Na
Lydia Churi-Mahakama
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
amewaapisha Majaji Kumi pamoja na viongozi wengine wa sekta ya sheria
aliowateua hivi karibuni na kuwataka kutanguliza maslahi ya Taifa
wanapotekeleza majukumu yao ili nchi iweze kusonga mbele.
Akizungumza
katika hafla ya kuwaapisha viongozi hao iliyofanyika Ikulu jijini Dar es
salaam, Rais Magufuli pia amewataka Majaji aliowaapisha kumtanguliza Mungu ili
waweze kutenda haki kwa kuwa kazi ya Jaji inahitaji mtu kumtanguliza Mungu hasa
katika kufanya maamuzi.
“Ninaamini
nimeteua watu wenye sifa zinazostahili pamoja na maadili hivyo fanyeni kazi
zenu kwa kuzingatia maadili mema na kwa maslahi ya Tanzania ili tusonge mbele”,
alisisitiza Mhe Rais.
Wakati
huo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji
walioapishwa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa bidii ili kumaliza kesi kwa
wakati na pia kuendana na kasi ya mahakama ya kumaliza mlundikano wa kesi Mahakamani.
“Naamini
wote mlioteuliwa kwenye nafasi hii ya Jaji mna sifa zote za kufanya kazi hii,
sasa kilichobaki kwenu ni kuthibitisha kwa vitendo”, alisema Jaji Mkuu na
kuongeza kuwa maisha yote ya Jaji ni ya kupimwa na kwamba kazi yao tayari
imeanza kupimwa leo.
Aidha,
Jaji Mkuu aliwataka Majaji hao kufuata maadili na kuacha tabia zisizofaa kama
vile ulevi, kudai wasiyostahili, kusababisha mlundikano wa kesi mahakamani kwa
kuahirisha kesi bila sababu za msingi pamoja na mienendo yote isiyoendana na
maadili ya kazi yao.
Akizungumzia
hali ya kesi mahakamani, Jaji Mkuu aliwaambia Majaji walioapishwa kuwa kazi ya
kuwa Jaji ina changamoto ya wingi wa kesi za mlundikano kwenye Mahakama
mbalimbali nchini ambapo alisema hivi sasa mzigo wa mashauri kwa kila Jaji
umepungua kutoka kesi 535 na kufikia kesi 460.
Alisema
Mahakama ya Tanzania imejiwekea mkakati utakaowezesha kupungua na hatimaye
kumalizika kwa mlundikano wa kesi mahakamani. Kufuatia mkakati huo, kila Jaji
amepangiwa kusikiliza na kumaliza 220 kwa mwaka na kwamba kesi isikae
mahakamani kwa zaidi ya miaka miwili kwa Mahakama Kuu.
Kwa
mujibu wa mkakati huo, katika Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za
wilaya kesi haipaswi kukaa mahakamani kwa zaidi ya miezi 12 wakati katika
Mahakama za Mwanzo kesi zinatakiwa kumalizika katika kipindi cha miezi sita.
Aidha, kila hakimu anatakiwa kusikiliza na kumaliza kesi 250 katika kipindi cha
mwaka moja.
Naye
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu wa
Mahakama ya Rufani Mhe. Harold Nsekela aliwaasa Majaji walioapishwa leo
kujiepusha na tabia zilizo kinyume na maadili kwa kuwa kazi waliyopewa
inawapasa kuwa na maadili ya hali ya juu.
“Suala
la maadili kwa Majaji ni la msingi sana hivyo ni vizuri mkaishi kwa kufuata na
kuzingatia maadili”, aliongeza Jaji Nsekela.
Aprili
15 mwaka huu, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Majaji
10 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka , Wakili Mkuu
wa serikali na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
Walioteuliwa
kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni Mhe. Ilvin Mugeta, Mhe. Elinaza
Luvanda, Mhe. Yose Mlyambina, na Mhe. Immaculata Banzi. Wengine ni Mhe. Mustafa
Siyani, Mhe. Paul Ngwembe, Mhe. Agnes Mgeyekwa, Mhe. Stephen Magoiga, Mhe. Thadeo
Mwenempazi na Mhe. Butamo Philip.
Aidha,
Rais alimteua Dkt. Evaristo Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Bw. Edson Makallo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Dkt. Julius Mashamba kuwa
Wakili Mkuu wa Serikali na Dkt. Ally Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
Baadhi ya Wahe. Majaji
wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakisubiri kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mapema Aprili 20, 2018
Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Ilvin
Mugeta kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Sherehe hizo za kuapishwa jumla
ya Majaji 10 wa Mahakama Kuu pamoja na Viongozi wengine wa Sekta ya Sheria
zilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mapema Aprili 20, 2018 na zilihudhuriwa
na Viongozi mbalimbali wa Serikali, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na
Mahakama, Wakuu wa Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dinim, Watumishi wa Mahakama
na kadhalika. Kabla ya uteuzi wake, Mhe. Mugeta alikuwa Msajili wa Mahakama Kuu
ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Elinaza
Luvanda kuwa Jaji wa Mahakama Kuuu ya Tanzania, kabla ya uteuzi huu, Mhe.
Luvanda alikuwa Katibu wa Mhe. Jaji Mkuu
wa Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Yose
Joseph Mlyambina kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Immaculata
Kajetan Banzi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Mustapher
Siyani kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kabla ya uteuzi Mhe. Siyani
alikuwa Naibu Msajili, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe.
Paul Joel Ngwembe kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Agnes
Zephania Mgeyekwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Stephen Murimi
Magoiga kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Thadeo
Mwenepazi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Butamo
Kasuka Philip kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Waheshimiwa Majaji
wapya wakisaini kiapo cha maadili ya Sektretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea jambo mara baada
ya kuwaapisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Picha ya pamoja baada
ya uapisho: katikati ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John
Pombe Magufuli, wa tatu kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma, wa tatu kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba
Kabudi, wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu- Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Prof.
Sifuni Mchome, wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Ferdinand Wambali na wa pili kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe.
Adelardus Kilangi, katika uapisho walioapishwa ni pamoja na Naibu Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Wakili Mkuu wa Serikali na
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni