Wananchi wa Tarafa ya Mdandu
wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wameanza kupata tena huduma za kimahakama baada
ya kufungwa kwa huduma hizo miaka kumi na tisa (19) iliyopita kufuatia uchakavu
wa jengo la Mahakama hali iliyowasababishia kufuata huduma hizo umbali mrefu
zaidi.
Jengo hilo la Mahakama
ya Mwanzo Mdandu lilifunguliwa rasmi Agosti 4 mwaka huu na Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Bibi Mary.
Aidha, wakati wa
ufunguzi wa jengo hilo baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Mdandu waliipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefi kwa ajili ya
kufuata huduma za kimahakama.
Jengo la Mahakama ya
Mwanzo Mdandu wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe lilijengwa mwaka 1940 na
watawala wa Kijerumani ambapo mwaka 1999 lilifungwa kutokana na kuchakaa.
Kufuatia utekelezaji wa
Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mradi wa Maboresho
ya Huduma za mahakama, Mahakama ya Tanzania inaendelea na uboreshaji wa
miundombinu ya mahakama kwa kujenga majengo mapya ya mahakama na kuyafanyia ukarabati
yale yaliyochakaa ili kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi.
Hivi sasa Mahakama ya Tanzania
tayari inaendelea na ujenzi wa majengo 16 ya Mahakama za wilaya, majengo matano
ya Mahakama za Hakimu Mkazi na Majengo mawili ya Mahakama Kuu katika mikoa ya
Mara na Kigoma.
Jengo la Mahakama ya Mwanzo Mdandu lililozinduliwa rasmi baada ya kufanyiwa ukarabati. Jengo hili lilijengwa mwaka 1940 na watawala wa Kijerumani na baada ya kutumika kwa muda mrefu na kuchakaa, Mahakama ya Tanzania ilisitisha huduma na kulifunga mwaka 1999. Aidha, jengo hili limefanyiwa ukarabati na huduma zake kurejeshwa tena.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Mary Shangali akizungumza na Wananchi wa Mdandu (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mahakama ya Mwanzo Mdandu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Mary Shangali akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Njombe mara baada ya kufungua Mahakama ya Mwanzo Mdandu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni