
yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania yote yakiwalenga wananchi
ambao ndio wateja wa Mahakama.
“Miongoni mwa maeneo ambayo tunayoendelea kupambana
nayo ili kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama ni pamoja na Rushwa, katika
hili tmefanya jitihada kadhaa ikiwa ni pamoja na kusambaza mabango ‘posters’ yenye
ujumbe wa kupinga rushwa na kuyasambaza katika ofisi za Mahakama kote nchini
pamoja na kusambaza simu za kuwawezesha wananchi wenye malalamiko kutuma meseji
ili malalamiko yao yaweze kufanyiwa kazi,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia pia juu ya
uamuzi wa utoaji wa nakala za hukumu bure kwa wananchi wenye kesi ili
kuwarahisishia wananchi wenye kipato cha chini kupata haki zao pia.
Mhe. Jaji Mkuu aliongelea pia juu ya huduma ya
Mahakama za Mwanzo, huku akisema kuwa wananchi wengi wanahitaji huduma za
Mahakama za Mwanzo, hivyo kuna haja ya kusogeza huduma hii karibu zaidi na
wananchi.
“Mfano hivi karibuni nilifanya ziara Mkoani Tabora,
miongoni mwa maeneo ambayo yapo mbali kufikika kutokana na Jiografia yaki ni pamoja
na Wilaya ya Uyui, hivyo basi maeneo kama haya yanatakiwa kuwa na huduma ya
Mahakama inayotembea ‘Mobile Court’,” alisema Mhe. Jaji Mkuu huku akiongeza juu
ya umuhimu wa Mahakama kushirikiana kwa karibu na Mabaraza ya Kata katika
ufanyaji kazi wake.
Miongoni mwa maeneo ambayo Viongozi wa Mahakama i.e
Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama walizungumzia katika mazungumzo kati
ya Meneja huyo kutoka Benki ya Dunia na Mhe. Jaji Mkuu, ni pamoja na ufanyaji
kazi wa Mahakama wenye kuzingatia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5),
ushirikiano kati ya Wada.
Bi. Smithers ambaye amewasili nchini kutokea
Washington D.C zilipo ofisi cha Benki ya Dunia amefanya ziara yake Mahakama kwa lengo la kuangalia maendeleo ya
utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ambao unatekelezwa kwa
ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB).
Maeneo muhimu yanaotekelezwa na Mradi wa Benki ya
Dunia (WB) ni pamoja na; Mapambano dhidi ya Rushwa; ni kwa jinsi gani Mahakama
pamoja na wadau wengine wanaweza kushirikiana katika kupiga vita vitendo vya
rushwa.
Maeneo mengine ni ushirikishaji wa wadau katika
masuala yote ya utoaji haki na kusogeza huduma ya utoaji haki karibu na
wananchi.
Meneja huyo wa Miradi ya Utawala
Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Smithers anatarajia pia kutembelea katika
Ofisi za Maboresho ya Mahakama, Kituo cha Mafunzo-Kisutu pamoja na Mahakama ya
Wilaya Kigamboni.
Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki
wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Nicola Smithers
akisaini Kitabu cha Wageni pindi alipowasili ofisini kwa Mhe. Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahimu Juma akiongea jambo na Mgeni wake Bi. Nicola Smithers ambaye ni Meneja
wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia
(WB).
Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Hussein Kattanga (wa pili kushoto) akichangia jambo katika Mazungumzo
hayo, wa kwanza kushoto ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina
Revokati, wa pili kulia ni Meneja kutoka Benki ya Dunia-Tanzania, Bw. Dennis
Biseko.
Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Katarina Revokati (wa kwanza kushoto) akichangia jambo.
Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki
wa Miradi ya Utawala Bora kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Nicola Smithers
akizungumza jambo.
Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokati akichangia jambo.
Mkuu wa Kitengo cha
Maboresho-Mahakama, Mhe. Zahra Maruma akiwa katika mazungumzo hayo.
Picha ya pamoja. (Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni