Jumamosi, 28 Julai 2018

MAAFISA HABARI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUITANGAZA MAHAKAMA

Na Lydia Churi-Dodoma
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mhe. Mohamed Awadh amefunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Mahakama kuhusu masuala ya habari na kuwataka watumishi hao kutumia ujuzi walioupata kutangaza kwa jamii shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania.

Akifunga mafunzo hayo jana mjini Dodoma, Jaji Awadh alisema baada ya watumishi kupata mafunzo hayo, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuwa sasa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wake ya kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama na kushirikisha wadau itatekelezwa kwa kuonyesha mabadiliko na mafanikio kwa kiwango cha juu zaidi.

Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia ujuzi walioupata kutoa habari za yanayofanywa na Mahakama kwa wananchi na kushirikisha wadau ili Mahakama ya Tanzania ionekane ni sehemu wazi kwa kila wananchi na siyo mahali pa kuogopwa kama ilivyo.

Jaji Awadh aliwataka watumishi hao kuonyesha matunda ya kile walichokipata kupitia mafunzo ya kuwajengea uwezo kwa kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wanaofika Mahakamani kufuatilia haki zao.

Mafunzo ya siku tano kwa Watumishi wa Mahakama pamoja na baadhi ya Taasisi wadau wa Mahakama yaliandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha Maafisa Habari, Maafisa Utumishi, Maafisa Tawala, Maafisa Tehama pamoja na Wasaidizi wa Kumbukumbu kutoka Kanda zote za Mahakama Kuu ya Tanzania na Divisheni zake, Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Taasisi wadau wa Mahakama zikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Kurekebisha Sheria, na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. 
 Mkurugenzi Msaidizi wa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Bibi Agatha Ng'ingo akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji wa Mahakama ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mohamed Awadh ili afunge Mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania kuhusu masuala ya Habari yaliyofanyika mjini Dodoma.
 Jaji wa Mahakama ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mohamed Awadh akifunga Mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania jana mjini Dodoma.
 Afisa Utumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Festo Hamisi Sanga akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Maafisa wote wa Mahakama waliohudhuria Mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania 
mjini Dodoma.
 Afisa Tehama wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Simon Lyova akipokea cheti baada ya kumaliza Mafunzo jana.
  Afisa Tehama wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Dhillon John akipokea cheti baada ya kumaliza Mafunzo jana.

Afisa Tawala Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Moses Mongi akipokea cheti baada ya kumaliza Mafunzo jana.
Afisa Tehama wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi, Angela Meela  akifurahia mara baada ya kupokea cheti. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni