Na
Mary Gwera, Mahakama-Morogoro
Waandishi wa Habari za
Mahakama wametakiwa kufikisha habari fasaha kwa jamii inayowazunguka ipasavyo kwani
wao ni nguzo muhimu katika kufikisha taarifa.
Hayo yamesemwa mapema
leo Julai 16 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa-Morogoro,
Mhe. Elizabeth Nyembele wakati alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo ya siku tano kuhusu
Uandishi wa Habari za Mahakama.
Mhe. Nyembele alisema
kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na upotoshaji wa habari za Mahakama zinazotolewa
na baadhi ya Waandishi wa Habari za Mahakama aidha kwa makusudi au kutokujua
sheria na taratibu za uandishi wa habari za kimahakama.
“Kupitia mafunzo haya,
Mahakama inakusudia kuwapa Waandishi wa Habari mambo muhimu ya kuzingatia
katika kuandika habari za Mahakama kwa jamii na hatimae kupunguza na kumaliza
kabisa mkanganyiko wa habari za Mahakama,” alisema Mhe. Nyembele.
Mafunzo hayo ya siku
tano (5) ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na
kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) chini ya ufadhili wa Benki ya
Dunia yamelenga kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari za Mahakama ili waweze
kuripoti vyema zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano-Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin
Ndimbe alisema kuwa lengo la Mafunzo hayo ni kuwapa uelewa zaidi Waandishi wa
Habari za Mahakama kupitia mada mbalimbali zitakazotolewa.
Nao waandishi wa Habari
wanaoshiriki katika mafunzo wameisifu Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa mafunzo
hayo ambayo yatawajengea uwezo wa kuripoti habari za Mahakama kwa ufasaha
zaidi.
Mafunzo hayo
yamehudhuriwa na jumla ya Washiriki 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari
nchini zikiwemo Televisheni, redio, Magazeti na Blogu.
Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati
wake imejiwekea nguzo kuu tatu moja ya nguzo hizo ni ya Kurejesha imani ya wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau.
Kwa kuwajengea uwezo Waandishi wa habari za Mahakama, wananchi wataweza kupata
taarifa nyingi na zilizo sahihi kuhusu utendaji kazi wa Mahakama.
Hakimu Mkazi Mwandamizi
Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa-Morogoro, Mhe. Elizabeth Nyembele, akifungua rasmi
mafunzo hayo.
Sehemu ya Waandishi wa
Habari wanaoshiriki katika Mafunzo hayo.
Mkuu wa Kitengo cha
Habari, Elimu na Mawasiliano-Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe akitoa
neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Nyembele kufungua rasmi mafunzo
hayo.
Washiriki wakifuatilia
kwa makini.
Mratibu wa Mafunzo
kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto, Bw. Lameck Samson (aliyesimama
mbele) akitoa mada kwa Washiriki wa Mafunzo.
Mgeni rasmi, Hakimu
Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa-Morogoro, Mhe. Elizabeth Nyembele
(aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Washiriki wa
Mafunzo hayo (aliyeketi kulia) ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano-Mahakama
ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe, (aliyeketi kushoto) ni Mtalaam wa Mawasiliano-Kitengo cha
Maboresho ya Huduma za Mahakama, Dkt. Cosmas Mwaisobwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni