Alhamisi, 2 Agosti 2018

WIZARA YA SHERIA NA KATIBA YAITEMBELEA MAHAKAMA BUKOBA

Na Mushobozi Josiah, Mahakama Kuu-Bukoba
Timu maalum kutoka wizara ya Sheria na Katiba na ile ya Mambo ya Ndani ya Nchi wameitembelea Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Bukoba ikiwa ni sehemu ya ziara yao iliyolenga kuboresha upatikanaji wa haki nchini.

Timu hiyo inayoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Prof. Sifuni Mchome imemuelezea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Bukoba Mhe. Salvatory Bongole kuwa lengo la ziara hiyo ni kuangalia hali halisi ya Magereza, kutatua changamoto ya mlundikano wa Mahabusu na wafungwa Magerezani na kuhimiza na kudumisha ushirikiano na Taasisi zilizo kwenye sekta ya Sheria.

  
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Prof. Sifuni Mchome akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Bukoba Mhe. Salvatory Bongole(wanne kulia) pamoja na viongozi wengine walipotembelea Mahakama hiyo.

Aidha, ujumbe huo uliainisha changamoto mbalimbali zilizopo katika mfumo wa utoaji haki kwenye kanda ya Bukoba na kuahidi kwenda kuzifanyia kazi ili kuboresha suala zima la utoaji na upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Baadhi ya changamoto hizo ni upungufu wa waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, upungufu wa fedha za uendeshaji wa vikao vya mashauri mahakamani, pamoja na tatizo la usafirishaji wa washtakiwa/mahabusu kutoka magerezani kwenda Mahakamani hasa kwenye Mahakama zilizo mbali na Magereza na vituo vya Polisi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni