Na
Mary Gwera
MTENDAJI, Mahakama Kuu
Divisheni ya Biashara, Bw. Willy Machumu amewataka Watumishi wa Divisheni hiyo kuacha
kufanya kazi kwa mazoea bali kufanya kazi kwa malengo kwa kutoa huduma nzuri
zitakazowaridhisha wateja.
Bw. Machumu aliyasema
hayo Agosti 10, alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo ya siku moja kuhusu Mahusiano
kati ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama na Tathmini ya Utendaji kazi
(OPRAS) katika Ukumbi wa Mahakama ya Biashara.
Mtendaji huyo alisema
ili kufanya kazi kwa matokeo zaidi aliona ni vyema kuhuisha malengo ya Mfumo wa
Utendaji (OPRAS) na malengo ya Mpango Mkakati unaotekelezwa na Mahakama kwa
sasa.
“Lengo kuu la kufanya
hivi ni kushirikisha Watumishi wa kila Kada ili kuona umuhimu wa kufanya kazi
ili kwa pamoja kama Taasisi tuweze kufikia malengo makuu mojawapo ikiwa ni kuongezeka kwa kiwango
cha wananchi kuridhika na huduma zitolewazo na Mahakama,” alieleza Bw. Machumu.
Kwa upande wake, Mchumi
Mwandamizi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Geofrey Mashafi ambaye alishiriki katika
Mafunzo hayo kuwakumbusha Watumishi kuhusu Mpango Mkakati alisema kuwa Mahakama
ya Biashara inayo jukumu kubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
“Kama mnavyofahamu
jukumu kuu la Mahakama hii ni kushughulika na utatuzi wa migogoro ya kibiashara
ili kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji nchini kwa lengo la kuongeza
nafasi za ajira na kukuza uchumi wa nchi,” alisema Bw. Mashafi wakati akitoa
mada kwa Watumishi wa Mahakama hiyo.
Bw. Mashafi alisema
kuwa mahusiano ya Mpango Mkakati na OPRAS hayawezi kutenganishwa kwani
viashiria vilivyowekwa kupima utekelezaji wa Mpango Mkakati haviwezi kupimika
kwa ujumla ila kwa kupima utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja.
Pichani ni Mtendaji,
Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bw. Willy Machumu akiongea na Watumishi wa
Divisheni hiyo (hawapo pichani) alipokuwa akifungua Mafunzo hayo.
Mchumi Mwandamizi,
Mahakama ya Tanzania, Bw. Geofrey Mashafi akitoa Mada kuhusu Mpango Mkakati kwa Watumishi wa Mahakama ya Biashara.
Naibu Msajili, Mahakama
Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Angelo Rumisha akiongea jambo na Watumishi.
Watumishi wakisikiliza
kwa makini.
(Picha na Mary Gwera)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni