Ijumaa, 17 Agosti 2018

WAJUMBE WAPYA WA BARAZA LA UONGOZI WA TAWLA WAJITAMBULISHA KWA MHE. JAJI MKUU


Na Magreth  Kinabo, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma  amekitaka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kufanya tafiti katika baadhi ya Sheria ambazo zinahitaji marekebisho ili kuweza  kuongeza uzito wa mabadiliko  hayo.

Mhe. Jaji Mkuu aliyasema hayo mapema Agosti 17, alipotembelewa na wajumbe wapya wa Baraza la Uongozi wa TAWLA, ambao waliongozwa na Mwenyekiti  wao, Bi. Athanasia Soka  na Mkurugenzi  wa TAWLA, Bi. Tike  Mwambipile, waliofika kwa ajili ya kujitambulisha rasmi. 

Akizungumzia kuhusu mabadiliko hayo ya Sheria, Jaji Mkuu alisema  yanawezekana kufanyika endapo utatifi wa kina utafanyika ili kuongeza uzito wa mabadiliko hayo,  “ni vizuri unapotaka kufanya mabadiliko kisheria kufanya utafiti ,tunaweza kufanya kwa kushirikiana,”  alisema Jaji Mkuu.

Awali  akizungumzia kuhusu mabadiliko ya Sheria yanayohitajika, Mkurugenzi huyo wa TAWLA, Bi. Tike Mwambipile, aliitaja Sheria ya  ndoa.

 “Katika sheria hii mathalani kumekuwa na mgawanyo wa mali usio sawa  hususani pale ambapo mwanaume  inapothibitishwa ndiye  anamiliki  mali  hupata asilimia  nyingi na  mwanamke  hupata  asilimia chache wakati ikithibitika mwanamke ndiye anamiliki  mali hugawanywa asilimia 50 kwa asilimia 50,” alisema Bi. Mwambipile.

Mbali na sheria ya ndoa, Wajumbe hao pia waliitaja sheria ya Mtoto kuwa miongoni mwa Sheria zinazohitaji kufanyiwa marekebisho hususani kumlinda mtoto pale anapofanyiwa Ukatili wa kijinsia mfano kubakwa.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu aliwataka pia kuweka rekodi za takwimu  vizuri na kuongeza kwamba  hilo ni eneo ambalo, Mahakama   inahitaji kufanya kazi kwa ushirikiano na chama  hicho.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao, walizungumzia jinsi ya kuweza kushirikiana  katika kesi za ubakaji, namna ya kumaliza kesi za migogoro ya mirathi kwa kutumia  upatanishi na usuluhishi kabla ya  shauri kufunguliwa Mahakamani  na uendeshaji wa kesi za ukatili wa kijinsia (GBV).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akimsikiliza Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Tanzania, Bi. Tike Mwambipile (kulia) pindi yeye pamoja na Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa TAWLA walipotembelea Mhe. Jaji Mkuu ofisini kwake, Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akiongea jambo na Viongozi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) hawapo pichani.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TAWLA), Bi. Athanasia Soka (kushoto) akimueleza jambo Mhe. Jaji Mkuu.



Mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TAWLA), Bi. Nelly Mwasongwe akiongea jambo katika Majadiliano hayo.

Mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TAWLA), Bi. Happiness Mchaki (mwenye blauzi wa bluu) akichangia jambo wakati wa mazungumzo kati ya Mhe. Jaji Mkuu na Uongozi wa Chama hicho.
Mhe. Jaji Mkuu akikabidhi zawadi mbalimbali kwa Mwenyekiti wa TAWLA, Mhe. Jaji Mkuu pia amewapatia nakala za Mpango Mkakati wa Mahakama.
 Viongozi wa TAWLA wakifurahia zawadi walizopatiwa na Mhe. Jaji Mkuu.
Mhe. Jaji Mkuu akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa TAWLA, Bi. Athanasia Soka.
 Mhe. Jaji Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa TAWLA, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Bi. Tike Mwambipile na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa TAWLA, Bi. Athanasia Soka pamoja na Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chama hicho waliomtembelea Mhe. Jaji Mkuu.


(Picha na Mary Gwera, Mahakama)



 
 
 
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni