Jumatano, 4 Aprili 2018

TUMIENI RASILIMALI ZILIZOPO KUFIKIA MALENGO: JAJI ABOUD

Na Amina Ahmad- Mahakama Kuu, Tanga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud ameziagiza Mahakama za kila ngazi kwenye kanda yake kuhakikisha zinatumia rasilimali chache zilizopo katika kufikia malengo ya vipaumbele vya Mahamaka ya Tanzania.

Jaji Aboud pia aliwataka Watumishi wa Kanda ya Tanga kuhakikisha wanafanikisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/2016 hadi 2019/2020) kwa kutumia rasilimali chache zinazopatikana ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili Mhimili huo katika kutekeleza jukumu lake la Msingi na la kikatiba la Utoaji wa Haki kwa wananchi.
Akizungumza kwenye kikao cha Menejimenti ya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga kilichofanyika hivi karibuni jijini Tanga, Jaji Aboud alizielekeza Mahakama zote zilizo kwenye kanda hiyo kuhakikisha zinasimamia kikamilifu utekelezaji wa Waraka Namba 1 wa mwaka 2018 wa Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, unaotoa Mwongozo wa namna bora ya utoaji wa nakala za hukumu bure kwa wadaawa na wananchi kwa ujumla.

Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Tanga ilifanya kikao cha Menejimenti ya Kanda ambapo pamoja na mambo mengine kilijadili na kupitisha Bajeti mpya ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa vituo vyake vyote ambavyo ni Mahakama kuu, Mahakama ya Mkoa, Mahakama za Wilaya pamoja na Mahakama za mwanzo.
Mbali ya kuhudhuriwa na wajumbe wake wa kawaida, kikao hiki pia kiliwashirikisha Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama zote za Mwanzo ili kutekeleza dhana ya Bajeti shirikishi.

Katika kikao hicho, taarifa za kiutendaji kutoka kila kituo yaani Mahakama ziliwasilishwa na wakuu wa Idara na Vitengo wa Kanda, Mahakimu wakazi Wafawidhi na Maafisa Utumishi/Tawala kutoka Mahakama za Wilaya na Mkoa.

Aidha, Jaji Mfawidhi pia alitumia fursa hiyo kuwaagiza Watendaji wa Mahakama waliohudhulia kikao cha kutathmini Mpango Mkakati wa Mahakama hivi karibuni jijini Arusha, kutoa mafunzo kwa watumishi wenzao juu ya umuhimu wa Mpango Mkakati huo ili kuwajengea uelewa wa kina hatimaye waweze kuumiliki na kuutumia kama Dira na Mwongozo thabiti katika kazi za kuwapatia wananchi haki.
  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud, (katikati) akiongoza kikao cha Menejimenti ya Kanda, kulia ni Naibu Msajili Mhe. Adrian Kilimi na Kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Crisencia M. Kisongo.
  Mtendaji wa Mahakama kuu kanda ya Tanga, Bwn. Ahmed Ng’eni akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti 2017/2018 kwa wajumbe wa kikao cha menejimenti ya Kanda.

  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Mahakama ya Wilaya Korogwe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vitengo wa Mahakama Kuu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Tanga, na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama akifuatana na Mhe. Kasim S. Mkwawa, Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mahakama ya Wilaya Muheza.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni