Na
Lydia Churi- Mahakama ya Tanzania
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali amewataka Watendaji, Naibu
Wasajili na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi nchini kufanya kazi
kwa kushirikiana ili kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama na kuwapatia
wananchi haki kwa wakati.
Akifunga Mkutano Maalum
wa siku mbili wa Watendaji, Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama za Hakimu
Mkazi jijini Arusha uliojadili namna ya kumaliza mashauri ya Mlundikano
Mahakamani, Jaji Kiongozi amewaambia viongozi hao kuwa wanalo jukumu la
kuhakikisha Mahakama ya Tanzania inatimiza azma yake ya kuboresha huduma zake
kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano pamoja na Mradi wa Maboresho ya
Huduma za Mahakama unaotekelezwa hivi sasa.
“Lazima tushirikiane
kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yetu ili Mahakama ya Tanzania isonge
mbele, tufanye kazi kwa pamoja na kuacha tofauti zetu kwa kuwa kila mmoja ana
umuhimu wake ndani ya Mahakama”, alisema Jaji Kiongozi.
Akizungumzia namna ya
kupunguza mashauri ya muda mrefu kwenye Mahakama mbalimbali nchini, Jaji
Wambali aliwaambia viongozi hao kuwa Mahakama inakusudia kuongeza idadi ya
Majaji kwenye baadhi ya Kanda za Mahakama Kuu nchini zenye idadi kubwa ya
mashauri ya mlundikano.
Jaji Kiongozi aliizitaja
kanda za Mahakama Kuu zenye idadi kubwa ya mashauri ya mlundikano kuwa ni pamoja
na kanda ya Bukoba, Dar es salaam na Njombe.
Wakati
huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bwn. Hussein
Kattanga amewataka Viongozi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kuujenga
Mhimili huo.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama aliwakumbusha viongozi hao dhamira ya Mahakama kwenye maboresho ya utoaji haki kuwa
ni pamoja na kuondokana na tabia ya makusudi ya uzuiaji wa haki ya msingi ya
kukata rufaa kwa kuhakikisha nakala za
hukumu na mwenendo wa mashauri vinapatikana kwa wakati na bila vikwazo.
Alisema Mahakama
imedhamiria kuongeza bajeti ya kanda, Mkoa na wilaya ili kutekeleza Mpango
Mkakati wa Mahakama unaolenga kuongeza na kuboresha Watumishi, majengo, weledi
maslahi, wadau, utawala bora na sheria na kupiga vita vitendo vinavyokiuka
maadili na rushwa.
Kuhusu Mashauri, Bwn. Kattanga
alisema Mahakama imedhamiria kusimamia utekelezaji wa umalizaji wa mashauri ya
mlundikano katika Mahakama za Hakimu Mkazi, wilaya na Mahakama za Mwanzo hadi
kufikia kutokuwa na mashauri ya aina hiyo kila mwaka wa Mahakama unapomalika Desemba
ya kila mwaka.
Alisema Mahakama pia
inayo dhamira ya kuimarisha Menejimenti ya mashauri tangu shauri linaposajiliwa
mpaka linapomalizika pamoja na kusimamia na kusaidia kudhibiti mienendo isiyofaa
ya Mawakili na Madalali wa Mahakama kama maofisa wa Mahakama.
Hivi sasa Mahakama ya
Tanzania inatekeleza Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16-2019/20) pamoja
na Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama ambapo kupitia Mpango Mkakati huo,
Mahakama inasimamia matumizi bora ya rasilimali, upatikanaji wa haki kwa wakati
na kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama.
Jaji kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akifunga Mkutano wa siku mbili wa Naibu Wasajli, Watendaji na Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi uliofanyika jijini Arusha.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bwn. Hussein Kattanga akizungumza wakati wa Mkutano Naibu Wasajli, Watendaji na Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi uliofanyika jijini Arusha. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ununuzi na Ugavi wa Mahakama ya Tanznaia, Bwn. David Kivembele.
Naibu Wasajili, Watendaji na Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi wakiimba wimbo wakati wa kufunga Mkutano wao jana jijini Arusha. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni