Ijumaa, 17 Agosti 2018

JAJI MZUNA NA MAJAJI WENZAKE WAKABIDHIWA RASMI OFISI YA MAHAKAMA KANDA YA ARUSHA


Na Catherine Francis –Mahakama Kuu Arusha
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Mosses Mzuna amekabidhiwa rasmi Kanda hiyo ya Mahakama na aliyekuwa Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe Jaji Sekela Moshi.

Makabidhiano hayo yamefanyika mapema Agosti 16 katika kikao cha utambulisho wa  wahe.Majaji wapya pamoja na  Jaji Mfawidhi ambayo pia yalihudhuriwa na  baadhi ya Watumishi wa Mahakama.

Katika kikao hicho Mhe Jaji Moshi aliwasisitiza watumishi wa Mahakama Arusha kuendeleza ushirikiano, uwajibikaji na kufanya kazi kwa malengo kwani hiyo ndiyo sababu inayoifanya Arusha kuwa kanda ya mfano kwa mafanikio. 

Jaji Sekele aliendelea kuwahimiza watumishi  waache kufanya kazi kwa mazoea bali wajitume kwa bidii ili kuweza kuondoa kabisa mlundikano wa kesi Mahakamani.

Kwa upande wake, Mhe Jaji Mzuna alimshukuru Mhe Jaji Moshi kwa mapokezi mazuri aliyoyaandaa yeye pamoja na viongozi wake, pia aliwaomba watumishi ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kila siku. 

Kwa kusisitiza hilo alinukuu usemi wa mwandishi John C Maxwell usemao “VALUE TEAM LEADERSHIP ABOVE INDIVIDUAL  LEADERSHIP” akiwa na maana ya kuwa uongozi mzuri ni ule wa ushirikiano na siyo wa mtu binafsi.

Vilevile; Mhe Jaji Mwenempazi ambaye amepangiwa kazi katika Kanda hiyo ya Mahakama naye aliwaomba ushirikiano wa hali ya juu Watumishi kwa kuwa yeye ni mgeni. 

Mhe. Jaji Mwenempazi alisema kuwa yupo tayari kujifunza kutoka kwa Watumishi mbalimbali pasipo kujali ngazi ya mtumishi husika,hivyo aliwaomba watumishi kuwa tayari kumsaidia pindi atakapohitaji msaada.

Sambamba na Mhe Jaji Mfawidhi, Majaji wengine walioripoti katika Kituo hicho ni pamoja na Mhe Jaji Issa Maige aliyetokea Mwanza na Mhe Jaji Thadeo Mwenempazi ambaye ni Kituo chake cha kwanza tangu ateuliwe kuwa Jaji.

Kabla ya uhamisho huu, Mhe . Jaji Mzuna alikuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam na Mhe. Jaji Sekela alikuwa Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, ambaye naye  amepata uhamisho wa kwenda Mahakama Kuu kanda ya Songea kuwa Jaji Mfawidhi. 
 Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe Jaji Mosses Mzuna (katikati), kushoto ni aliyekuwa Kaimu Jaji Mfawidhi Mhe Jaji Sekela Moshi na Mhe. Jaji Thadeo Mwenempazi walipokuwa wakizungumza na Watumishi wa Mahakama, Kanda ya Arusha (hawapo pichani).
Mhe. Jaji Mfawidhi  (aliyesimama) akizungumza na Watumishi.
Watumishi wakiwa katika kikao cha Mhe. Jaji Mfawidhi.
Mhe Jaji Sekela Moshi (aliyesimama) akizungumza  jambo kwa watumishi wa Mahakama Arusha.

Mhe Jaji Thadeo Mwenempazi (aliyesimama) akizungumza jambo na Watumishi.

 
 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni