Na Lydia Churi-Mahakama
Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali Mhe. Dkt. Ally Possi leo amekitembelea kitengo cha Usimamizi wa Utekelezaji
wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (Judiciary Delivery Unit-JDU) na kusema kuwa
endapo ofisi yake itakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu maboresho yanayofanyika
ndani ya Mahakama ya Tanzania ni wazi kuwa utekelezaji wa shughuli za Taasisi
hizo utaimarika.
Akizungumza katika
kikao kilichowakutanisha baadhi ya watendaji wakuu wa ofisi hizo, Dkt. Possi amesema
kikao hicho ni muhimu kwa kuwa Mahakama ya Tanzania ni miongoni mwa wadau
wakubwa wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Akiwa katika kikao
hicho, Dkt. Possi alipata nafasi ya kuelezewa kuhusu Mpango Mkakati wa Miaka
Mitano wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za
Mahakama kupitia Mada iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo hicho cha Maboresho Mhe.
Zahra Maruma.
Aidha, Naibu Wakili
huyo Mkuu wa Serikali pia alipata nafasi ya kuelezewa masuala mbalimbali kuhusu
namna Mahakama ya Tanzania inavyojipanga katika kushughulikia Mashauri kupitia
Mada iliyotolewa na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri Bibi Eva Nkya.
Kuhusu Mahakama
inavyotekeleza azma yake ya kuingia katika matumizi ya Teknolojia kwenye kazi
zake, Mhe. Dkt. Possi pia alipatiwa maelezo ya namna Mfumo wa Kielekitroniki wa
Takwimu za Mashauri (JSDS) wa Mahakama ya Tanzania unavyofanya kazi.
Mahakama ya Tanzania
pamoja na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zimekubaliana kushirikiana katika kubadilishana
Taarifa mbalimbali muhimu, kupitia upya sheria zinazorahisisha umalizaji wa
kesi kwa wakati Mahakamani pamoja na hatua za kuleta ufasini katika masuala ya
biashara.
Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali Mhe. Dkt. Ally Possi akiwa katika kikao cha pamoja kati ya Ofisi yake na Mahakama ya Tanzania kuzungumzia masuala mbalimbali juu ya utekelezaji wa kazi za Mahakama pamoja na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika ofisi za Kitengo cha Usimamizi wa Utekelezaji wa Maboresho ya Huduma za Mahakama.
Baadhi ya wajumbe wa kikao baina ya Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Mahakama ya Tanzania
Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali Mhe. Dkt. Ally Possi akiwa kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wa Mahakama ya Tanzania.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Utekelezaji wa Maboresho ya Huduma za Mahakama Mhe. Zahra Maruma akitoa Mada kuhusu Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania kwenye kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni