Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewasihi Watumishi wa Mahakama kuwa
na utayari katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya Teknolojia inayoanzishwa Mahakamani
ili kuendelea kuboresha huduma ya utoaji
haki nchini.
Aliyasema hayo Agosti
02, alipokuwa akiwasilishiwa mada juu ya mfumo wa ‘Video Conferencing’
utakavyofungwa na utakavyofanya kazi katika Mahakama husika iliyowasilishwa na
Mkandarasi atakayefanya kazi ya ufungaji
wa mfumo wa ‘Video Conferencing’, Kampuni ya ‘Invention Technologies.’
“Mahakama yenyewe inatakiwa
kuwa tayari kutumia mifumo mbalimbali inayowekwa ili hata Wadau wengine kama
Magereza, Polisi waweze kwenda sambasamba na Mahakama katika kuboresha huduma
ya utoaji haki,” alisisitiza Mhe. Feleshi.
Aidha Wajumbe wengine
waliohudhuria katika kikao hicho, ambao ni Majaji wawili wa Mahakama Kuu,
Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Msajili Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi wa
TEHAMA-Mahakama, na Maafisa wengineo waliunga mkono juu ya Mahakama kuwa na
mfumo huo na kumtaka Mkandarasi kutekeleza kazi hiyo kwa wakati kama
alivyoahidi.
Kwa kuanzia mfumo wa ‘Video
Conferencing’ utafungwa maeneo yafuatayo; Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu,
Kanda ya Bukoba, Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Gereza la Keko.
Aidha; Mkandarasi
anayefanya kazi hii ameahidi kukamilisha kazi hii mwishoni mwa mwezi Oktoba,
2018.
Kwa sasa mfumo wa ‘Video
conferencing’ Mahakamani umefungwa katika Kituo cha Mafunzo-Kisutu pamoja na
Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya.
Mfumo wa ‘Video
conference’ Mahakamani utasaidia na utakuwa ni chachu kubwa ya kuharakisha
uendeshaji wa mashauri, kupunguza gharama za mashahidi watokao mbalina Mahakama
husika na vilevile utasaidia hata katika kuendesha mafunzo mbalimbali ya
Watumishi wa Mahakama katika vituo vyao vya kazi.
Mahakama ya Tanzania
kupitia Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama chini ya ufadhili wa Benki ya
Dunia inaendelea na miradi mbalimbali ya maboresho yote yakiwa na lengo la
kuwapa wananchi huduma bora ya upatikanaji wa haki zao.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiongea jambo katika kikao hicho.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiongoza majadiliano mara baada ya
uwasilishwaji wa mada ya mfumo wa ‘Video Conferencing.’
Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi (mwenye suti nyeusi)
akichangia jambo katika kikao hicho.
Mtaalamu kutoka ‘Invention
Technologies’ akiwasilisha mada.
Wajumbe wakifuatilia
mada katika kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni