Watumishi wa Mahakama
ya Tanzania wote nchini wametakiwa kujishusha pindi wanapotoa huduma za utoaji
haki kwa wananchi wanaofika Mahakamani ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mradi
wa Maboresho ya Mhimili huo yanayoendelea.
Akifungua kikao kazi
cha Watendaji na Wataalamu wa Mahakama kutathmini Utekelezaji wa Mpango Mkakati
wa Miaka Mitano (2015/16- 2019/20) na
Utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Utoaji huduma za Mahakama unaofanyika
mjini Arusha, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka
Watumishi hao kuacha tabia binafsi ikiwemo kujikweza zinazoweza kuwa kikwazo
katika maboresho ndani ya mhimili huo.
“Kila mmoja ni kiongozi
na ni lazima tujishushe wote tulingane kwa lengo moja la maboresho ndani ya
Mhimili wa Mahakama”, alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Akitoa mfano wa
kujishusha na kutojitukuza, Jaji Mkuu alimnukuu Mwandishi wa kitabu kiitwacho “The
Making of Tanganyika”, Judith Listowel ambaye anazungumzia kutojitukuza kwa
Mwalimu wakati wa Harakati za kupigania Uhuru. Kwa mujibu wa kitabu hicho, Mwalimu
Nyerere alijiuliza ni kwa namna gani angeweza kutumikia nchi yake kwa uaminifu
na weledi bila kujidai na kujitukuza yeye binafsi.
Akizungumzia Maboresho,
Jaji Mkuu alisema mafanikio ya maboresho yanategemea kwa kiasi kikubwa
ushirikiano ndani ya Mhimili wa Mahakama na pia ushirikiano wa wadau na
wananchi ambao wako nje ya Mhimili huo.
Alisema Mradi wa
Maboresho ya Mahakama unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya
Tanzania na Benki ya Dunia unatajwa kuwa
mfano katika bara la Afrika na kwamba mradi huu unatumiwa na Benki ya Dunia kama
mfano wa Mhimili kuwa na uwezo wa ndani wa kufanya maboresho ya huduma ya
utoaji haki.
Aliwataka watumishi wa Mahakama
kuwa darasa zuri la Mradi wa Maboresho ya huduma kwa nchi nyingine za bara la
Afrika kwa kuwa nchi hizo zinasubiri mafanikio ya Mradi huo ili nazo zianzishe
kwenye nchi zao.
Aidha, Jaji Mkuu
amesema kiongozi yeyote wa Mahakama atakayechelewesha upatikanaji wa nakala za
hukumu atachukuliwa hatua za kinidhamu. Akiwa kwenye ziara ya kikazi Mahakama
Kuu kanda ya Tabora hivi karibuni, Jaji Mkuu aliwaagiza Mahakimu wote nchini
kutoa bure nakala hizo.
Kwa upande wake
Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga amewataka Watendaji
na Wataalamu wengine wa Mahakama kufanya kazi kwa ushirikiano lengo likiwa
kujenga Taasisi imara.
“Mahakama ina jukumu
kubwa la kufanya maboresho katika kazi zake za kila siku, hivyo ni vyema
kushirikiana ili kufikia azma” alisema Mtendaji Mkuu.
Aidha; Mtendaji Mkuu
alisema kuwa suala la maboresho ya Mahakama linatakiwa kueleweka kwa Watendaji
na Watumishi wote wa Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya
Rufani.
Kikao kazi hicho
kilichofunguliwa rasmi na Mhe Jaji Mkuu mapema Machi 08, kimehusisha Wakurugenzi,
Manaibu Wasajili, Mahakimu pamoja Watendaji wa Mahakama nchini kimelenga kufanya
tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano
(2015/2016-2019/2020) pamoja na Mradi wa maboresho ya Huduma za Mahakama.
Mkuu wa kitengo cha
Usimamizi wa Mradi wa Maboresho ya
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma akifafanua Jambo katika kikao
kazi hicho.
Baadhi ya wajumbe wakiwa katika kikao kazi cha Watendaji na Wataalamu wa Mahakama kutathmini Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16- 2019/20) na Utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Utoaji huduma za Mahakama.
Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Ilvin Mugeta akifafanua jambo katika kikao kazi hicho. |
Mkurugenzi wa Utawala
na Rasilimali Watu,Edward Nkembo (kulia) na Mkurungezi wa Mipango na Ufuatiliaji, Mathias Mwang’u wakifuatilia kikao hicho. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni