Alhamisi, 26 Aprili 2018

MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA YA TANZANIA KUJENGWA MKOANI DODOMA: JAJI MKUU AZINDUA ENEO LA KIWANJA KWA KUPANDA MITI



Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
JAJI Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma amezindua zoezi la upandaji miti katika eneo la Kiwanja cha Mahakama ya Tanzania kilichopo  eneo la ‘NCC LINK’(Mlimani) mkoani Dodoma.
Akizungumza katika Sherehe ya Upandaji miti, Aprili 26 mjini Dodoma, Mhe. Jaji Mkuu aliweka bayana faida mbalimbali za miti na utunzaji mazingira kwa ujumla kuwa ni pamoja na kupambana na tabia nchi.
“Kwasababu leo ni siku ya kupanda miti, ningependa tu nieleze faida za miti, kwanza ni kupambana na tabia nchi, pili kusafisha hewa, kupunguza joto, kutunza vyanzo vya maji na kadhalika kwani faida zake zipo nyingi zaidi ya 50,” alieleza Mhe. Prof. Juma.
Akiongelea juu ya Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa ujenzi huo utaanza ndani ya mwaka huu baada ya taratibu zote kukamilika.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakama imepanga kujenga jengo zuri litakalovutia na kuwawezesha Watumishi kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Awali, akitoa taarifa ya kiwanja hicho ikiwa ni pamoja na mipango ya ujenzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango-Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso alisema kuwa  tayari utafiti wa Kijiosayansi kubaini hali ya miamba na athari za matetemeko katika eneo hilo umeshafanyika na matokeo yameonyesha eneo hilo linafaa kwa ujenzi.
“Aidha hatua za mwisho za ununuzi za kumpata Mtaalam Mshauri kupitia michoro hiyo zipo karibu kukamilika na matarajio ni kuanza ujenzi ndani ya mwaka huu, 2018,” alisema Bw. Uisso.
Sherehe za uzinduzi wa upandaji miti zilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Jaji Kiongozi-Mahakama Kuu ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu-Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Watumishi wa Mahakama na wengineo.
Mara baada ya uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, Mahakama ilifanya jitihada mbalimbali za upatikanaji wa Viwanja kwa ajili ya ujenzi, ambapo  juhudi hizo zilizaa matunda Desemba 07, 2017 wakati Mhe. Rais alipoahidi kuipatia Mahakama eneo la kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akitoa neon kabla ya uzinduzi rasmi wa zoezi la upandaji miti katika eneo la Kiwanja cha Mahakama itakapojengwa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania mkoani Dodoma.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akizungumza jambo kwa Watumishi na Wageni Waalikwa (hawapo pichani) waliohudhuria katika sherehe hizo, Mhe. Jaji Kiongozi amewataka Watumishi wa Mahakama Mkoani humo kutunza miti hiyo pamoja na Mazingira ya eneo hilo kwa ujumla.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza jambo, ameipongea Mahakama kwa kupata eneo zuri kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dodoma, Mhe. Mwanaisha Kwariko akizungumza katika Sherehe hizo.
Mkurugenzi Msaidizi-Mipango-Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso akitoa taarifa ya kiwanja hicho na hatua iliyofikiwa katika kuanza rasmi kwa ujenzi wa jengo la Makao Makuu.

Baadhi ya Sehemu ya Watumishi pamoja na Wageni waalikwa na Wananchi walioshiriki katika Sherehe hizo.
Meza Kuu ikiongozwa na Mhe. Jaji Mkuu wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kikijiri katika sherehe hizo, aliyeketi wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali, wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Mhe. Hussein Kattanga, wa kwanza kushoto ni Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati, na Viongozi mbalimbali walioshiriki katika sherehe hizo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa upandaji miti, kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, kushoto ni Mhe. Ferdinand Wambali,Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akipanda mti wake.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akipanda mti.
Watumishi na Wadau mbalimbali nao walishiriki katika zoezi la kupanda miti.
(Picha na Mary Gwera)
 
 
 



 
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni