Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Imani Aboud, amezindua
mfumo wa kielekitroniki wa kuhifadhi taarifa na nyaraka mbali za maktaba (E-Library)
pamoja na mfumo wa matangazo kwa njia ya kielekroniki (Public address system) utakaotumika
kuwatangazia wadaawa na wadau huduma mbalimbali zitolewazo Mahakamani.
Kufuatia
uzinduzi huo, ni dhahiri kuwa sasa Mahakama ya Tanzania imedhamiria kuingia
kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli
zake ili kurahisisha suala zima la upatikanaji wa haki kwa wakati.
Akizindua
mifumo hiyo, Jaji Aboud alisema mradi wa maboresho ya Maktaba ya Mahakama kuu ulikamilika
Julai 13 mwaka huu baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa ulioanza mwezi Juni 2018
ambapo mradi huu umewezesha kuanzishwa kwa mfumo wa E- Library unaosajili aina
zote za vitabu na nyaraka mbalimbali zinazopokelewa Maktaba.
Kupitia
mfumo mpya wa maktaba, orodha au idadi ya vitabu vinavyopatikana ndani ya Maktaba
hiyo na sehemu ambapo vitabu hivyo vimehifadhiwa huweza kuonekana ikiwa ni
pamoja na taarifa na tarehe ya kuazima
kitabu na siku ya kurudishwa.
Kuhusu
mfumo wa matangazo kwa njia ya kielekroniki, Jaji Aboud alisema Mfumo huo utawasaidia wananchi wanaofika Mahakamani
kufahamu kinachoendelea wakati wakisubiria kuitwa kwenye vyumba vya mashauri
muda ukifika.
Aidha,
matangazo ya kuitwa kwenye vyumba vya mashauri yatakuwa yakitolewa na wasaidizi
wa kumbukumbu kupitia simu maalum kumi (10) zilizofungwa kwenye ofisi zao
na kuwafikia wadaawa wanaosubiria kwenye
ukumbi maalum (waiting shade) na washtakiwa
wanaohifadhiwa kwenye vyumba vya Mahabusu kupitia vipaza sauti vya kisasa.
Katika Mfumo huu zimewekwa
simu 10 za kutangazia zilizofungwa katika kila Ofisi ya katibu muhtasi wa Jaji,
Ofisi za Masjala na Ofisi za Makatibu Muhtasi wa Mahakimu. Pia vimefungwa
vipaza sauti vitatu (3) vya kuwatangazia wadaawa wanaoketi kwenye ukumbi wa
kusubiria kuitwa shaurini na washtakiwa wanaohifadhiwa vyumba vya Mahabusu.
Afisa Tehama wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga, Amina Ahmad akimuelezea Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud na watumishi wengine wa Mahakama jinsi mfumo wa E-Library unavyofanya kazi wakati wa uzinduzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Iman Aboud akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Maktaba ya kielekitroniki iliyoanzisha na kanda ya Tanga.
Afisa Tehama wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga, Amina Ahmad akifafanua kuhusu mfumo wa E-Library.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni