Na
Mary Gwera
MAHAKAMA ya Tanzania imeingia
Mkataba na Shirika la Posta Tanzania kutoa huduma za usafirishaji wa nakala za
hukumu, barua na nyaraka muhimu za Mahakama.
Mkataba huo ulisainiwa
na Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta mapema
Aprili 05 katika Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mahakama ya Rufani-Dar es
Salaam.
Mkataba huu chini ya
huduma mpya ya Posta mlangoni (The post
at your doorstep) iliyoanzishwa na Shirika la Posta hivi karibuni, utalipa
jukumu la kukusanya na kusafirisha/kusambaza nakala za hukumu na nyaraka
mbalimbali za Mahakama na kuzifikisha kwa wahusika kulingana na anwani zao na
mahali walipo (Anwani za makazi).
Akizungumza kabla ya
utiani saini wa mkataba huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Hussein Kattanga
amesema kuwa hatua hii ni mwendelezo wa maboresho mbalimbali yanayoendelea
kufanyika ili kuwafikia wananchi.
Aidha; Mtendaji Mkuu
amelitaka Shirika hilo kutekeleza makubaliano hayo kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja
na kusambaza nakala za hukumu na nyaraka nyingine kwa wahusika na kwa wakati.
“Sitarajii kuona
wananchi wanapanga foleni Mahakamani kutafuta hukumu zao na nyaraka nyingine,
nina imani kuwa Posta mtafanya kazi ya kukusanya na kusambaza nyaraka hizo kwa
wananchi ipasavyo,” alisema Mtendaji Mkuu.
Naye Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Katarina Revocati ameeleza kufurahishwa kwake na hatua ya utiaji saini wa Mkataba huo
kwani utasaidia kufikia ndoto ya Mahakama ya muda mrefu ya kuwafikia wananchi
kwa karibu zaidi.
“Naomba kusema kuwa,
nimefurahishwa sana na hatua hii , kwani ni ndoto ya Mahakama ya muda mrefu,
vilevile hatua hii itarahisisha utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Jaji Mkuu ya
kutoa nakala za hukumu bure kwa zitawafikia wananchi popote watakapokuwa,”
alisema Mhe. Revocati.
Kwa upande wake Posta
Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe alisema
alimuhakikishia Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa watafanya kazi hiyo kwa ufanisi
mkubwa.
“Kusainiwa kwa Mkataba
huu kutawezesha pia kuongeza kasi ya usambazaji wa barua za kawaida za Mahakama
kuwafikia walengwa mapema zaidi kwani zitachukuliwa Mahakamani na Maofisa wa Posta na kupelekwa
moja kwa moja kwa wahusika/mhusika,” alisema Bw. Mwang’ombe.
Vilevile Mkuu huyo
alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Maofisa wa Posta hususani kwa
kuandika anwani za makazi pamoja na postikodi.
Hafla hiyo fupi
ilihudhuriwa na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka Mahakama ya Tanzania pamoja
na Shirika la Posta Tanzania.
Mtendaji Mkuu, Mahakama
ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga (aliyeketi katikati) akiongea jambo katika
hafla fupi ya utiani saini ya mkataba wa utoaji huduma ya usambazaji wa nyaraka
mbalimbali za Mahakama huduma ambayo itatolewa na Shirika la Posta Tanzania.
Msajili Mkuu- Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati akiongea jambo katika hafla hiyo. (Waliosimama) wa kwanza kulia ni Mtendaji-Mahakama ya Rufani, Bw. Sollanus Nyimbi, wa pili kulia ni Msajili-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ilvin Mugeta, wa tatu ni Mtendaji-Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na Maofisa kutoka Shirika la Posta Tanzania.
Postamasta Mkuu wa
Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe akiongea jambo kabla ya
kutiliana saini Mkataba kati la Shirika la Posta na Mahakama ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu, Mahakama
ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga (katikati) akitia saini Mkataba huo,
anayeshuhudia kulia ni Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina
Revocati aliyeketi kushoto ni Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw.
Hassan Mwang’ombe, wanaoshuhudia (waliosimama) ni baadhi ya Viongozi/Maafisa
kutoka Mahakama na Shirika la Posta.
Postamasta Mkuu wa
Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe akitia saini Mkataba huo.
Mwanasheria wa Mahakama
ya Tanzania, Bi. Peace Mpango akitia saini Mkataba huo aliyeketi kushoto ni
Mwanasheria kutoka Shirika la Posta, waoshuhudia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama
kulia pamoja na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta.
Wakikabidhiana Mikataba
hiyo kwa nyuso za furaha mara baada ya kuhitimisha zoezi la utiaji saini. Kulia
ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga na kushoto ni Postamasta
Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni