Ijumaa, 31 Agosti 2018

HAKIMU MKAZI MFAWIDHI MKOA WA ARUSHA AKAGUA MAHAKAMA YA WILAYA LONGIDO: AWAPONGEZA WATUMISHI KWA USHIRIKIANO


Na Catherine Francis – Mahakama Kuu Arusha

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Mhe. Niku Mwakatobe amewapongeza Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Longido kwa kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri jambo lililowezesha Mahakama hiyo kuweza kumudu majukumu yake kwa wakati.

Akiwa katika ziara ya ukaguzi katika Mahakama ya Wilaya ya Longido Agosti 30, 2018, Mhe. Mwakatobe alikagua utendaji kazi wa Mahakama hiyo na alipata nafasi ya kuzungumza na Watumishi wa Mahakama hiyo.

Aidha, Mhe. Mwakatobe aliwahamasisha Watumishi hao kuendeleza jitihada za kufanya kazi kwa bidii.

“Katika ukaguzi wangu nimebaini kuwa taarifa za mashauri yote huingizwa kwenye mfumo wa (JSDS) kila siku pasipo kulaza kiporo cha kazi,” alisema Mhe. Mwakatobe.

Katika ziara yake, alipata nafasi pia ya kutembelea na kujionea hatua ya ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Longido.

Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutaongeza hamasa ya kazi kwa Watumishi wa Mahakama hiyo na pia kutaongeza ubora wa huduma zitolewazo na Mahakama hiyo kwani kwa sasa wapo kwenye jengo dogo ambalo halikidhi mahitaji ya kiofisi.
     Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Mhe. Niku Mwakatobe (kushoto), akizungumza na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Longido.
UKAGUZI WA MAENDELEO YA UJENZI WA JENGO JIPYA LA MAHAKAMA YA WILAYA LONGIDO: Hakimu Mahakama ya Mwanzo Longido Mjini, Mhe. Andrew Hayuma (wa kwanza kulia) akifafanua jambo kuhusu jengo hilo lililopo katika ujenzi, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mkoa-Arusha, Mhe. Niku Mwakatobe, katikati ni Mhe. Aziza Temu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Longido, (aliyesimama nyumamwenye suti nyeusi) ni Bw. Tedfred Mloe Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Longido.
Muonekano wa  mbele wa jengo la Mahakama ya Wilaya Longido linaloendelea kujengwa.

(Picha na Catherine Francis – Mahakama Kuu Arusha)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni