Na
Mary Gwera
Mahakama Kuu, Kanda ya
Dar es Salaam imezindua rasmi programu maalum ya kuzungumza na wateja wake kwa
lengo la kutoa elimu kuhusu taratibu mbalimbali za Kimahakama na vilevile
kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma zake.
Akizindua rasmi zoezi hilo
mapema Agosti 29, kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu- Kanda ya Dar es
Salaam; Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Ilvin Mugeta alisema
kuwa zoezi hili ni miongoni mwa maboresho ya Mahakama ikiwa ni mkakati wa
kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.
Katika maneno yake ya
ufunguzi, Mhe. Jaji Mugeta alisema kuwa zoezi hilo litakuwa likifanyika mara
moja kwa juma, ambayo ni Jumatano ya kila wiki kuanzia saa 02:00 asubuhi hadi
saa 02:15 asubuhi.
“Sisi Mahakama Kuu,
Kanda ya Dar es Salaam, tumeona ni vyema tukawa na muda mfupi angalau mara moja
kwa wiki kuzungumza na wateja wetu na Umma wote kwa ujumla kuhusu huduma zetu,”
alisema Jaji Mugeta.
Kwa upande wake, Naibu
Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga
alisema kuwa lengo la kampeni hiyo si tu kutoa elimu bali pia kupokea
changamoto mbalimbali kutoka kwa wateja kwa lengo la kujiboresha zaidi katika
utoaji wa huduma zake.
Mhe. Tiganga alitoa
wito kwa wananchi kutosita kutoa
malalamiko yao kwa Watumishi wa Kanda hiyo ikiwemo Manaibu Wasajili na Makarani
ili waweze kupatiwa ufumbuzi.
Aidha; mbali na kuwaona
Wasajili wa Makarani wa Kanda hiyo, Mhe. Tiganga aliwataka wananchi pia kutuma
Malalamiko yao kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu nambari 0735 501 400.
Nao baadhi ya Wananchi
walioshiriki katika uzinduzi huo waliipongeza Mahakama kwa uamuzi huo kwani
itawasaidia kujua zaidi taratibu mbalimbali za Mahakama na kuondoa baadhi ya
maswali waliokuwa wakijiuliza.
Bw. Rajab Mwimi na
Bi.Hamisa Chaurembo ni miongoni mwa wananchi walioshiriki katika zoezi hilo,
ambapo waliipongeza Mahakama Kanda ya Dar es Salaam kwa kuanzisha huduma hiyo
ambayo itawarahisishia katika kutafuta huduma ya haki zao.
“Zoezi hili nimelipokea
vizuri na nimelipenda, tunaishukuru Mahakama kwa kusikiliza kero za wananchi na
kutuelimisha, vilevile naiomba iendelee kusukuma kesi haraka na haki
zitendeke bila upendeleo,” alieleza Bi. Chaurembo.
Zoezi la utoaji elimu
kwa wananchi na kuwasikiliza wateja wanaofika katika Mahakama nchini tayari
limeshaanza katika Kanda mbalimbali za Mahakama, ikiwa ni pamoja na Mahakama
Kuu Kanda ya Mwanza, Tabora, Dodoma na kadhalika.
Mahakama ya Tanzania
kupitia Mpango Mkakati wake imejiwekea nguzo kuu tatu moja ya nguzo hizo ni ya Kurejesha
imani ya jamii na Ushirikishwaji wa Wadau ambapo kupitia nguzo hii
Mahakama inafanya jitihada mbalimbali ili
wananchi waweze kujua zaidi huduma na maboresho yanayojiri kwa manufaa ya
wananchi kwa kuwa wao ndio wadau wakubwa wa Mhimili huu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza na wananchi
(hawapo pichani) wakati wa uzinduzi rasmi wa programu maalum ya Kanda hiyo ya
kuzungumza na wateja wake.
Wananchi wakimsikiliza
kwa makini, Mhe. Jaji Mugeta (hayupo pichani) alipokuwa akizindua rasmi
programu ya utoaji elimu kwa wananchi/wateja wa Mahakama Kanda ya Dar es
Salaam.
Naibu Msajili Mfawidhi,
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza na
Wananchi waliokuwepo wakati wa hafla hiyo, waliosimama nyuma ni baadhi ya
Watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Naibu Msajili, Mahakama
Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza na Wananchi
waliokuwepo wakati wa hafla hiyo.
Baadhi ya Maafisa wa
Mahakama walioshiriki katika hafla hiyo wakiwa wamejumuika pamoja na wananchi,
wa pili kulia ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Said
Ding’ohi na mwenye koti jeupe ni Bi. Wanyenda Kutta, Mkurugenzi
Msaidizi-Utawala, Mahakama ya Tanzania.
Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Dar es Salaam akisalimiana na wananchi mara baada ya kuzindua rasmi
zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wanaofika kupata huduma katika Kanda hiyo.
Mhe. Jaji Mugeta alimuwakilisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama ya Tanzania)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni