Jumamosi, 1 Septemba 2018

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA KUU KANDA YA DODOMA AWAASA WATUMISHI KUENDELEZA NA KUTHAMINI MRADI WA MABORESHO


Na Rashid Omar, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Pwani

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wamekumbushwa kuendeleza na kuthamini maboresho yanayoendelea ndani ya Mahakama kupitia Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama. 

Hayo yalisemwa Agosti 31 na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma Mh. Ignas Kitusi jijini Dodoma alipokuwa akifunga rasmi mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu za ndani za Mahakama yaliyohusu usimamizi na udhibiti wa fedha za miradi ya wafadhili. 

“Kila mmoja ana jukumu kwenye mradi huu wa maboresho unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Hivyo tunawajibika kuhakikisha tunasaidia mradi huu katika kuongeza tija kwa Mahakama” Alisisitiza Mhe. Jaji Kitusi . 

Katika hotuba yake kwa washiriki wa mafunzo hayo, Mhe. Jaji Kitusi aliwasihi Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu za Mahakama kushauri namna bora katika kuwezesha kuongezeka kutumika kwa fedha za mradi. 

Mhe. Kitusi alisema kupitia mafunzo hayo ana uhakika yatasaidia kuongeza uwezo na vilevile amewashauri Wahasibu hao kuwa wawezeshaji wa  pesa kutumika badala ya kuwa kikwazo. 
“Hivyo mna kazi kubwa ya kushauri namna bora katika kutumia ,sio kuzuia tu pesa isitumike bila sababu za msingi” Alisema Mhe. Jaji Kitusi

Nao Washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Mahakama ya Tanzania, Benki ya Dunia na Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto kwa kufanikisha mafunzo hayo ambayo yamewaongezea maarifa,ujasiri na uwelewa mpana katika manunuzi na namna bora ya usimamizi na udhibiti wa fedha za mradi wa maboresho ya Mahakama.
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Dodoma Mhe.Jaji Kitusi akifunga rasmi mafunzo hayo jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza  mgeni rasmi, Mhe.Jaji Kitusi.
Mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo Ndugu Ephraim Rwakatare, Mhasibu kutoka Mahakama ya Rufani, Dar es Salaam akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki.

Washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Jaji Ignas Kitusi (katikati) baada ya kufunga mafunzo hayo. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mh. Anord Kilikiano.
 
 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni