Jumanne, 3 Julai 2018

MADALALI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUBORESHA UTENDAJI KAZI WAO

Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi  amewataka Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuwa na mijadala huru itakayosaidia kuboresha utendaji kazi wao ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi kutokupata huduma bora. 

 Akifungua mafunzo ya siku tano katika awamu ya kwanza ya mafunzo  hayo leo  jijini Dar es salaam, Jaji Kiongozi amesema endapo Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama watalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi ni dhahiri kuwa Mahakama ya Tanzania pia itakuwa imelalamikiwa kwa kuwa watu hao hufanya kazi na Mahakama.

Jaji Kiongozi amesema mafunzo hayo ni mpango wa Mahakama ya Tanzania wa kuboresha huduma zake kupitia utekelezaji wa  Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/2016 – 2019/2020) ambao unalenga kutoa haki kwa wote na kwa wakati, kurejesha imani  ya wananchi kwa Mahakama na kuimarisha utawala bora na usimamizi wa rasilimali.

Alisema, kuanzishwa kwa mafunzo ya Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama ni tukio linaloonyesha maendeleo makubwa katika kazi hiyo kwa kuwa kipindi kilichopo cha uchumi wa kati kinahitaji kuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka watakaofanya kazi kwa kufuata kanuni zilizopo.

“Uchumi unapokua na migogoro nayo huongezeka hivyo hii ni fursa kwa Mahakama ya Tanzania ya kuweka mikakati mbalimbali ya namna bora ya kuboresha huduma zake hasa katika eneo hili, ndiyo maana tunaandaa mafunzo kwa watu wanaosaidiana na Mahakama katika kutoa huduma”, alisema Jaji Kiongozi”.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa Mahakama ya Tanzania inakuwa na Madalali wenye mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi.

Awali akimkaribisha Jaji Kiongozi, Mkuu wa chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo alisema mafunzo hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama ili kuwajengea uwezo na kujenga taswira nzuri ya Mahakama ya Tanzania.

Alisema sheria inaweka masharti kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuhuisha leseni za kufanyia shughuli hizo ili kutimiza matakwa ya sheria inayoongoza shughuli zao. Pamoja na mambo mengine, imeweka vigezo vya mtu mwenye kufanya shughuli hizo ambapo moja ya vigezo hivyo ni kupatiwa mafunzo ya umahiri kutoka chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Awamu ya kwanza ya mafunzo hayo inawahusu wale ambao leseni zao za kufanya shughuli za Mahakama zilifikia ukomo baada ya mabadiliko ya sheria yaliyotolewa katika tangazo la Serikali Namba 363 la Septemba 22, 2017 itahitimishwa Julai 6, mwaka huu.

Mafunzo mengine ya aina hiyo yatatolewa katika vipindi tofauti tofauti kwa lengo la kumpa fursa mtu yeyote mwenye vigezo stahiki kupatiwa mafunzo maalum yatakayomwezesha kupata cgheti cha umahiri katika udalali na usambazaji nyaraka za Mahakama.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwasili kwenye kituo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania kilichopo Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam kwa ajili ya kufungua Mafunzo ya Madalai na Wasambaza nyaraka za Mahakama.  
 Baadhi ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakimsikiliza Mhe. jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania akifungua Mafunzo yao jana jijini 
Dar es salaam. 
 Baadhi ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakimsikiliza Mhe. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania akifungua Mafunzo yao jana jijini 
Dar es salaam. 
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakati akifungua awamu ya kwanza ya Mafunzo hayo.  
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe Jaji. Dkt. Paul Kihwelo akizungumzia Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyara za Mahakama wakati wa uzinduzi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. 
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili na watumishi wengine wa Mahakama mara baada ya kufungua Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama.  
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi Mahakama ya Tanzania mara baada ya kufungua Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama.  
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama mara baada ya kufungua awamu ya kwanza ya Mafunzo yao.  
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama mara baada ya kufungua awamu ya kwanza ya Mafunzo yao. 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni