Jumatatu, 6 Agosti 2018

POKEENI MABADILIKO NDANI YA MAHAKAMA KWA MTAZAMO CHANYA

Na Tamim Hussein-Mahakama Kuu Mtwara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Bukoba Mhe. Lameck Mlacha amewataka watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Mtwara kuwa na moyo wa kujifunza na kuyapokea mabadiliko ndani ya Mahakama kwa mitazamo chanya ili kutoa haki kwa wakati.

Jaji Mlacha aliyekuwa Jaji wa Kanda ya Mtwara ambaye hivi karibuni amehamishiwa kanda ya Bukoba amesema watumishi hao hawana budi kuyapokea mabadiliko hasa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo ndiyo mwelekeo wa Mahakama ya Tanzania kwa sasa katika kurahisisha utoaji wa haki.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na Mahakama Kuu kanda ya Mtwara , Jaji Mlacha pia amewataka watumishi hao kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16-2019/2020)huku akiwaomba Mtendaji, Naibu Msajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo kuendelea kutoa ufafanuzi wa Mkakati huo kwa watumishi wote ili wauelewe na hatimaye kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maadili.
Aidha, Jaji Mlacha pia ameishauri Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mtwara  kuwa na programu ya mafunzo endelevu kwa watumishi wake inayolenga kuwaongezea ujuzi ili kuleta ufanisi katika suala zima la utoaji wa haki kwa wakati.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Mhe. Dkt. Fauz Twaib amempongeza Jaji Mlacha na kumuelezea kuwa ni mchapa kazi, mshauri na rafiki wa kweli. Aliongeza kuwa kutokana na utendaji wake katika utoaji wa haki uliotukuka ndiyo maana ameteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi, nafasi ambayo ni hatua nyingine katika kuendelea kuwatumikia wananchi.
Wakati huo huo, Naibu Msajili wa Mahakama kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Projestus Kahyoza amemuelezea Jaji Mlacha kuwa ni mwalimu mzuri hususan katika mashauri ya Ndoa na Mirathi huku akitolea mfano wa hukumu iliyowahi kutolewa na Jaji Mlacha ya shauri la Mirathi ya Hadija Said Matika vs. Awesa Said Matika Rufaa Namba 2/2016 ambayo imeongeza uelewa mkubwa na imekuwa kama mwongozo unaotumiwa Mahakamani na kwenye Taasisi nyingi za kisheria za wapenda haki katika masuala hayo mtambuka.

Kufuatia uhamisho wa kawaida katika utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania, Jaji Mlacha amehamishiwa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba ambapo atakuwa ndiye Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo.
  Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara wakiwa katika Hafla ya kumuaga Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Lameck Mlacha aliyehamishwa na kuteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba.
  Mhe. Lameck Mlacha ambaye sasa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Bukoba akizungumza na watumishi pamoja na uongozi wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mtwara wakati wa hafla ya kumuaga rasmi iliyofanyika hivi karibuni.
  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Mhe. Dkt. Fauz Twaib akizungumza wakati wa hafla hiyo. Kutoka kulia ni Naibu Msajili wa kanda hiyo Mhe. Projestus Kahyoza na wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama hiyo Bw. Celestine Onditi.  

Maoni 1 :