Na Prisca Libaga, Maelezo, na Catherine Francis, Mahakama Kuu Arusha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kuwa
kisiwa cha amani na utulivu kutokana na
kufuata utawala wa sheria na kujali haki za binadamu.
Akizungumza kwa niaba ya Rais, Mhe. Dkt
John Pombe Magufuli katika hafla ya
kuapishwa kwa Majaji watatu wapya wa Mahakama
ya Afrika ya Haki za Binadamu (AFCHPR), jana jijini Arusha, Makamu wa
Rais alisema Tanzania itaendelea kuwa mfano wa kuigwa dhidi ya mataifa mengine
kutokana na kujali haki za binadamu.
“Tumejitahidi kuifanya Tanzania kuwa
ni mfano wa kuigwa na nchi zingine katika haki za binadamu na ndiyo maana hali ya amani
na utulivu imeendelea kuwepo kwa kuwa tumekuwa tukifuata utawala wa
sheria,”alisema.
Alisema mbali na Serikali ya
Tanzania kukubali kutoa jengo linalotumiwa na Mahakama hiyo kuendeshea kesi
zake, pia imeendelea kutoa misaada mbalimbali ikiwemo kiwanja kwa ajili ya
kujenga jengo lake la kudumu.
“Katika kuonyesha tunathamini Mahakama
hii, hata watendaji wetu wamekuwa wakitembelea mara kwa mara Mahakama hii, na hivi
majuzi tu hapa Mwanasheria Mkuu na Mwendesha mashtaka Mkuu wa Serikali
walitembelea Mahakama hii na kufanya mazungumzo na Rais, natumaini na viongozi wengine
katika nchi nyingine na wao watafanya hivyo,”alisema.
Kwa upande wake Rais wa Mahakama
hiyo Jaji Mhe. Sylvain Ore aliwakaribisha Majaji watatu walioteuliwa katika Mahakama
hiyo na kuwataka kutenda haki katika kutoa maamuzi bila kufanya upendeleo
wowote.
Alisema majaji hao walichaguliwa
katika mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika hivi karibuni mjini Nouakchott nchini
Mauritania kufuatia kupendekezwa na nchi zao baada ya majaji watatu waliokuwa
wakihudumu mahakamani hapo kustaafu.
Majaji waliokula kiapo jana ni
pamoja na Jaji Imani Daudi Aboudi wa Tanzania
aliyechukua nafasi ya Jaji Solomy
Balungi Bossa wa Uganda ambaye aliachia nafasi hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Jaji
wa Mahakama ya kimataifa ya Haki za binadamu (ICC).
Wengine waliokula kiapo ni Jaji
Stella Isibhakhomen Anukam wa Nigeria na Jaji
Blaise Tchikaye wa Kongo ambao kwa pamoja
wamechukua nafasi za majaji Gerald Niyungeko kutoka Burundi pamoja na Jaji El
Hdji Guisse kutoka Senegali ambao wamestaafu baada ya kutumikia Mahakama hiyo
kwa vipindi viwili vya miaka sita.
Awali akitoa salamu katika hafla
hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya Umoja wa Afrika inayoshughulikia masuala ya rushwa,
Dkt Begoto Miarom alisema rushwa ni janga la kimataifa ambalo limekuwa
likififisha uchumi wa nchi nyingi barani humu.
Alisema pamoja na changamoto nyingi
za mapambano dhidi ya rushwa, bado
ushirikiano wa hali ya juu unahitajika kutoka
kwa wakuu wa nchi za umoja wa Afrika katika kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande wake Jaji mpya mteule
kutoka Tanzania Jaji Imani Aboud alisema
kuteuliwa kwao sasa kumefanya Majaji wanawake
wa Mahakama hiyo kufikia sita huku wanaume wakiwa watano jambo ambalo amesema ni
faraja kwao na kwamba hiyo inaonyesha namna jinsia inavyozingatiwa katika Mahakama
hiyo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika na
Haki za Binadamu Mhe. Jaji Sylvain Ore.
Pichani
ni Mhe. Jaji Iman Aboud wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyeapishwa kuwa Jaji
wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu.
Majaji
walioapishwa, kushoto ni Mhe. Jaji Blaise Tchikaya kutoka Kongo, katikati ni Mhe. Jaji Stella
Anukam kutoka Nigeria na kulia ni Mhe. Jaji Iman Aboud kutoka Tanzania.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
akizungumza katika hafla hiyo ya Uapisho.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Augustine Mahige katika hafla hiyo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea
zawadi kutoka kwa Rais wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu, Mhe.
Jaji Sylvain Ore.
Majaji wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa
Rais (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Afrika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni