Jumanne, 14 Agosti 2018

JAJI MRANGO AKARIBISHWA RASMI MAHAKAMA KANDA YA SUMBAWANGA


Na James Kapele – Mahakama ya Hakimu Mkazi- Katavi
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Jaji John Mgeta pamoja na Jaji Mfawidhi mpya wa Kanda hiyo, Mhe. David Mrango kwa pamoja wametembelea mkoani Katavi kwa lengo la kukabidhiana na kumtambulisha Jaji mpya aliyehamia katika Kanda hiyo.

Waheshimiwa Majaji hao walitembelea Mkoani Katavi mapema Agosti 13, kwa lengo  la kumkaribisha na kumtambulisha Mhe, Jaji David Mrango ambaye amehamishiwa katika Kanda ya Sumbawanga akitokea katika Kanda ya Songea. 

Ziara hii pia imempa fursa  Jaji Mgetta ya kumkabidhi eneo la kiutendaji la Mkoa wa Katavi  Jaji Mrango ambalo ni Sehemu ya Kanda ya Sumbawanga na kuwaaga watumishi wa Mahakama na wadau wengineo  wa Mahakama.
                    
Wakiwa mkoani  Katavi wamefanya kikao pamoja na watumishi wa Mahakama Mkoani humo ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wote wamewaasa watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa upendo utii na unyenyekevu kwa lengo la kuhakikisha kwamba wadau wa Mahakama wanahudumiwa kwa weledi na kwa wakati.  

Akimkaribisha Jaji Mrango katika Mkoa wa Katavi Mhe, Jaji Mgetta amewataka watumishi wa Mahakama na kuwaomba kwa dhati kushirikiana na Mhe, Jaji Mrango kwa kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanasonga mbele.

“Naomba mumpe ushirikiano wote Mhe. Jaji Mrango ikiwezekana hata zaidi ya ule mlionipa mimi ili aweze kufanya kazi yake kwa wepesi zaidi, zidisheni upendo miongoni mwenu kwa kuwa nyinyi nyote mnajenga nyumba moja” Alisema Jaji, Mgetta.        

Kwa upande wake Mhe, Jaji David Mrango licha ya kuwashukuru watumishi wa Mahakama kwa mapokezi mazuri amewasihi kuwa na utii na unyenyekevu katika kuwahudumia wananchi bila kujali hali zao, amewataka pia kufanya kazi kwa kujituma kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo. 

Nao Watendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga Ndugu Emmanuel Munda na Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Katavi  Ndugu Ipyana Kakuyu  wote kwa umoja wao wamemshukuru sana Mhe, Jaji Mgeta ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa utendaji wake wa kazi  uliyotukuka kwa kipindi chote alichotumikia Mahakama katika kanda ya Sumbawanga.  

Aidha Watendaji hao kwa umoja wao wamemkaribisha pia Mhe. Jaji Mrango katika Kanda ya Sumbawanga na kumhakikishia kumpa ushirikiano katika maeneo mbalimbali katika kuboresha huduma ya Mahakama kwa wananchi.
                                     
Awali kabla ya kufanyika kwa kikao hicho na Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi, Waheshimiwa Majaji walitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na kupokelewa na Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Mkuu wa Wilaya wa Mpanda Mhe. Lilian Charles Matinga ambapo nao  wamemshukuru sana Mhe. Jaji Mgetta kwa ushirikiano wake aliyowaonyesha katika kipindi chote alichofanya nao kazi katika Kanda hiyo.
 
Katika hatua  nyingine Mhe, Jaji Mgetta amemtembeza na kumuonyesha baadhi ya miradi kadhaa ya ujenzi na uboreshaji miundo mbinu ya majengo ya Mahakama Mkoani Katavi. 

Miongoni mwa miradi waliotembelea ni Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi  unaojengwa na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Katika kuhitimisha zoezi la ukaguzi wa Miradi hiyo ya ujenzi Wahe. Majaji hao pamoja na viongozi wengine wa Mahakama walitembelea na kukagua hatua iliyofikiwa ya Mradi wa upanuzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mpanda ambalo linajengwa kwa ubunifu wa viongozi  waandamizi wa Mahakama Mkoa wa Katavi.

 Mhe. Jaji Mrango amehamia Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga akitokea Mahakama Kuu Kanda ya Songea, naye Jaji Mgetta amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo awali alikuwa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Mhe, Jaji John Samwel Mgetta aliyesimama kushoto akimkaribisha Mhe, Jaji David Mrango ili awasilimie watumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi waliohudhuria kikao hicho.
Mhe, Jaji David Mrango aliyesimama akiwashukuru watumishi  wa Mahakama  Mkoa wa Katavi kwa mapokezi mazuri.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi wakiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji, Jaji John Mgetta (wa pili kulia) na Mhe. Jaji David Mrango baada ya kikao kumalizika, wa pili kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, Bw. Emmanuel Munda Aliyeketi kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi, Bw.Ipyana Kakuyu.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni